Mkuu
wa wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Mohamed Utaly akimkabidhi mkazi wa
kijiji cha Kiegea, Bibi Sarah Matereka mbegu za mtama kwa ajili ya
shamba lake kama mpango wa wilaya hiyo kuhamasisha wananchi wilayani
humo kulima mazao yanayohimili ukame ili kukabili maafa ya njaa ,
wanaoshuhudia kushoto ni Mkurugenzi Idara ya uratibu maafa Ofsi ya
Waziri Mkuu, Brig. Jen. Mbazi Msuya na katikati ni mbunge wa Jimbo la
Mpwapwa, Mhe. George Lubeleje tarehe 31 Desemba, 2015.
Mmiliki
wa shamba la Uzalishaji Mbegu bora za Muhogo aina ya Mumba katika
Kijiji cha Choka wilayani Mpwapwa, Edward Kusenha akieleza ubora wa
mbegu ya muhogo huo kuwa tangu apande mbegu hiyo mwaka 2014 anaouhakika
wa chakula kwa kipindi chote cha hali ya ukame kijijin hapo
anayemsikiliza ni Dereva Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Uratibu maafa,
Nuru Gagu wakati ofisi hiyo ilipokuwa ikifuatilia hali ya upungufu wa
chakula kijijini hapo tarehe 31 Desemba, 2015.
Kufuatia
ziara ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa maafa katika Wilaya
za Mpwapwa na Kondoa mkoani Dodoma tarehe 30 Desemba, 2015, iliyolenga
kufuatilia hali ya upungufu wa chakula katika wilaya hizo hususan katika
maeneo yote yaliyoathirika na ukame. Ofisi ya waziri mkuu, Idara ya
Uratibu wa maafa imetembelea wananchi wa Wilaya hizo na kufanikiwa kuona
baadhi yao wanayo mashamba ya mbegu na mazao yanayohimili ukame suala
linalowezesha familia zao kuwa na uhakika wa chakula kwa kutohitaji
chakula cha msaada kutoka Ofisi ya waziri mkuu.
Ofisi
ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu maafa inazishauri Kamati za Maafa za
Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji ambazo ndizo zenye jukumu kubwa la
kusimamia masuala ya maafa katika ngazi hizo ziombe mbegu za mazao yenye
kuhimili ukame katika Halmashauri zao na kuzigawa bure kwa wananchi
badala ya kuwa wanawaombea chakula cha msaada kila mwaka.
Hivyo;“Nashauri
watendaji wakuu wa Halmashauri na mikoa kupitia kamati za maafa
maombi yanayokuja ofisini kwangu kuanzia sasa wasiombe chakula cha
msaada tu bali waombe na mbegu zinazo himili ukame kwa kuwaorodhesha
wananchi wote wanaohitaji mbegu hizo na kuwasilisha katika Ofisi ya
Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu maafa na Ofisi yangu itatuma fedha za
kununua mbegu kutoka kwa wananchi wenye mashamba ya mbegu hizo ili
zigawiwe bure kwa wananchi wengine wenye upungufu wa chakula.
tunahitaji wananchi wote wawe na uhakika wa chakula .” amesema Brig.
Jen. Msuya
Katika
kuhakikisha ushauri huo unatekelezwa Mkurugenzi Idara ya Uratibu Maafa,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Jenerali Mbazi Msuya amebainisha kuwa,
ili wananchi walime wanahitaji chakula hivyo tayari ofisi yake
imeshapeleka tani, 1,396 za mahindi ya chakula cha msaada mkoani Dodoma
kuanzia mwezi Septemba hadi Desemba 2015, ikiwa tani 200 za mahindi
zimepelekwa wilayani Mpwapwa na tani 150 za mahindi wilayani Kondoa.
Awali
akiongea katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Mohamed Utaly
ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu Maafa kwa kufuatilia
hali ya upungufu wa chakula wilayani humo pamoja na kuahidi kutoa mbegu
pamoja na chakula cha msaada kingine wilayani humo kwa kuwa wilaya hiyo
imeshaanza mipango endelevu wa kukabili njaa wilayani humo na kuvitaka
vyombo vya habari kuripoti taarifa sahihi za hali ya chakula wilayani
humo.
“Napenda
kwanza kukanusha taarifa zilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari
hapa nchini kuwa wananchi wa wilaya yangu wanapika mawe hilo sio kweli
bali sisi chakula tumeshaletewa na Ofisi ya waziri Mkuu lakini tatizo la
wananchi wetu ni uwezo wa kununua mahindi hayo yanayouzwa kwa bei nafuu
hivyo kimsingi tunaendelea kuwashauri wananchi walime zao la muhogo
kwani linahimili ukame katika wilaya hili kwa ajili ya chakula na
biashara lakini pia na ufugaji wa kuku na mbuzi utawawezesha wananchi
wangu kukabili athari za ukame kama njaa” amesisitiza Utaly.
Mbunge
wa jimbo la Mpwapwa Mhe. George Lubeleje alifafanua kuwa, kama kiongozi
aliyechaguliwa na wananchi ataendelea kuwahamasisha wananchi kulima
mazao yanayohimili ukame ambayo yatawawezesha kuwa na uhakika wa chakula
na uchumi.
“Kimsingi
Ofisi ya Waziri Mkuu kuamua kutoa mbegu bure zinazohimili ukame
litakuwa jambo jema kwa kuwa wananchi kipindi cha upungufu wa chakula
huacha shughuli zao na badala yake kutafuta vibarua ili waweze kupata
pesa na kununua chakula lakini kwa mpango huu watakuwa wanalima mashamba
yao” amesema Lubeleje.
Aidha;
Sheria Na. 7 ya Mwaka 2015 ya Menejimenti ya Maafa inamtaka kila mdau
kutekeleza wajibu wake katika suala zima la menejimenti ya maafa ikiwa
pamoja na Kuzuia, Kujiandaa, Kukabili na Kurejesha hali baada ya maafa
kutokea.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
OFISI YA WAZIRI MKUU
31 DESEMBA 2015
0 comments :
Post a Comment