VYUO takribani 80 vinatarajiwa kushiriki maonesho ya elimu ya juu, sayansi na teknolojia yanayotarajiwa kufanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es salaam, kuanzia tarehe 26 mpaka 29 Julai, mwaka huu, anaandika Hellen Sisya.
Eleuther Mwageni, Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Vyuo vikuu hapa nchini (TCU), amewambia wanahabari leo kuwa maadhimisho hayo yatafanyika ikiwa ni kuenzi desturi ya TCU kama ambavyo imekuwa ikifanya kila mwaka.
“Mpaka sasa hivi tunatarajia vyuo kama 80, vya ndani na nje ya nchi. Lakini hayo ni matarajio tu. Wakija ndiyo tutakuwa na uhakika ni wangapi watakuja lakini tuna maombi ya ndani na nje ya nchim,” amesema Mwageni.
Awali, akizungumzia suala la udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu mwaka huu, Kaimu Mkurugenzi huyo amesisitiza kuwa maombi ya udahili yataanza kupokelewa rasmi kuanzia tarehe 22 mwezi huu katika vyuo vyote vikuu nchini.
Utaratibu wa wanafunzi kuomba kudahiliwa moja kwa moja katika vyuo husika ni mpya, ambapo katika miaka iliyopita wanafunzi walikuwa wakiomba vyuo kupitia TCU katika mfumo uliokuwa ukijulikana kama Central Admission System (CAS).
0 comments :
Post a Comment