Uamuzi wa serikali kuhusu suala la kusafirisha mchanga wa madini kwenda nje ya nchi
utategemea ripoti ya kamati ya pili iliyoundwa na Rais Magufuli kuchunguza sakata hilo.
Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa ikiwa ni siku
moja tangu Kampuni ya Acacia ilipotaka kuundwa kwa kamati huru ya kuchunguza kiasi cha
madini kilichomo kwenye makinikia hayo.
“Sijui chochote kuhusu hao Acacia kuomba iundwe kamati huru , lakini tunasubiri ripoti ya kamati ya
pili iliyoundwa kuchunguza sakata hili wampelekee ripoti Rais,” alisema Msigwa.
Kamati ya awali iliyokuwa ikiongozwa na Prof. Mruma ambayo ilikabidhi ripoti yake Mei 24
mwaka huu ilionyesha kuwa kiwango cha madini yaliyomo kwenye makinikia hayo ni zaidi ya yale
ambayo hujazwa kwenye makabrasha.
Mbali na kuonekana kiasi kuzidi, lakini kamati hiyo ilibaini pia kuna madini makakati (strategic
metals) ambayo yamo kwenye makinikia hayo lakini hayakuwa yakitajwa na kampuni
zinazosafirisha mchanga nje jambo lililosababisha serikali kupata hasara ya mabilioni.
Kwa upande wao Acacia, walipinga ripoti hiyo na kusema wao hutangaza kila kitu kwa mujibu wa
sheria na kulipa tozo zote stahiki hivyo kuomba iundwe kamati huru kuchunguza upya kiasi cha
madini kwenye mchanga huo.

BE THE FIRST TO COMMENT

Leave a Reply

Your email address will not be published.

*