Paul Makonda Awaige Zitto na Luhende Utata wa Vyeti vya Elimu




Mwaka 2005, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, akiwa kijana mdogo, alipewa changamoto kuhusu elimu yake, wakati akigombea jimbo la Kigoma Kaskazini, kwa tiketi ya Chadema.

Aliyempa changamoto hiyo ni aliyekuwa mgombea kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, Lazaro Matete. Katika mikutano yake, Matete alisema Zitto hajasoma na kwamba alikuwa anawadanganya wapigakura wa Kigoma Kaskazini.

Zitto alikata mzizi wa fitina kwa kuweka wazi vyeti vyake. Matete alikosa hoja nyingine na baada ya Zitto kuanika ukweli wake, haujawahi kuwepo mjadala mwingine wowote kuhusu elimu ya Zitto.

Hivi ndivyo Makonda anatakiwa kuwakata vilimilimi wote wanaomsema kuwa yeye siyo Paul Christian bali jina lake halisi ni Daud Albert Bashite. Makonda akifanya alivyofanya Zitto mbona mambo yatakuwa kimya? Wanaomsema leo hawatakuwa na hoja nyingine.

Upo mfano wa pili; mwaka jana Rais Magufuli alipoteua wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali nchini, aliyeteuliwa kuwa mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi, Luhende Pius, alisemwa kuwa aliishia kidato cha nne na kwamba alikuwa meneja wa Hoteli ya City Style, Sinza, Dar es Salaam.

Hivyo ndivyo ilivumishwa. Ikawa gumzo hasa kwenye mitandao ya kijamii. Hata hivyo, Rais Magufuli alikata mzizi wa fitina na kuuchimbua kabisa kwa kuonesha hadharani vyeti vya Luhende.

Rais Magufuli alisema: “Huyo mnayemsema ni wa kwenu, ninayemfahamu na niliyemteua ana master (shahada ya uzamili).” Baada ya hapo Luhende aliweka wazi cheti chake, kamera za vyombo vya habari zikarekodi. Ubishi ukaishia hapo.

Ndivyo ambavyo Makonda anapaswa kufanya. Unajua njia ya uongo ni fupi. Ikiwa yote yanasemwa ni kumsingizia, basi atokeze aweke wazi vyeti vyake. Aseme alisomea wapi darasa la kwanza mpaka alipofikia na kwa majina yapi. Akate mzizi wa fitina.

Rais Magufuli hana kupindapinda, ndiyo maana suala la Luhende japo halikuwa kubwa, lakini aliamua kulitolea ufafanuzi. Hili la Makonda limekuwa kubwa mno. Ufafanuzi wake unahitajika.

Kwa hiyo, Makonda akiwaiga Zitto na Luhende na kufanya kama wao walivyofanya, utata wote kuhusu tuhuma kuwa alighushi cheti cha kidato cha nne, utakwisha.

Ndimi Luqman MALOTO
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment