Baraza
la Habari Tanzania (MCT), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)
na Mtandao wa Haki za Binadamu Tanzania ( THRDC) leo Jumatano ya Januari
11, 2017 wamefungua kesi ya kuipinga Sheria Mpya ya Huduma za Vyombo
vya Habari namba 12 ya mwaka 2016 katika Mahakama ya Afrika Mashariki
(EACJ).
Akizungumza
na waandishi wa habari baada ya kufunguliwa kesi hiyo, Katibu Mtendaji
MCT, Kajubi Mukajanga amesema washirika waliofungua kesi hiyo wanataka
baadhi ya vifungu vya sheria vinavyokandamiza uhuru wa habari na
kujieleza vifutwe kwakuwa vinakiuka matakwa ya mkataba wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC).
Na kwamba mahakama ya EACJ imepewa mamlaka ya kutafsiri mkataba huo na kuhakikisha nchi wanachama wanaufuata na kuusimamia.
“Vifungu
hivyo vya sheria vinakandamiza uhuru wa habari na wa kujieleza, vifutwe
kwani vinakiuka matakwa ya mkataba wa EAC ambao unataka nchi mwanachama
kuzingatia na kulinda haki ambazo zimeelezwa katika mkataba huo kwenye
ibara ya 6(d) na 7(2),” amesema.
Amesema
kuwa, Ibara ya 6(d) ya mkataba wa EAC inahimiza umuhimu wa kufuata
kanuni za utawala bora, wa kidemokrasia, sheria, uwajibikaji, uwazi na
haki kwa wote ikiwa pamoja na usawa wa kijinsia, kulinda na kuheshimu
haki za binadamu.
“Kama
ilivyo kwenye kifungu cha 8(1) (c), Tanzania inatakiwa kuchukua hatua
za kuhakikisha haki zote zinazotajwa katika mkataba huo zinafuatwa na
kutekelezwa,” amesema.
Mkurugenzi
Mtendaji wa LHRC, Helen Kijo-Bisimba amesema baadhi ya vifungu vya
sheria hiyo vinakiuka haki za binadamu na kwamba wameshiriki kufungua
kesi hiyo ili kuipinga sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari.
“Sheria imekaa sivyo, tumeona tuungane na wenzetu ili kuipinga sheria hii,” amesema.
Mkurugenzi
wa THRDC, Onesmo Olengurumwa amesema sheria inabidi ibadilishwe hasa
katika vifungu kandamizi kabla ya kuanza kutumika.
“Kuna
mazingira yatakayowaweka katika mazingira magumu waandishi wa habari,
ni vyema kuipinga sheria hii isitumike hadi ibadilishwe.”
0 comments :
Post a Comment