Jeshi LaPolisi Laendeleza Msako Walioua Askari Pwani

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu akiongea.

PWANI: Ngoma ni mbichi mkoani Pwani hususan katika Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji baada ya polisi wanane kuuawa kwa kupigwa risasi na wahalifu wanaotumia silaha za kivita, Uwazi limetembelea.

Mwandishi wetu aliyekuwa katika wilaya hizo anaripoti kwamba, hali ni tete kutokana na tukio hilo kwani sasa wakazi wa eneo hilo wana wasiwasi mkubwa baada ya wauaji hao kutekeleza mauaji yao bila kuwa na lengo la kuiba mali au fedha.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili mjini Kibiti huku wakiomba majina yao kuhifadhiwa, walisema watu kadhaa wamekuwa wakikamatwa na polisi ambapo Jumapili ya Pasaka, Uwazi lilishuhudia watu wanne waliokuwa wamevaa kanzu wakiwa ndani ya gari la polisi lililokuwa likiliza king’ora, wakashushwa Kituo Kikuu cha Polisi Kibiti.

Hakuna polisi aliyekuwa tayari kusema watu hao walikuwa nani na kwa nini walikimbizwa kituoni hapo kwa gari la polisi lililokuwa likiliza king’ora.
RPC wa Pwani, Onesmo Lyanga akiongea jambo.

WANANCHI WAZUNGUMZA NA UWAZI
Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliozungumza na Uwazi kwa sharti la kutoandikwa majina yao gazetini walidai kwamba, wamekuwa wakiishi kwa wasiwasi mkubwa kwani kuna polisi wamekuwa wakiwapiga bila sababu za msingi na kusababisha raia kuogopa kutembea sehemu mbalimbali, ikiwemo kwenda mashambani.

“Hakuna siri, polisi wanapiga raia hovyo na wamekuwa wakali kana kwamba sisi ndiyo tulioua polisi wakati ukweli ni kwamba hata sisi viongozi wetu wameuawa na wahalifu hao,” alilalamika mwananchi mmoja.

Mwananchi mwingine alidai kuwa, kwa sasa kuendesha pikipiki ‘bodaboda’ katika maeneo ya kuanzia Mkuranga, Mwarusembe, Kibiti hadi Ikwiriri ni hatari kwa sababu wakikutwa na polisi wanakamatwa.

Askari wakiangalia kitu chini.

UKAGUZI WA MAGARI USIKU
Uwazi likiwa kwenye gari mwishoni mwa wiki iliyopita, saa 1:30 usiku lilishuhudia kizuizi cha barabarani karibu na Kijiji cha Mwarusembe, Kibiti ambapo kulikuwa na askari polisi zaidi ya 30 waliokuwa wamepelekwa hapo kukagua kila gari lililokuwa likipita kutoka Lindi kwenda Dar au kutoka Dar kwenda Lindi.

Basi dogo lililopandwa na Uwazi mara baada ya kusimama, polisi walimvamia dereva na kumhoji huku wengine wakidai kwamba inawezekana aliwabeba wahalifu. Hata hivyo, mkuu wao aliyekuwa na nyota mbili alijitokeza na kuruhusu basi hilo kuondoka baada ya kukaguliwa ndani.

MADUKA YAFUNGWA
Uwazi pia lilishuhudia maduka mengi yaliyopo kando ya barabara kuu ya Dar – Lindi kati ya Kibiti na Ikwiriri yakiwa yamefungwa saa 11 za jioni na walipoulizwa wenyeji wa Jaribu Mpakani sehemu ambayo aliwahi kuuawa Mkuu wa Upelelezi Kibiti, OC-CID, Peter Kubezya na watu wengine wawili, walisema wao siku hizi hulala saa 9 alasiri kuhofia kukamatwa na polisi.

“Kama mnavyoona, tumekuwa tukijifungia majumbani mapema, unaona maduka yote kuanzia Ikwiriri hadi hapa Mwarusembe Kibiti yamefungwa. Hii ni kwa usalama wetu lakini ukweli ni kwamba hatuna raha,” alisema mwananchi mwingine wa kijiji hicho.

Pia kuna habari kwamba, baadhi ya raia wema wamekuwa wakijisaidia ndani usiku kwa kushindwa kutoka kwenda vyoo vya nje wakihofia usalama wao kutoka kwa wahalifu hao ambao polisi wanawasaka usiku na mchana mitaani.
MAANDAMANO YALETA BALAA
Mwananchi mwingine wa Kibiti aliliambia Uwazi kwamba, maisha ya wananchi wa Jaribu Mpakani wilayani Kibiti ni ya hofu baada ya Jumamosi iliyopita, polisi kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatawanya wananchi waliokuwa wakiandamana, kitendo kilichosababisha mmoja kujeruhiwa.

