
Ndugu Zangu,
Nilikuwepo
pale Viwanja vya Jangwani. Nilipomsikia Ben Mkapa akiwaita wapinzani '
Wapumbavu na Malofa', basi, nikajua hiyo ndio ingekuwa ' Habari ya
Mjini'. Nilikuwa sahihi. Ni kwa vile aliyetamka hayo alikuwa Ben, Rais
Mstaafu.
Na
hakika, mitaani nikawakuta watu wanaohangaika sana hata kuingia kwenye
kamusi ya Kiswahili
kuona tafsiri ya maneno aliyotamka Ben, kama ni
matusi au la!
Niliandika,
kuwa Ben kwa kauli ile alichangia kupromoti lugha ya Kiswahili. Lofa,
ina tafsiri ya mtu aliyefilisika,kupungukiwa mtaji na hata mwenye
kutembea akipoteza muda. Yaweza pia kutafsiriwa kuwa kufilisika kisiasa.
Inategemea imetamkwa katika muktadha gani. Chimbuko lake ni kwenye
kimombo; ' wasting time'- Are you loafing, you better hurry up and do!
....
Niliandika,
kuwa mapambano ya kisiasa, na hususan kwenye kampeni za uchaguzi huwa
na sura ya mikakati inayyofanana na ya mapambano ya kijeshi. Na kwenye
vita kinachopelekea ushindi ni vitu vitatu; Silaha bora, uwezo wa
wapiganaji na propaganda.
Huenda si
wengi waliokuwa na kumbukumbu kuwa Ben Mkapa alipata kuwa Waziri wa
Mambo ya Nchi za Nje kwenye kipindi ambacho Tanzania ilikuwa vitani
dhidi ya Idd Amin.
Ni Ben
Mkapa aliyeongoza vita vya propaganda dhidi ya Idd Amin, dunia
ikaaminishwa kuwa Tanzania ilikuwa na sababu, uwezo na nia ya kumpiga
Idd Amin. Ni kwenye kipindi kile cha vita, na kazi ya fasihi kwenye
lugha ya vita ilifanywa na watu wa aina ya Ben Mkapa na Paul Sozigwa, na
iliyotumika vema kwenye propaganda za kimapambano. Ndio, ikamfanya Idd
Amin aonekane si lolote si chochote.
Nini basi tofauti ya Mjinga na Mpumbavu?
Marehemu
Mzee Jongo alipata kutamka; ” Kusoma sio kuufuta ujinga, bali ni
kuupunguza”. Kila mwanadamu ana ujinga wa jambo moja au mia moja. Kuwa
na ujinga wa jambo si kosa, hata Profesa anaweza asijue namna ya
kuchochea kuni za kuchomea hindi bichi likachomeka. Kijana wa darasa la
saba anaweza kuwa hodari wa jambo hilo kumshinda Profesa.
Lakini,
upumbavu ni ile hali ya mwanadamu kufanya jambo isivyotakiwa huku akiwa
na uelewa wa namna ya kufanya inavyotakiwa. Huo ndio upumbavu.
Baada ya vumbi lile la kisiasa kutuama, leo kuna wengi, hata wale waliokuwa wakimpinga Ben, wanamwelewa Ben alimaanisha nini...
Kama bado kuna wajumbe wenye kutofautiana na Ben Mkapa, ukumbi wa mjadala uko wazi...
Chanzo :Maggid.(P.T)
0 comments :
Post a Comment