DAR ES SALAAM
CHAMA CHA ACT-WAZALENDO KINAITAKA TANZANIA NA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI KUKOMESHA MAUAJI NCHINI BURUNDI
1. Chama cha ACT-Wazalendo
kinasikitishwa sana na maujai yanayoendelea nchini Burundi na hasa Mji
Mkuu wa nchi hiyo Bujumbura. Hali hii ya mauaji imesababishwa kwa kiasi
kikubwa na uamuzi wa Rais wa
sasa wa nchi hiyo Ndugu Piere Nkurunzinza
kuendelea kugombea na hatimaye kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo katika
mazingira yaliyovunja demokrasia na utawala bora.
2. Tangu machafuko
nchini Burundi yaanze zaidi ya watu 100 wameshauawa kufikia wiki hii na
wengine kadhaa kujeruhiwa. Aidha, wimbi la wakimbizi kutoka Burundi
linarudi kwa kasi na wengi wao wakikimbilia nchini Tanzania.
3. Bahati mbaya sana Jumuiya ya
Kimataifa na hasa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Burundi ni
mwanachama, haikuchukua hatua za maana za kuzuia kuchafuka kwa utawala
wa kidemokrasia na utawala wa sheria nchini Burundi, na wala haichukui
hatua stahiki kuzuia mauaji yanayoendelea. Hii ni kinyume kabisa na
Mkataba unaounda Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao unatoa kipaumbele cha
juu kulinda uhai na haki za raia katika Jumuiya hiyo
4. Kutokana na hali ya kisiasa na
usalama nchini Burundi, na kwa kuzingatia nafasi ya kihistoria ya
Tanzania katika kutafuta na kufanikisha Mkataba wa Amani nchini Burundi,
na kwa kuzingatia nafasi yake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na
Umoja wa Afrika, tunaitaka serikali ya Tanzania, kwa hali kubwa ya
dharura, ichukue hatua zifuatazo:
a. Iitake serikali ya Jamhuri ya Burundi
kukomesha mara moja maujai yanayoendelea nchini humo na kuwahakikishia
raia wa nchi hiyo usalama
b. Iitake serikali ya Jamhuri ya Burundi
kuitisha mkutano wa wadau wote wa siasa na utawala nchini humo ili
kujadili mustakabali wa nchi hiyo kisiasa na kijamii, ikiwemo uwezekano
wa kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayosimamia Katiba ya Burundi
kuelekea uchaguzi wa kidemokrasia
c. Itumie nafasi yake katika Jumuiya ya
Afrika Mashariki kuitakaJumuiya hiyo kuzuia machafuko nchini Burundi na
kuhakikisha kwamba utawala wa demokrasia na utawala wa sheria
unazingatiwa nchini humo
5. Chama cha ACT-Wazalendo kinasisitiza
kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki itakosa uhali wa kuendelea kuwepo kwake
kama itaendelea kuwa Jumuiya ya viongozi wa nchi zinazounda Jumuiya
hiyo na kishindwa kusimamia haki za kuishi na haki za kiraia za wananchi
wa Afrika Mashariki.
Venance Msebo
Katibu wa Kamati ya Mambo ya Nje
ACT-Wazalendo
Jumatano, 16 Desemba 2015


0 comments :
Post a Comment