Shuhuda huyo alisema tukio hilo lilitokea mchana baada ya wananchi wa eneo hilo kukaidi amri iliyotolewa na jeshi la polisi ya kuwataka kutawanyika baada ya kutaka kuandamana kwa kudai kwamba wanaonewa.

“Tulikuwa tukiandamana kupinga uonevu wa polisi tukiwa na matawi ya majani, tulipowaona polisi tulikimbia kunusuru maisha yetu kwa sababu walikuwa wakifyatua risasi za moto na mwenzetu mmoja zilimpata,” alisema shuhuda huyo.

Uwazi: “Huyo mwenzenu aliyepigwa risasi kwa sasa yupo wapi?”

Shuhuda: “Alichukuliwa na polisi na kupelekwa Hospitali ya Misheni ya Mchukwi. Alionekana kujeruhiwa mkononi jirani na kwapa.”

Uwazi: “Kuna mtu amefariki dunia katika tukio hilo?”

Shuhuda: “Hapana, labda sehemu nyingine tofauti na hapa.”

Uwazi: “Hali ikoje kwa sasa kijijini hapo?” Shuhuda: “Kwa kweli hali ni shwari lakini wananchi wana wasiwasi mkubwa na maisha yao.”

Uwazi: “Wana wasiwasi wa nini wakati polisi wenye silaha wapo kuwalinda?”

Shuhuda: “Ni kweli kuna ulinzi mkali eneo hili, lakini kwani huyo mwananchi aliyejeruhiwa na kukimbizwa hospitali ya Mchukwi, amejeruhiwa na majambazi? Ni polisi.”

WANANCHI NA WAHALIFU
Wakati wananchi wakilalamikia hilo, kuna madai kwamba, baadhi yao wamekuwa wakishirikiana na wahalifu hao kwa kuwaficha au kuwapa ushirikiano wa namna moja au nyingine hivyo kulifanya jeshi la polisi kupata wakati mgumu katika kuwasaka wahalifu na kulazimika kutumia akili ya ziada na sasa, wahalifu wamezidiwa nguvu.

KAMANDA WA POLISI PWANI
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, SACP Onesmo Lyanga alipopigiwa simu na Uwazi na kuulizwa hali ilivyo Mkuranga, Kibiti na Rufiji na juu ya mapambano hayo hakuthibitisha wala kukanusha.

“Matukio yote ya huko tunafuatilia,” alisema kwa kifupi kamanda huyo bila kutoa ufafanuzi zaidi.

KUTOKA HOSPITALI
Afisa mmoja wa Hospitali ya Misheni ya Mchukwi aliyejitambulisha kwa jina moja la Emmanuel alikiri kumpokea majeruhi aliyejeruhiwa kwapani kushoto kwa risasi ambapo alisema alivunjwa mbavu mbili pamoja na kuharibiwa pafu lake.

“Hivi sasa tunafanya mpango ili mgonjwa apelekwe Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi,” alisema.

Wilaya hizo za Mkoa wa Pwani zimekuwa zikikumbwa na matukio ya viongozi wa vijiji na watendaji pamoja na askari kuuawa hali inayozua hofu kubwa na kulifanya eneo hilo kutokuwa salama. Katika tukio la hivi karibuni, polisi wanane waliokuwa wakitoka zamu walishambuliwa kwa risasi na watu waliokuwa wamejificha kichakani kando ya barabara.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba akiwa eneo la tukio walipouawa polisi nane Kibiti Mkuranga.

TUJIKUMBUSHE
Mei, 2016: Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunda, Saidi Mbwana aliuawa kwa kupigwa risasi, Oktoba 2016, aliyekuwa Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, Ally Milandu naye aliuawa kwa risasi, Novemba 2016, wenyeviti wawili wa vijiji hivyo waliuawa kwa risasi, Januari 19, 2017 Oswald Mrope wa Kitongoji cha Mkwandara aliuawa kwa risasi na wahalifu hao.

Matukio mengine; Februari 2017, wauaji walivamia nyumba ya Mwenyekiti wa Jaribu, Bakari Msanga, lakini alifanikiwa kutoroka, Februari 24, 2017, Ofisa Upelelezi Peter Kubezya na maofisa wa maliasili waliuawa kwa risasi, Machi 2017 polisi iliwaua watu watatu waliovaa kama wanawake walipojaribu kukwepa kizuizi cha polisi kwenye Daraja la Mkapa na Aprili 13, mwaka huu, polisi wanane wilayani Kibiti waliuawa na wahalifu hao.

Uwazi lina idadi ya polisi 17 kuuawa mkoani humo huku viongozi wa vijiji wakifikia hesabu ya 18
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment