Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amethibitisha kupokea barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad iliyomtaarifu kuhusu kuvuliwa uanachama wabunge wawili wa chama hicho, huku akisita kuchukua hatua.
Wabunge hao ni Magdalena Sakaya wa Kaliua mkoani Tabora na Maftaha Nachuma wa Mtwara Mjini ambao kwa mujibu wa barua hiyo, wabunge hao walivuliwa uanachama na kikao cha baraza kuu la chama hicho lililoketi hivi karibuni visiwani Zanzibar.
Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, mbunge anapovuliwa uanachama na taarifa kufikishwa kwa Spika, Spika anapaswa kutangaza nafasi ya mbunge husika kuwa wazi kwa kuwa anakuwa amepoteza sifa ya msingi ya kuwa mbunge.
Katika majibu yake, Spika Ndugai amesema kuwa anasita kuchukua uamuzi wowote kuhusu barua hiyo kutokana na barua nyingine aliyonayo kutoka kwa Prof. Ibrahim Lipumba inayomtaarifa kuwa nafasi ya katibu mkuu wa chama hicho inakaimiwa na Magdalena Sakaya baada ya katibu mkuu Maalim Seif kushindwa kutimiza majukumu yake, hivyo kuhesabika kuwa hayupo ofisini.
“Spika amemuandikia Maalim Seif Sharif Hamad kwamba anasita kuifanyia kazi barua yake kutokana na taarifa za awali alizozipokea” Imeeleza sehemu ya taarifa kutoka ofisi ya bunge.
0 comments :
Post a Comment