KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) leo imekabidhi mradi mkubwa wa Mkongo wa
Mawasiliano ambao umeyaunganisha matawi yote ya Bohari ya Dawa Nchini
(MSD) na Makao Makuu ili kufanya kazi zake kwa haraka na kwa ufanisi.
Hafla ya kukabidhi mradi huo imefanyika leo Makao Makuu ya Ofisi za MSD
zilizopo jijini Dar es Salaam.
Akikabidhi mradi huo, kwa niaba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk.
Kamugisha Kazaura, Ofisa Mkuu wa Masoko na Mauzo wa kampuni ya Simu
Tanzania, Peter Ngota alisema kampuni hiyo inajisikia fahari kufanikiwa
kuunganisha ofisi zote za kanda za MSD na Makao makuu kupitia mkongo wa
mawasiliano ambao ni salama na wauhakika katika utendaji wa kazi.
Alisema
MSD ni moja ya wateja wake wakubwa ambao wameunganishwa kihuduma
kupitia mkongo wa mawasiliano ambao ufanisi wake ni mkubwa na salama kwa
wateja tofauti na teknolojia nyingine za mawasiliano. Alisema huduma za
mkongo wa mawasiliano zinazotolewa na TTCL kwa wateja wake ni salama na
zenye ubora katika ufanisi jambo ambalo limevuta idadi kubwa ya wateja
kuongezeka kila uchao.
Alisema
kwa sasa TTCL inatoa huduma hizo kwa makampuni ya simu, taasisi
mbalimbali za umma na binafsi, mabenki, hospitali kadhaa, vyombo vya
habari, wateja binafsi pamoja na mataifa kama Rwanda, Burundi, Uganda,
Kenya, Zambia na nchi ya Malawi.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa MSD,
Cosmas Mwaifwani alisema MSD ilianza kufungiwa mawasiliano ya mkongo
Mwezi Mei, 2011 kwa kuunganisha ofisi za makao makuu na baadaye ofisi
mpya za mauzo zilizopo Muleba zilizounganishwa mwaka 2013.
Alisema
MSD ilifanya uamuzi wa kuhamia kwenye teknolojia ya Mkongo baada ya
kuona uwepo wa matatizo makubwa yaliyokuwepo katika teknolojia ya awali
ambayo ni waya wa jadi yaani shaba ambayo pia ilitolewa na kampuni ya
TTCL.
"...Bohari ya Dawa iliamua kuhamia katika teknolojia hii baada ya
kufanya utafiti wa kina na kuona faida ambazo zinaweza kupatikana kwa
kutumia teknolojia hii (mkongo) na hivyo kuachana na matatizo
yanayosababishwa na teknolojia ya shaba. Hii ina maana mkongo unaweza
kubeba habari zaidi na kwa ubora mkubwa kuliko waya wa shaba," alisema
Mwaifwani.
Alisema
kwa sasa MSD imeanza kupata mafanikio makubwa baada ya kuanza kutumia
huduma za mkongo na tayari TTCL imeyaunganisha Ofisi 10 za MSD ambazo ni
Kanda nane (8) pamoja na vituo viwili vya mauzo; alizitaja Kanda
zilizounganishwa ni pamoja na Dar es Salaam, Moshi, Iringa, Mbeya,
Mwanza, Tabora, Dodoma, Mtwara, Muleba, Tanga, Makao Makuu ya Muda
Jamana na Ofisi za Keko Mwanga.
"...Tunasema kwamba Bohari ya Dawa imedhamiria kuokoa maisha ya
Watanzania kwa kutumia teknolojia ya Mkongo yenye kasi zaidi, usalama,
na gharama nafuu zaidi katika kuhakikisha dawa zenye ubora zinamfikia
kila Mtanzania kwa wakati na kupunguza kero ya kusubiri huduma zetu kwa
muda mrefu kwani sasa huduma zinapatikana kwa wakati kwa kuwa teknolojia
inayotumika ni ya kisasa na yenye ubora wenye kukidhi viwango
vinavyohitajika na bohari ya dawa," alisema Mkurugenzi Mkuu, Mwaifwani.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com


0 comments :
Post a Comment