Mwenyekiti wa Chama cha wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba
amekanusha tuhuma za kuwa na ukaribu unaotia shaka kati yake na serikali
na kutolea ufafanuzi ishu mbalimbali zinazoashiria ukaribu huo ikiwemo
ya kuchepusha ruzuku ya chama.
Mwenyekiti huyo anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa amesema
kinachodaiwa kuwa ni ukaribu wake na serikali, siyo sahihi kwa kuwa yeye
huwa anaalikwa tu kwenye matukio mbalimbali ya kitaifa ambayo hawezi
kukataa mwaliko.
"Kwa mfano ukikaribishwa kwenye shughuli ya serikai, labda Rais
anazindua kitu, au sherehe za kitaifa na Rais yupo utakataaje" Amesema
Lipumba.
RUZUKU
Suala la ruzuku ya chama hicho kuchepushwa pia ni jambo linalodaiwa kuwa
ushahdi wa Prof Lipumba kuwa karibu zaidi na serikali, ambapo amesema
ilikuwa ni lazima iwe hivyo kutokana na uamuzi wake kama Mwenyekiti wa
chama wa kutengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Fedha, ambaye ndiye aliyekuwa
mtia sahihi katika masuala ya fedha.
Pia sababu nyingine ya kuchepusha fedha za ruzuku amesema ni mahitaji ya
chama kwa kuwa kilikuwa kinaingia kwenye uchaguzi hivyo kilihitaji
fedha kwa ajili ya shighuli mbalimbali.
" Kuhusu ruzuku, nilikuwa nimetengua uteuzi wa mkurugenzi wa fedha,
bwana Bashange, kwahiyo hakuwa tena signatory wetu, kwa nafasi yangu
kama mwenyekiti niliona hafai, tukajitahidi kufungua akaunti nyingine
lakini haikuwezekana. Ikabidi Naibu Katibu Mkuu ambaye ndiye anayeshika
nafasi ya Katibu Mkuu anapokuwa hayupo ofisini, aandike barua ya kuomba
ruzuku kwa ajili ya mahitaji tuliyokuwa nayo" Ameeleza Lipumba
Lipumba ameendelea kusema "Tukapeleka taarifa kuomba ruzuku. Kwahiyo
Naibu Katibu Mkuu akaandika barua kwenda kwa Msajili kuwa tunaomba
ruzuku na ipitie kwenye akaunti nyingine, na hilo likafanyika"
MIKUTANO
Kuhusu yeye kuruhusiwa kufanya ikutano, huku Katibu Mkuu wake
akizuiliwa, hususani tukio lililotokea mkoani Mtwara, Lipumba amesema
hata yeye alipokwenda Mtwara hakuruhusiwa kufanya kilichokuwa
kimempeleka, na badala yake aliishia kufanya mikutano ya ndani, huku
akibainisha kuwa kilichomkwamisha Maalim Seif ni kwenda bila kutoa
taarifa kwa kiongozi wa wilaya.
"Nimekwenda Mtwara, nilikaribishwa na viiongozi wa wilaya, kazi yangu
ilikuwa ni kufungua matawi, lakini polisi wakanizuia kuwa sitakiwi
kufanya mikutano ya nje, nikafanya mikutano ya ndani...Lakini Maalim
Seif alikwenda bila kumtaarifu kiongozi wa wilaya". Amesema
ULINZI
Lipumba aliyekuwa katika mahojiano na kituo kimoja cha TV, amekanusha
taarifa za kupewa ulinzi na serikali na kufafanua tukio la kupigiwa
saluti na askari, akisema kuwa siku hiyo hakupigiwa yeye saluti bali
diwani wa eneo ambalo yeye alishiriki kufanya usafi.
"Pale Buguruni, tulikuwa katika usafi, na tulikuwa na diwani wa eneo
lile, askari walikuwa wakiangalia usalama, na alipotokea diwani wa eneo
lile, askari walimpigia yeye kwa kuwa ndiye mkuu wa eneo lile, siyo
mimi"
Katika hatua nyingine, amesema anaendelea kumtambua Maalim Seif kama
Katibu Mkuu halali wa CUF, huku akimtaka amfuate ili wamalize tofauti
zao na kufanya kazi kwa pamoja.
0 comments :
Post a Comment