Kikao
cha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Tanzania na
Malawi kimeweka mazingira mazuri ya kushughulikia mgogoro wa mpaka
katika Ziwa Nyasa ambapo juhudi za kutafuta suluhu zilisimama kutokana
na mabadiliko ya uongozi nchini Malawi.
Kauli
hiyo ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Dkt, Augustine Mahiga (Mb) wakati alipokuwa anasoma hotuba ya
kufunga kikao hicho jijini Lilongwe siku ya Jumapili tarehe 05 Februari
2017.
Mhe.
Waziri alieleza kuwa kikao hicho kimefanyika kufuatia maelekezo ya
Waheshimiwa Marais wa Tanzania na Malawi ambao walifanya mazungumzo
walipokuwa Ethiopia katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika
na kutoa wito kwa jopo la viongozi wa zamani wa Jumuiya ya Maendeleo ya
Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kuongeza kasi ya kutafuta suluhu ya
mgogoro huo.
Jopo
la viongozi wa zamani wa SADC lililopewa dhamana ya kushughulikia suala
hilo linaundwa na Mhe. Joachim Chissano, Rais wa zamani wa Msumbiji;
Mhe. Thabo Mbeki, Rais wa zamani wa Afrika Kusini na Mhe. Festus Mogae,
Rais wa zamani wa Botswana.
Waziri
Mahiga alieleza kuwa japo Tanzania na Malawi zinatofautiana katika
mpaka wa Ziwa Nyasa lakini tofauti hizo sio kikwazo kwa nchi hizo
kushirikiana katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya faida ya wananchi wa
pande zote mbili.
Alisema
kikao hicho cha JPCC kinatoa fursa kwa pande mbili kujadili na
kukubaliana maeneo mbalimbali ya ushirikiano na kuweka utaratibu wa
utekelezaji.
Aidha,
katika kikao cha JPCC, wajumbe wanakitumia kubuni mikakati ya
kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa maeneo ya
ushirikiano yaliyoafikiwa.
“Nafurahi
kusikia mmejadili na kukubaliana maeneo mengi ya ushirikiano ikiwemo
biashara, kilimo, utalii, tehama, utangazaji, utunzaji wa mazingira na
usafiri wa anga”. “Ni jambo la kupongezwa katika majadiliano yenu pia
mmependekeza iundwe Kamati ya Makatibu Wakuu ambayo itakuwa inakutana
kila baada ya miezi sita ili kutathmini utekelezaji wa maeneo
yaliyoafikiwa kwa mujibu wa muda uliokadiriwa”.
Mhe.
Mahiga alitoa maelezo namna Serikali ya Awamu ya Tano inavyoboresha
miuondombinu ya Bandari ya Dar Es Salaam, barabara na mipango ya
kuboresha Reli ya TAZARA kwa kushirikiana na China ili Malawi iweze
kusafirisha bidhaa zake kwa urahisi.
“Ni
jukumu letu na pia ni wajibu wa kimataifa kuzihudumia nchi zisizokuwa
na bandari. Hivyo, Tanzania ambayo imezungukwa na nchi nane zisizokuwa
na bandari itaboresha miundombinu ili nchi hizo ziweze kusafirisha
bidhaa zao bila usumbufu wowote.
Kwa
upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Mhe. Francis Kasaila
alisisitiza umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya bandari, barabra na
reli ili Serikali ya Malawi na wafanyabiashara waweze kusafirisha bidhaa
kwa urahisi.
Alisema
ili vituo vya mizigo vya Malawi vilivyopo Dar es Salaam na Mbeya
vifanye kazi kwa ufanisi hakuna budi kuboresha Bandari ya Dar es Salaam,
Reli ya TAZARA, barabara ya Dar es Salaam hadi Mbeya na kujenga Kituo
cha Pamoja cha kutoa Huduma mpakani.
Kikao
hicho kilimalizika kwa kushuhudiwa uwekaji saini wa mikataba ya
makubaliano katika Mashauriano ya kisiasa na kidiplomasia na usafiri wa
anga.
Mhe.
Waziri kabla ya kurejea Dar es Salaam siku ya Jumatatu amepangiwa miadi
ya kuonana na Rais wa nchi hiyo, Mhe. Prof. Peter Mutharika ambapo
amepanga pamoja na mambo mengine kujadili suala la Watanzania wanane
wanaoshikiliwa katika gereza kuu la Mzuzu kwa tuhuma za kuingia kinyume
cha sheria katika mgodi wa urani wa Kayerekera.
Imetolewa na: Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki
Tarehe 06 Februari 2017



0 comments :
Post a Comment