Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara
wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Robert Pascal
(Kulia) akimsikiliza Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kisheria wa Benki,
Bibi Neema Christina John (aliyevaa miwani) wakati wa uhakiki wa fomu
zilizojazwa na moja kati ya vikundi vilivyofanikiwa kupata mkopo kutoka
Benki hiyo.
Mwanasheria mwandamizi wa TADB,
Bibi Salome Masenga (Kulia) akimuelekeza mmoja wa wanakikundi waliopata
mikopo kutoka Benki hiyo.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki
ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Thomas Samkyi (Kushoto)
akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Bw. Kasunga (Kulia).
Picha ya pamoja
……………………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu, Iringa
Benki mpya ya Maendeleo ya Kilimo
Tanzania (TADB) imesema hadi kufikia miaka mitano ijayo itakuwa
imefungua ofisi sita za kikanda zenye lengo la kuwahudumia wakulima nchi
kote.
Mikakati hiyo iliwekwa bayana na
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo, Bibi Rosebud Kurwijila
wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano ya mikopo kati ya TADB na
wakulima wadogo wadogo wa mkoa wa Iringa, katika kijiji cha Igomaa,
wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Bibi Kurwijila alisema kuwa TADB
inalenga kutelekeza kwa vitendo Maelekezo ya Serikali ya kupunguza
changamoto zinazowakabili wakulima nchi kote.
Aliongeza kuwa kwa sasa Benki inalenga kusambaa nchi nzima kwa kuanzisha Ofisi za Kikanda ndani ya miaka mitano ijayo.
“Tunalenga kuwafikia wakulima
wote nchini kadri siku zinavyoendelea kwenda na kutegemea mtaji
unavyoongezeka ama upatikanaji wa fedha toka vyanzo mbali mbali ili
kuweza kuwawezesha kumudu shughuli zao za kilimo,” alisema.
Aliongeza kuwa Benki inaleenga
kuwajengea uwezo na kuanzisha Programu Maalumu ya Vijana wajihusishao na
shughuli za Kilimo cha kibiashara na kushirikiana na wadau wengine
kuhuisha shughuli za umwagiliaji na miradi ya kisasa ya umwagiliaji.
Malengo mengine ni kutafuta fedha
toka vyanzo mbalimbali zenye gharama nafuu kwa minajili ya kuwakopesha
Wakulima katika hatua zote za mnyororo wa ongezeko la thamani kwenye
mazao ya Kilimo na kupanua wigo wa utaoji mikopo toka Minyororo Kumi na
Minne (14) ya Mwanzo na kuhusisha pia mazao mengine ya Kilimo na pia
kuwaunganisha Wakulima na masoko ya ndani na nje ya nchi.
Akizungumza katika hafla hiyo,
Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Bw. Thomas Samkyi amesema kwamba Benki
yake imedhamiria kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo
nchini ili kuchagiza na kusaidia kuwezesha Sekta ya Kilimo kutoka kilimo
cha kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara ili kukuza uchumi na
kupunguza umaskini nchini.
Bw. Samkyi alisema TABD
imejizatiti kuchangia kwa kiasi kikubwa katika mapinduzi ya kilimo kwa
kuongeza tija na upatikanaji wa mikopo ya riba nafuu maalum kwa sekta ya
kilimo, kama njia ya kuleta Mapinduzi yenye tija kwa wakulima nchini.
“Benki imejipanga kutoa mikopo
yenye riba nafuu katika muda mfupi, wa kati na mrefu kwa Wakulima wadogo
wadogo, wa kati na wakubwa, hususan kuziba pengo la upatikanaji wa
fedha za kwenye mnyororo wa ongezeko la thamani katika tasnia za kilimo,
mifugo, uvuvi na mazao ya misitu (ufugaji nyuki),” alisema Bw. Samkyi.
Mkurugenzi huyo alisema kwamba
kwa kuanzia walengwa wakuu wa TADB ni wakulima wadogo wadogo, hatahivyo,
hata wale wakulima wa kati na wakubwa watahudumiwa.
Bw. Samkyi imejidhatiti katika
kufanya tathmini ya kina katika mnyororo mzima wa thamani ili kutambua
mapengo na mapungufu yanayohitaji utatuzi kwa minajili ya kuongeza
thamani na ushindani kwenye masoko.
“Sera ya TADB ni kutathmini
mnyororo mzima wa thamani ili kutambua mapengo na mapungufu yanayohitaji
utatuzi, na ambayo utatuzi wake utaongeza tija na uwezo wa ushindani
kwenye masoko, na hivyo kukuza uchumi wa walio wengi na kupunguza
umaskini,” aliongeza.
Katika hafla hiyo, jumla ya
vikundi nane (8) vyenye jumla ya wakulima wadogo wadogo 857, vilimiza
vigezo na kupewa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja.
Kwa mujibu wa Bw. Samkyi kabla ya
kutoa mikopo hiyo, benki iliwatembelea na kutoa elimu kwa wakulima
jinsi ya kuimarisha vikundi vyao, ambapo jumla ya vikundi 89 vyenye
jumla ya wanakikundi 21,526 vilifikiwa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mama
Amina Masenza amewaasa Wakulima wote nchini kutumia vizuri mikopo
wanayopewa ili kuweza kutimiza malengo yao binafsi na ya Serikali katika
kusaidia upatikanaji wa utoshelezi na usalama wa chakula ambao ni
endelevu nchini Tanzania.
Mama Masenza alisema kuwa
wakulima wakitumia mikopo waliyopewa kwa malengo husika watafika mbali
na kuweza kuchagiza mikakati ya Benki hiyo katika kusaidia Mapinduzi ya
Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kilimo kibiashara ili
kukuza uchumi na kupunguza umaskini.
“Naamini, wakati Benki ya
Maendeleo ya Kilimo itapoanza kufanya tathmini ya mikopo hii iweze kuona
matunda ya uwekezaji wake hasa kwa nyie ambao mmeweza kubahatika kupata
fursa ya awali kabili kunufaika na huduma za TADB,” aliwasihi.
Mama Masenza aliwaomba wakulima
hao kuwa Mfano Bora na wanaojitambua vilivyo, hasa nia ya kutoka katika
kiwango fulani cha maisha kwenda katika hatua nyingine za juu zaidi
kimaisha kwa kuongeza kipato na ubora wa kimaisha kwa ujumla kupitia
huduma za TADB.
“Nawasihi kutotumia pesa hizi
kinyume na malengo yaliyokusudiwa, kwani kwa kufanya hivyo, siyo tuu
tunaiua Benki yetu bali pia tunajimaliza wenyewe kiuchumi. Wito wangu
kwenu ni kujipanga kwa dhati ili kuweza kutimiza malengo makuu ya mikopo
hii ambayo ni kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini
kwa kusaidia upatikanaji wa fedha na sera nzuri zitakazosaidia
maendeleo ya kilimo nchini,” aliongeza.
Benki ya Maendeleo ya Kilimo
Tanzania ilizinduliwa Rasmi na Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kwenye Kilele cha
Maadhimisho ya Siku ya Wakulima nchini, mnamo tarehe 8 Agosti 2015 mjini
Lindi. Uanzishwaji wa Benki hii ni utekelezaji wa malengo ya muda mrefu
ya Serikali, katika kuitikia wito wa wananchi na wadau wengine wa
maendeleo ili Tanzania iweze kupiga hatua endelevu za kimaendeleo.
0 comments :
Post a Comment