Mwenyekiti wa chama cha riadha mkoa wa Mwanza Silas
Lucas akiwapa maelekezo wakimbiaji wa km 21 wakati wa mbio za Rock City
Marathon kabla ya mbio kuanza kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza jana.
Wanariadha katika kundi la km 21 wakikatiza katika mitaa ya
jiji la Mwanza kuelekea katika viwanja vya CCM Kirumba kumaliza mbio hizo.
Festus Taram kutoka Kenya akimaliza katika nafasi ya kwanza kwenye mbio za Rock
City Marathon zilizofanyika jijini Mwanza jana baada ya kutumia muda wa saa
01:04:40, akifuatiwa kwa karibu na mshiriki mwenzake kutoka nchini humo Evancy
Kiplagan aliyetumia muda wa saa 01:04:55
Afisa michezo mkoa wa Mwanza, James William, akimkabidhi
zawadi ya kitita cha shilingi milioni moja na nusu mshindi wa kwanza wa mbio za
km 21 upande wa wanawake Alice Mogire kutoka Kenya baada ya kutumia muda wa saa 01:14:42
kumaliza mbio hizo.
Wanaoshuhudia ni Meneja Mkuu kampuni ya Capital Plus International Limited
ambao ni waandaaji wa mashindano hayo, Erasto Kilawe (kushoto), Meneja Kiongozi
wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) mkoa wa Mwanza, Hamis Faki (wa
pili kushoto), mjumbe wa shirikisho la riadha Tanzania (RT), Peter Mwita (wa
pili kulia) na Mwenyekiti wa chama cha riadha mkoa wa Mwanza, Silas Lucas.
Wanariadha katika kundi la kilomita tano wakipasha kabla ya
kuanza kwa mbio hizo.
Raia wa kigeni nao walijitokeza kuchuana vikali katika mbio
hizo.
Wanariadha wakianza
kukimbia mbio za km 21 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza jana, wakati
wa mbio za Rock City Marathon 2015.
Washindi wa nafasi tatu za juu katika mbio za km 21 upande wa
wanaume wakionyesha medali na pesa taslimu walizopokea kama zawadi baada ya
kuibuka washindi katika mbio hizo.
Mwandishi wetu, Mwanza
Festus Taram kutoka Kenya aliibuka
mshindi wa kwanza kwenye mbio za Rock City Marathon zilizofanyika jijini Mwanza
jana baada ya kumaliza kwa muda wa saa 01:04:40, akifuatiwa kwa karibu na mshiriki
mwenzake kutoka nchini humo Evancy Kiplagan aliyetumia muda wa saa 01:04:55
Mbio hizo za kilomita 21 zilianzia
Uwanja wa CCM Kirumba kupitia Barabara ya ikulu ndogo hadi mzunguko wa samaki
na kuelekea Buzuruga kisha kutokea barabara ya pasiansi na kumalizikia uwanjani
Kirumba.
Nafasi ya tatu upande wa wanaume
ilichukuliwa na Mtanzania Fabian Joseph aliyetumia muda wa saa 01:05:00, ikiwa
dakika chache nyuma ya mpinzani wake.
Akizungumzia siri ya ushindi wake,
Talam alisema hii ni mara ya pili kushiriki mashindano hayo ambapo mwaka jana
alishika nafasi ya tatu jambo lililompa chachu ya kujituma kufanya mazoezi zaidi
na kukaa kambini muda mrefu jambo lililopelekea kufanya vizuri katika michuano
ya mwaka huu.
“Maandalizi ya mwaka huu ni mazuri
na washiriki wameendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka jambo linalotufanya
wanariadha kujiwekea mikakati mizuri ili kuweza kukabiliana na ushindani mkali
uliopo katika mbio hizi,” alisema.
Upande wa wanawake mshindi wa kwanza
ni Mkenya Alice Mogire aliyetumia muda wa saa 01:14:42 akifuatiwa na Mtanzania
Natalia Elisante aliyetumia saa 01:15:16 huku Raia mwingine wa Tanzania
Angelina Isere akishika nafasi ya tatu baada ya kutumia saa 01:15:35
Washindi wa kwanza katika mbio hizo
zilizofanyika kwa mara ya saba jijini Mwanza waliibuka na kitita cha
Sh1.5 milioni kila mmoja, washindi wa pili Sh900,000 na washindi wa tatu
Sh700,000 kila mmoja.
Mashindano hayo ya kila mwaka yaliyo
katika kalenda ya RT yaliandaliwa na Kampuni ya Capital Plus kwa udhamini wa
Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bank M, Precision Air, New Mwanza
Hotel, Bodi ya Utalii Tanzania na PPF.
Wakati huohuo, Katibu tawala mkoa wa
Mwanza alipongeza waandaaji wa mbio hizo na kutoa wito kwa wadau mbalimbali
kushirikiana kwa pamoja ili kurejesha hadhi ya mchezo wa riadha nchini.
Akikabidhi zawadi kwa washindi wa
mbio hizo kwenye uwanja wa CCM Kirumba kwa niaba ya Katibu tawala jana, Afisa
michezo mkoa wa Mwanza, James William, alisema mbio hizo ni nyenzo muhimu ya
kuwaandaa wanariadha wetu nchini kuwa katika nafasi ya kufanya vizuri katika
michuano ya kimataifa na kuirudishia nchi yetu heshima ya kipekee katika mchezo
huo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
0 comments :
Post a Comment