Manara Aitunishia Msuli TFF

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara amepingana na maamuzi ya hukumu iliyotolewa jana na Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) dhidi yake na kusema kuwa ataendelea na shughuli zake za soka kama kawaida. 
Hukumu hiyo ilisomwa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Joseph Msemo ikiwa ni baada ya Manara kutofika kwa ajili ya mahojiano kwa madai kuwa alipata dharura ya kifamilia huko Zanzibar.
 
Akieleza kupingana na hukumu hiyo, Manara alisema kuwa TFF wameitoa hukumu hiyo bila yeye kusikilizwa na hakubaliani na jambo hilo kwani ni uonevu dhidi yake.
 
“Naitumikia Simba na barua waliyotuma TFF ni kupitia anwani ya timu, kwa hiyo sikuona ajabu viongozi kujibu kwani kweli nilikuwa na dharura, sasa cha kujiuliza waliogopa nini kunisubiri hadi Jumanne na hukumu wametoa jana (Jumapili)?” Alihoji.
 
“Bado nitaendelea kutumikia Simba na sitasita kufanya hilo, Malinzi (Rais wa TFF) na watu wake wanafanya haya kwa faida yao na sipo tayari kuona naonewa katika hili.” aliongeza
 
Akisoma hukumu hiyo, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Joseph Msemo alisema Manara alipatikana na makosa matatu tofauti. Kosa la kwanza likiwa ni kukashifu, kutuhumu na kuidhalilisha TFF, la pili kueneza chuki za ukabila na la tatu ni kuingilia utendaji wa TFF.
 
Kutokana na kupatikana na hatia, kamati hiyo imemwamuru Manara asijihusishe na shughuli za soka kwa miezi 12 na kulipa faini ya Sh9 milioni.
 
Hata hivyo, pamoja na hukumu hiyo, TFF bado imempa Manara nafasi ya kukata rufaa iwapo ataona kuwa hajatendewa haki katika hilo.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment