Wapigakura
wanne wa Jimbo la Bunda waliofungua shauri kupinga matokeo ya Uchaguzi
Mkuu uliopita wameendelea kumng’ang’ania mbunge wa jimbo hilo, Ester
Bulaya kwa kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu wa kutupa maombi
yao.
Msajili
wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Francis Kabwe alisema jana kuwa rufaa
ya wapigakura hao, Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na
Acetic Malagila iliyosajiliwa kwa namba 199 ya mwaka 2016, itasikilizwa
mfululizo kuanzia Februari 20.
Alisema
rufaa hiyo itasikilizwa jijini Mwanza na jopo la majaji watatu wa
Mahakama ya Rufani, Salim Mbarouk, Augustine Mwarija na Shabani Lila.
Katika
maombi ya msingi waliyofungua Mahakama Kuu, wapigakura hao
wanaowakilishwa na Wakili Constantine Mutalemwa, wanaiomba Mahakama
kutengua ushindi wa Bulaya dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Stephen
Wasira kwa madai kuwa uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka 2015 haukuwa huru na
wa haki.
Pamoja
na madai mengine, Masato na wenzake wanadai kuwa mchakato wa kampeni,
upigaji kura na utangazaji wa matokeo uligubikwa na ukiukwaji wa sheria
na utaratibu wa uchaguzi, vikiwamo vitendo vya rushwa, msimamizi wa
uchaguzi kumnyima haki Wasira kwa kukataa ombi lake la kura kuhesabiwa
upya.
Hoja
nyingine ni msimamizi wa uchaguzi kutangaza matokeo bila Wasira kuwapo
ukumbini na kuchanganya tarakimu za idadi ya wapigakura walioshiriki
uchaguzi.
Novemba
17, mwaka jana, Jaji Noel Chocha wa Mahakama Kuu alimtangaza Bulaya
kuwa mshindi halali wa uchaguzi huo baada ya kutupilia mbali maombi ya
wapigakura hao.



0 comments :
Post a Comment