Polisi
wameingilia kati mvutano ndani ya Kanisa la Anglikana baada ya kumzuia
Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Dkt. Valentino Mokiwa kushiriki
ibada ya kumsimika Askofu mpya wa Dayosisi ya Lweru.
Askofu
Mokiwa amekuwa katika mvutano na Askofu Mkuu wa Anglikana Tanzania,
Dkt. Jacob Chimeledya tangu alipotangaza kumvua uongozi wa Dayosisi ya
Dar es Salaam, akidai mkuu huyo hakufuata utaratibu na kwamba hana
mamlaka ya kuchukua uamuzi huo.
Aidha
Askofu Mokiwa aliwasili makao makuu ya Dayosisi ya Lweru mjini Muleba
mkoani Kagera na alitarajiwa kuungana na maaskofu wengine kumsimika
Godfrey Mbelwa kuwa askofu mpya wa dayosisi hiyo.
Lakini
taarifa zilizopatikana zimesema Askofu Mokiwa alichukuliwa na polisi
na kuhojiwa katika kituo cha Muleba, kutokana na kuhofu kuwa kuwapo
kwake kungeweza kusababisha vurugu katika ibada iliyokuwa iongozwe na
Dkt. Chimeledya kutokana na mvutano uliopo.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kagera Augustino Ollomi,amesema kuwa jeshi hilo
halikumkamata Askofu Mokiwa na kumhoji, badala yake amesema walichukua
hatua haraka baada ya kupata taarifa za kiintelijensia kuhusu masuala ya
usalama.
“Ni
wajibu wetu kufuatilia, tulimuonya kuhusu suala la kuhudhuria ibaada
kwa sababu kulikuwa na viashiria vya uvunjifu wa amani lakini ilikuwa ni
hiari yake kutohudhuria, huo utakuwa ni uamuzi wake,” amesema Ollomi.
Kamanda
Ollomi amesema walimuita Askofu Mokiwa juzi saa moja usiku kwa ajili ya
kumpa ushauri wa kutohudhuria sherehe hizo kwa kuwa mgogoro uliopo
katika kanisa hilo ungeweza kusababisha uvunjifu wa amani.



0 comments :
Post a Comment