Wanawake wa kijiji cha Lumecha wilayani Nyasa Mkoani Ruvuma wameiomba Serikali kuweka ratiba ya kudumu ya utoaji huduma za uzazi wa mpango bure kwenye vijiji vya pembezoni ili kuwasaidia kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi usio salama.
Wananchi hao wamekerwa na kitendo cha kutozwa fedha mbalimbali za vipimo ikiwamo kuuziwa mipira ya kiume, kuweka vipandikizi, kuchoma sindano na kupima watoto kliniki.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na wanawake hao wakati wakizungumza na mwandishi wa gazeti hili ambapo walionyesha uhitaji zaidi wa kupatiwa elimu na huduma za uzazi wa mpango.
Mmoja wa wanawake hao, Neema Komba alisema huduma hiyo imekuwa ikitolewa kwa zamu ambapo wakienda wataalamu wa afya kutoka taasisi ya Marie Stopes wamekuwa hawatozwi fedha, lakini siku za kawaida kuweka vipandikizi wanalipia Sh10,000, mipira ya kiume wanauziwa Sh1,000, kuchoma sindano za kujikinga na mimba Sh2000 na kupima watoto kliniki Sh200.
Alisema wanawake wengi hawana uwezo wa kulipia huduma hizo, hivyo hujikuta wakitumia njia za kienyeji na wengine huzaa mara bila mpango kutokana na kukosa elimu sahihi ya uzazi salama.
Neema alisema kijijini hapo idadi kubwa ya watoto wanajilea wenyewe kutokana na wazazi wao kuelemewa na idadi kubwa ya watoto waliozaa bila mpango hivyo kushindwa kuwahudumia kwa kuwaendeleza kielimu.
Kwa upande wake, Agnela Hyella alisema bado tatizo la upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango katika kijiji hicho ni kubwa na limechangia wanawake wengi kuzaa idadi kubwa ya watoto ambao hawana uwezo wa kuwatunza.
Mganga wa zahanati ya kijiji cha Kingerikiti ambayo pia inahudumia wananchi wa Lumecha, Linda Sanga alikana wanawake kutozwa fedha akisema huduma hiyo inatolewa bure na kuahidi kufuatilia iwapo kuna baadhi ya wahudumu ambao wanafanya vitendo hivyo.
Muuguzi wa zahanati hiyo, Emelita Mapunda alisema tatizo kubwa wananchi ni imani potofu kwamba huduma hizo zina matatizo, lakini kila baada ya miezi mitatu Marie Stopes hufika kwenye zahanati hiyo na kutoa huduma bure.
Aliwataka wananchi hao kujitokeza ili waweze kusaidiwa kwa kuwa vipandikizi vipo vingi na kondomu za kutosha.
Mganga mfawidhi hospitali ya Mkoa wa Ruvuma, Dk Magafu Majura alisema ili kuondokana na tatizo la utoaji mimba usio salama elimu juu ya kuepuka mimba zisizotarajiwa kwa akinamama wote walioolewa, wasioolewa pamoja na wanafunzi wa kike inapaswa kutolewa mara kwa mara.
Kwa mujibu wa taasisi ya Children Choice ya Marekani, wanawake saba kati ya 100 hupata mimba bila kutarajia kila mwaka huku mwanamke mmoja kati ya sita hakuwa amepanga kupata ujauzito nchini Uingereza mwaka jana, lakini aliupata bila kutarajia na hivyo kulazimika kujifungua.