Dkt. Hassan Abas, Kulia ni uzinduzi wa Kamusi Kuu ya Kiswahili uliofanyika bungeni Dodoma

Serikali imetolea ufafanuzi matumizi ya neno “Mbashara” kuwa ndiyo neno sahihi lenye maana ya ‘inayorushwa hewani moja kwa moja au kuonwa kwa wakati huohuo kupitia redio na televisheni’ na siyo “Mubashara” kama ambavyo limekuwa likitumika na vyombo vingi vya habari.
Msemaji wa serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Dkt. Hassan Abbasi ametoa ufafanuzi huo leo wakati akikabidhi Kamusi Kuu ya Kiswahili kwa watumishi wa Idara ya Habari (MAELEZO) katika ofisi za Idara hiyo zilizopo Jijini, Dar es Salaam.
Ameitaka Idara ya Habari kuitumia Kamusi hiyo kama nyenzo muhimu katika kutangaza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi pamoja na kutumia misamiati mipya.
“Kamusi hii ina maneno mpaka yaliyoaanza kutumika hivi karibuni, kama vile bajaji. Pia ina misamiati mingi ambayo haitumiki, hivyo kwa kuitumia kamusi hii kutaongeza idadi ya misamiati ya Kiswahili kwa watumiaji wa lugha ya Kiswahili,” amesema Dkt. Abbasi.
Aidha ametoa mfano wa misamiati mingine iliyopo katika kamusi hiyo kuwa ni neno sharubati linalomaanisha kinywaji laini ambacho hutengenezwa kwa maji ya matunda au sukari na kisha kutiwa rangi. Neno lingine ni mnyange ambalo linamaana ya mtu mwenye mwonekano mzuri, maridadi, mtanashati, mrembo, mlimbwende.
Dkt. Abbas amewataka watumishi wa idara hiyo kuwa chemchem ya kutumia misamiati iliyoko katika kamusi hiyo ili kukuza lugha ya Kiswahili kwani mojawapo ya jukumu la idara hiyo ni kuhabarisha Umma, hivyo kamusi hiyo itakuwa msaada mkubwa katika uandishi wa habari za kila siku.
Kamusi Kuu ya Kiswahili ilizinduliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Juni 19, mwaka huu, Bungeni Mjini Dodoma