Dodoma. “Anakatwa, hakatwi” ndilo swali lililokuwa linaulizwa nchi nzima
jana, lakini hatimaye Kamati Kuu ya CCM iliyokutana hadi usiku wa
manane iliibuka na jibu kwamba Edward Lowassa amekatwa, huku kukiwa na
wingu zito baada ya wajumbe watatu kupingana na uamuzi huo.
Muda mfupi baada ya kikao hicho, pamoja na kuwa Katibu wa Itikadi na
Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikataa kutaja majina yaliyopitishwa,
akaunti ya Twitter ya CCM, iliwataja waliopitishwa kuwa ni Bernard
Membe, Dk John Magufuli, Dk Asha Rose Migiro, January Makamba na Amina
Salum Ali na kuwatupa wengine 33 akiwamo Lowassa.
“Kikao cha Kamati Kuu kimeisha salama. Kesho (leo) Halmashauri Kuu
itakutana kuanzia saa 4:00 asubuhi,” alisema Nape baada ya kikao hicho.
Alipotakiwa kutaja majina ya makada watano waliopitishwa, Nape alisema:
“Nimeambiwa mchakato bado unaendelea na kesho (leo) Halmashauri Kuu
itakutana kuendelea na kazi. Kwa hiyo nawakaribisha kesho kuanzia saa
4:00 asubuhi mje mchukue picha, habari, karibu sana.” Mkutano Mkuu
utafanyika saa nane mchana leo.”
Dakika chache baada ya kikao hicho kumalizika, wajumbe watatu wa Kamati
Kuu, wakiongozwa na mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi
waliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa wanapinga
uamuzi huo ambao hawakuutaja, wakidai kuwa si majina yote
yaliyowasilishwa mbele ya kamati hiyo.
Dk Nchimbi, akiongozana na mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dodoma, Adam
Kimbisa na mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sofia Simba
waliwaeleza waandishi wa habari mara tu baada ya mkutano wa Kamati Kuu
kuwa kikao hicho hakikufuata kanuni kwa kuwa majina machache
yaliwasilishwa na hayakuhusisha mgombea anayekubalika.
Ingawa hawakumtaja mgombea huyo waliyesema anatajwa na wengi, wajumbe hao wanafahamika kuwa wanamuunga mkono Lowassa.
Baada ya kikao hicho taarifa za wagombea hao zilisambaa kwa kasi katika
mitandao ya kijamii na mijadala ya wazi ilianza kuhusu uamuzi wa kumtosa
Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya
Nne.
Mmoja wa makada watano waliopitishwa kwenye mchujo huo aliithibitishia
Mwananchi kuwa jina lake limepita, lakini akasema hataki akaririwe na
badala yake akamshauri mwandishi aangalie akaunti ya twitter ya CCM
baada ya nusu saa.
Habari za jina la Lowassa kukatwa zilizagaa tangu jana asubuhi,
ilipoelezwa kuwa CCM ilifanya majadiliano na wadau mbalimbali kuangalia
jinsi ya kudhibiti watu wanaounga mkono baada ya kupata taarifa kuwa
ameenguliwa.
Lowassa azua mjadala
Awali wakati Kamati Kuu ya CCM ikikutana jana usiku kupitisha majina ya
makada watano walioomba kuwania urais, jina la Edward Lowassa ndilo
lililotawala mijadala mingi kwenye mitandao ya kijamii, likiambatana na
swali moja; amekatwa, hajakatwa?
Hali hiyo iliendelea zaidi jana usiku wakati CCM ilipotangaza mabadiliko
ya tatu ya ratiba za vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu.
Watu wengi walikuwa wamefurika kwenye jengo la makao makuu ya CCM mjini
hapa, maarufu kama White House na walioruhusiwa kuingia walikuwa
waandishi wa habari na wajumbe wa Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu, ambao
walikuwa wakifuata makabrasha na vitambulisho.
Mapema jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliwaambia
waandishi wa habari kuwa kikao cha Kamati ya Maadili na Usalama
ingekutana kuanzia saa 4:00 asubuhi na kufuatiwa na Kamati Kuu saa 8:00
mchana, lakini baadaye akatangaza mabadiliko mengine ambayo yalionyesha
kuwa Kamati Kuu ingekutana kuanzia saa 10:00 jioni na Halmashauri Kuu
baada ya futari.
