DAR ES SALAAM: Msala tena! Baada ya mwanaye kukamatwa na kushtakiwa kwa tuhuma za kutumia madawa ya kulevya, kuhama chama na juzikati nyumba yake kupigwa mawe kwa muda mrefu na watu wasiojulikana, Miriam Sepetu, mama mzazi wa muigizaji Wema Sepetu, amejikuta mikononi mwa polisi, Risasi Jumamosi linakupa mchapo kamili.
Chanzo cha uhakika kimelidokeza gazeti hili kuwa mama huyo amejikuta mikononi mwa polisi baada ya kufikishwa Kituo cha Polisi Oysterbay, akidaiwa kumtapeli mfanyabiashara Alex Msama, kiasi cha fedha kinachotajwa kufikia shilingi milioni 16.
Wema Sepetu
“Mama Wema alipatwa na matatizo, akataka kuuza nyumba yake ile ya Sinza Lion, sasa katika kutafuta wateja akakutana na Msama, lakini Msama akamwambia kwa wakati ule alikuwa hana hela, lakini kuna mkopo wake katika benki moja ulikuwa umeiva, hivyo avute subira kidogo angeinunua nyumba hiyo (bei haijatajwa).
“Wakakubaliana, sasa mama akamwambia Msama hata hivyo ana shida kidogo ya hela, basi jamaa akawa anampa mara leo milioni mbili, mara tatu hadi zikafika hizo 16, lakini ghafla Msama akaja kusikia ile nyumba imeshauzwa kwa mtu mwingine, alipofuatilia akakuta ni kweli, kumuuliza mama akawa haeleweki hadi jamaa akaamua kwenda polisi,”kilisema chanzo hicho.
Msama
Ili kuweka sawa mambo hayo, Risasi Jumamosi lilifika nyumbani kwa mama Wema, Sinza Mori Jumanne iliyopita, lakini lilizuiwa kuingia ndani kwa maelezo kutoka kwa mlinzi kuwa mama hakuhitaji kuonana na mtu yeyote siku hiyo. Kesho yake, alipigiwa simu yake ya mkononi na akaipokea, lakini mwandishi alipojitambulisha na kuanza kumsomea tuhuma hizo, alisema hana muda wa kuzungumzia jambo hilo kabla ya kukata simu.
Wema na mama yake.
Kwa upande mwingine, Risasi Jumamosi lilifika ofisini kwa Alex Msama, iliyopo Kinondoni Block 41, lakini mfanyabiashara huyo hakuwepo. Mmoja wa maofisa wa ofisi hiyo, ambaye alikataa utambulisho wake kwa kuwa siyo msemaji wa Kampuni ya Msama Promotions, alikiri kuwahi kumsainisha mama Wema kiasi cha shilingi milioni tatu. Hata hivyo, gazeti hili lilimfikia Msama kwa njia ya simu yake ya mkononi na alipoulizwa kuhusu madai hayo, alisema;
“Ni kweli nimetapeliwa na mama Wema, lakini kwa kuwa jambo hili nimeshalifikisha polisi, nadhani mkondo wa sheria utafuatwa,” alisema na kuomba asilizungumzie zaidi suala hilo. Jalada la shauri hilo limefunguliwa katika kituo cha Polisi Oysterbay kwa namba OB/RB/3358/2017.
0 comments :
Post a Comment