………………………………………………………………………………………….
Na Shamimu Nyaki MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Mkesha
mkubwa wa kuiombea amani Tanzania utakaofanyika Disemba 31 mwaka huu
katika uwanja wa Taifa.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Makanisa ya Pentekoste (TFC) Godfrey Malassy alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari leo jijin Dar es Salaam, na kuthibitisha kuwa
maandalizi yote yamekamilika ikiwemo kibali kutoka polisi, pamoja
washiriki mbalimbali watakaoshiriki katika mkesha huo.
Askofu Malassy ameongeza kuwa mkesha huo
utakuwa ni kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kuijalia nchi yetu
kumaliza Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Oktoba mwaka huu kwa amani na
utulivu,pamoja na Dua maalum ya kumuombea Mhe. Rais afya njema na
utendaji mzuri anaoendelea kuufanya kwa maendeleo ya Taifa letu kwa kuwa
mara zote amesisitiza kufanyiwa maombi na watanzania.
“Tutatumia nafasi hiyo kumuombea Mhe.Rais
katika kutekeleza jukumu kubwa alilokabidhiwa na watanzania kuongoza
Taifa letu ili aweze kufanikiwa katika hilo.”Alisema Askofu Malassy.
Aidha Mwenyekiti huyo amewataka wananchi
wote kutumia siku hiyo kumuomba na kumshukuru Mungu kwa amani iliyopo
nchini kwa vile ndio msingi mkubwa wa shughuli za kila siku zinazosaidia
kupata kipato na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Naye Mch.Olivia Mallonga ambaye ni mjumbe
katika kamati ya maandalizi ya Mkesha huo amesema kwamba wao kama wadau
wanaendeleza desturi ya kuliombea Taifa amani ili lisije kutumbukia
kwenye machafuko kama nchi nyingine .
“Watanzania wana dini ndio maana wanatumia
imani zao kufanya maombi ili Mungu awalinde na maovu au machafuko
yanayoweza kutokea kutokana na sababu yoyote.”Aliongeza Mch. Olivia.
Mkesha huo ni wa 17 tangu ulipoanza
kufanyika Tanzania na umeleta mafanikio makubwa ikiwemo kuunganisha
watanzania bila kujali imani zao.
0 comments :
Post a Comment