Majira ya saa 2:00 usiku, Nape alitangaza kuwa kikao cha Kamati Kuu
kingeanza muda huo na kwamba kingechukua muda mrefu na hivyo Halmashauri
Kuu itakutana leo kuanzia saa 4:00 asubuhi na orodha ya makada watano
waliopita kwenye mchujo itatangazwa muda huo.
Wakati Nape anawaambia waandishi wa habari jana asubuhi kuhusu sababu za
kuahirishwa kwa vikao, tayari kulikuwa na habari kuwa Lowassa
ameenguliwa baada ya vikao vya maridhiano kabla ya vikao hivyo vya juu
kuhusu namna ya kudhibiti wanachama wanaomuunga mkono.
Habari hiyo ndiyo iliyokuwa mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii.
“Amekatwa au hajakatwa?” ndilo swali lililoulizwa na wengi kwenye
mitandao hiyo kutaka kujua kama kada huyo, aliyeonyesha kuungwa mkono na
wengi wakati wa kusaka wadhamini.
Akizungumza na waandishi jana asubuhi, Nape alisema kuahirishwa kwa
vikao hivyo muhimu kulitokana na mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete kuwa
na vikao na watu mbalimbali kupata ushauri kuhusu namna ya kumaliza
mchujo kwa usalama.
“Mwenyekiti alikuwa na vikao mbalimbali vya consultation (mashauriano)
na wadau ili kuhakikisha vikao vinakwenda salama,” alisema Nape na
kuongeza kuwa hiyo ndiyo ilisababisha ratiba ya vikao kubadilishwa.
Hata hivyo, Nape hakuelezea vikao vya mashauriano kati ya Rais Kikwete na Serikali vilihusisha makundi gani.
Nape alisema mabadiliko hayo pia yalitokana na shughuli za kiserikali na
kichama ambazo Kikwete alikuwa nazo mjini Dodoma, ambako Julai 9
mwenyekiti huyo wa CCM alifanya kazi mbili za kuzindua jengo jipya la
mikutano la chama hicho na baadaye kulihutubia kwa mara ya mwisho Bunge
la 10, siku ambayo alitakiwa kuongoza kikao cha Kamati Kuu.
Awali Kamati ya Usalama na Maadili, ambayo inachambua wagombea na kutoa
mapendekezo ya kila mmoja, ilipangwa kukutana Julai 8, na kufuatiwa na
Kamati Kuu (Julai 9), Halmashauri Kuu ya Taifa (Julai 10) na Mkutano
Mkuu ambao ungefanyika Julai 11-12.
Lowassa ndiye anayeonekana kuwa kinara miongoni mwa makada 38 walioomba
kugombea urais kwa tiketi ya CCM, akionekana kuwa na wafuasi wengi ndani
na nje ya chama, hali ambayo aliionyesha kwenye harakati za kutafuta
wadhamini.
Mbunge huyo wa Monduli aliungwa mkono na takriban wenyeviti 15 wa mikoa,
wabunge kadhaa waliojitokeza bayana kueleza misimamo yao kwake na
wajumbe kadhaa wa Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu.
Jana, baada ya kusogezwa mbele kwa kikao cha Halmashauri Kuu, watu wengi
waliondoka kwenye viwanja vya makao makuu ya CCM, na hakukuwapo na
makada wanaowania kugombea urais kwenye eneo hilo ambako Kamati Kuu
ilikuwa ikiendelea na kikao chake.
Kwa kawaida Kamati Kuu hupitisha majina matano kwa makubaliano licha ya
kwamba katiba ya CCM inaruhusu maamuzi kufikiwa kwa kupiga kura.
“Mara nyingi hakuna upigaji kura kwenye vikao vya Kamati Kuu,” alisema
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Profesa Mark Mwandosya
alipoongea na Mwananchi nje ya jengo hilo jana saa 2:40 usiku baada ya
kuarifiwa kuwa kikao cha Halmashauri Kuu kimeahirishwa hadi leo.
“Mara nyingi uamuzi huwa ni kwa maridhiano licha ya Katiba kuruhusu
upinzani kura pale mnaposhindwa kukubaliana,” alisema Profesa Mwandosya
ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu.
CREDIT:MWANANCHI.
0 comments :
Post a Comment