Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imesogeza mbele tarehe ya kusikiliza maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na jopo la mawakili wanaomtetea mfanyabishara Yusuph Manji ya kutaka mahakama kutengua zuio la kupatiwa dhamana kwa mteja wao.
Awali zuio la dhamana kwa mtuhumiwa Yusuph Manji liliwekwa na mkurugenzi wa mashtaka (DPP).
Upande wa Jamhuri unawakilishwa na mawakili wawili wakiongozwa na Paul Kadushi, huku upande wa utetezi ukiwa na jopo la mawakili wanane wakiongozwa na Alex Mgongolwa.
Usikilizwaji wa maombi umeahirishwa mbele ya naibu msajili wa mahakama hiyo, Mustapha Siami baada ya Jaji anayetakiwa kusikiliza maombi hayo Isaya Halfan kuwa nje ya kituo cha kazi.
Upande wa Jamhuri umewasilisha hati kinzani pamoja na notisi ya kupinga maombi ya dhamana kwa Yusuph Manji ambayo yana mambo matatu yanayoainisha sababu za kupinga maombi hayo.
Sababu hizo ni mahakama hiyo kukosa mamlaka ya kusikiliza maombi yaliyowasilishwa, pili ni kiapo walichokiwasilisha kuwa kinyume na sheria, huku vifungu vya sheria vilivyotumika kuwasilisha maombi hayo vikiwa na dosari.
Maombi hayo sasa yatasikilizwa tarehe 7 ya mwezi huu katika mahakama hiyo.
0 comments :
Post a Comment