Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.PICHA|MAKTABA
Kwa ufupi
Dar es Salaam. Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ameuliza
maswali saba ya msingi kwa wajumbe wa Bunge la Katiba wanaopinga Rasimu
ya Katiba iliyotolewa na Tume yake akitaka wawajibu wananchi ili
kutuliza kiu yao.
Jaji Warioba ambaye tangu awasilishe Rasimu ya
Katiba Desemba 30, mwaka jana amegeuka kuwa adui kwa watu wanaotaka
muundo wa serikali mbili, aliuliza maswali hayo jana katika uzinduzi wa
ripoti ya utafiti wa Taasisi ya Twaweza kuhusu mchakato wa Katiba.
Akizungumza kwa ukali, Jaji Warioba alisema:
“Kwanza, jibuni kwa nini mnapinga muundo wa Muungano wakati
walioupendekeza ni wananchi?
“Sheria inasema uwepo wa Muungano na mapendekezo
katika rasimu hayasemi Muungano usiwepo. Kumbukeni kuwa wananchi
walitakiwa kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha Muungano.”
Katika swali lake la pili, Warioba alisema kwa
nini Tanganyika imevaa koti la Muungano? Kwa kuwa katika ukusanyaji wa
maoni wananchi walieleza kuwa Serikali ya Muungano ya sasa siyo ya
Muungano, ni ya Tanganyika.
Katika swali la tatu alisema wajumbe hao
wanatakiwa kujibu maelezo ya wananchi ambao waliieleza tume hiyo kuwa
Katiba imevunjwa na madaraka ya rais yamechukuliwa na sasa kuna marais
wawili katika nchi moja.
“Tume inapewa lawama kubwa, wajibuni wananchi hii
tume ilitumwa na nani kukusanya maoni ya wananchi? Waambieni ilikusanya
maoni hayo kwa kutumia sheria ipi zaidi ya ile ya Mabadiliko ya Katiba?”
alisema Jaji Warioba katika swali lake la nne.
Katika swali lake la tano, Warioba aliwataka
wajumbe hao kutoa sababu za kumtuhumu kuwa amependekeza muundo wa
serikali tatu kwa sababu yeye pamoja na (Joseph Butiku) walikuwa wajumbe
wa Tume ya Jaji Kisanga na Jaji Nyalali ambazo nazo zilipendekeza
muundo wa serikali tatu, kitu ambacho alisema si kweli na hawakuwahi
kuwa mjumbe wa tume hizo.
Pia, aliwataka wajumbe hao kujibu swali la sita,
kwa nini hawataki kuzungumzia yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na badala
yake wanageuza rasimu hiyo kuwa imeandikwa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba.
Katika swali lake la saba, aliwataka wajumbe
kujibu kwa nini wanaishutumu Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa imeingiza
maoni yake, wakati ilikusanya maoni hayo kwa mujibu wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba?
Alisema badala ya kujadili hoja za msingi, wajumbe
wa Bunge hilo wamekuwa wakitoa lugha za kejeli na matusi kwa baadhi ya
watu (akiwamo na yeye), kitendo ambacho alisema si sahihi na kinaweza
kuligawa taifa kwa sababu yaliyomo katika Rasimu ya Katiba yametokana na
maoni ya wananchi.
Katika uzinduzi huo walikuwepo baadhi ya wajumbe
wa Bunge hilo ambao ni Dk Hamisi Kigwangalla aliyemwakilisha Katibu Mkuu
wa CCM, Abdulrahman Kinana, Julius Mtatiro, Maria Sarungi na aliyekuwa
mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole.
0 comments :
Post a Comment