Rais John Magufuli leo wakati akizindua barabara ya Bagamoyo – Msata amefunguka na kuwachimba biti wanafunzi wa kike wa shule za msingi na sekondari kuwa kama wakipata mimba wakiwa shuleni basi wasahau kuendelea na masomo.
Rais Magufuli amesema kuwa katika kipindi cha utawala wake mwanafunzi yoyote ambaye atapata ujauzito akiwa shuleni hatakiwa kurudi shule hata baada ya kujifungua na kusema kama wakiruhusiwa kurudi shule wataharibu wanafunzi wengine.
“Kuna watu nimewasikia wanatetea wanafunzi kurudi shule baada ya kujifungua, yaani sisi unataka tusomeshe wazazi? Ndani ya utawala wangu kama Rais hakuna mwenye mimba atarudi shuleni kama akipata ujauzito, hawa watu tukiwaacha watazaaa mno, sababu huo mchezo ni mzuri.
Katika kipindi changu kama Rais ukipata mimba kwaheri na hao NGO wanaotetea kama wanataka wajenge wao shule za wazazi lakini si shule za serikali” alisisitiza Rais Magufuli
Mbali na hilo Rais Magufuli amewataka watanzania kuwa makini na kuendelea kulinda utamaduni wao na kusema kuwa haya mambo ya kuiga iga kila kitu yanaharibu utamaduni na kuleta matatizo zaidi.
“Kuna watu wengine wanatuletea mambo ya kubakana hapa, sijui ndoa ya jinsia moja, wewe toka lini umeona mwanaume na mwanaume wanaoana, hata wanyama hawafanyi hayo mambo, tuwe makini na hawa watu, wewe ulishawahi kuona Mbuzi anakosea ile sehemu? ” alisema Rais Magufuli