Wednesday, December 2, 2015
@nkupamah blog
MWENYEKITI
wa Taifa wa chama cha siasa cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema
amesema hakufanya makosa na wala hajutii kumnadi Rais John Magufuli
kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu kwa sababu alitambua Watanzania
wamelamba dume la maendeleo.
Akizungumza
na mtandao huu jana mjini Moshi, Mrema alisema Watanzania wamepata mtu
wa kuendeleza kazi aliyokuwa akiifanya kipindi yeye wakati akiwa Naibu
Waziri Mkuu katika miaka ya 1990, ya kupambana na wahujumu uchumi, wala
rushwa na wafanyakazi wazembe.
Mrema
alisema Dk Magufuli ndiye mwenye uwezo pekee wa kuyaleta mabadiliko ya
kweli yanayohitajika, japo wengi waliamini hayawezi kupatikana ndani ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndio maana alichukua jukumu la kumpigia
kampeni.
Mrema
aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Vunjo mwaka 2010 hadi mwaka 2015,
alisema anamfahamu vizuri Dk Magufuli tangu akiwa Waziri wa Ujenzi,
kutokana na uchapakazi wake, ambapo walisaidiana kujenga barabara za
Vunjo, hali iliyosaidia jimbo hilo kuwa na mtandao mkubwa wa barabara
zilizojengwa kwa kiwango cha lami.
“Watu
walishangaa sana kwa nini nilimpigia kampeni Dk Magufuli, na kumwacha
mgombea wangu…nilijua mtu pekee wa kuyaleta mabadiliko makubwa na kweli
ni yeye… Kwanza nampongeza sana na nafurahi sana kwa taifa hili
linahitaji kiongozi mchapakazi, mwadilifu kama yeye,” alisema Mrema.
Katika
kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka huu, akiwa jimboni Vunjo, Dk Magufuli
alikutana na Mrema wakati huo naye akiomba kura za ubunge, na alimshika
mkono na kumtambulisha akiwa katika moja ya mikutano yake, na Waziri
huyo wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alimpigia debe mgombea huyo wa
urais wa CCM.
Mrema
alifanya hivyo huku chama chake, TLP kikiwa kimemsimamisha MacMillian
Lyimo kuwania urais wa Tanzania, hali iliyoibua mijadala wakati huo wa
kampeni, huku mwanasiasa huyo machachari nchini akitetea msimamo wake
huo wa kumnadi Dk Magufuli badala ya Lyimo.
Mrema
alisema Uchaguzi Mkuu umeibua rais mwema, mwadilifu na mwenye uchungu
na Watanzania wote. Aliwataka Watanzania kuacha ushabiki wa vyama vyao
vya kisiasa na kuangalia mtu anayefanya kazi ya kulikomboa Taifa hili,
kama Dk Magufuli kwa kumuunga mkono na kumuombea.
Alisema
tangu Taifa lipate Uhuru, kwa sasa Tanzania imeandika historia ya kuwa
na viongozi mahiri watatu wa kupambana na umaskini, ambapo aliwataja
viongozi hao ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Sokoine (sasa hayati) na Dk Magufuli.
0 comments :
Post a Comment