Aliyekuwa
mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na
kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
Edward Lowassa, ametangaza vita mpya na serikali ya kuanza safari ndefu
ya kuelekea Ikulu mwaka 2020.
Moja ya kati vita yake hiyo na serikali ni kuanza kwa msukumo mkubwa wa kudai tume huru ya uchaguzi.
Lowassa alisema hayo wakati akizungumza na wafanyabishara wanaotaka
mabadiliko wanaofanya shughuli zao Kariakoo, jijini Dar es Slamaa juzi.
Alisema ili safari ya 2020 iwe na mafanikio, lazima chama chake
kupitia kwa wabunge wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) washinikize
kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi.
Alisema ana amini kwamba bila kupatikana tume huru hakuna haki
itakayopatikana wakati wa uchaguzi, kusimamia matokeo na kumtangaza
mshindi.
Harakati za kudai tume huru ya uchagzi ziliwahi kufanywa na wadau
mbalimbali vikiwamo vyama vya upinzani, lakini kilio chao hakijawahi
kusikilizwa.
Miongoni mwa wadau waliojitolea kudai tume huru ya uchaguzi ni
marehemu, Christopher Mtikila, ambaye tangu kuanzishwa vyama vingi hapa
nchini aliipigania mpaka anafariki dunia mwaka jana.
Wengine waliopigania na kudai kwa nguvu kuwapo kwa tume huru ya
uchaguzi ni viongozi wa Chama cha Wananchi Cuf, upande wa Zanzibar kabla
ya mwaka 2010.
Hata hivyo, nguvu za CUF zilipungua nguvu baada ya mwaka 2009 baada
ya kubadilishwa Katiba ya Zanzibar iliyoruhusu serikali ya umoja wa
kitafa.
Lakini pia Katiba Mpya iliyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba iliyoongozwa na Jaji Mstaafu, Joseph Warioba, iliweka kipengele
cha kuuundwa tume huru ya uchaguzi pamoja na kuruhusu mgombea binafsi.
Hata hivyo, Bunge la Katiba ambalo wajumbe wake wengi walitoka
Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliondoa vipengele hivyo, hatua ambayo
imeendelea kufanya jambo hilo kuwa gumu japo limekuwa likilalamikiwa na
wadau wengi.
Aidha, katika kikao hicho na wafanyabiashara, Lowassa aliendelea
kudai kuwa alishinda nafasi ya urais lakini aliamua kukubali yaishe ili
kuepusha machafuko na kwamba hakuwa tayari kuingia Ikulu mikono yake
ikinuka damu.
Alidai baada ya kushinda na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kukataa
kumtangaza, angesema watu waingie barabarani wangechinjana jambo ambalo
hakutaka kuona linatokea hapa nchini.
"Sijakata tamaa kwa sababu naamini nilishinda katika uchaguzi
uliopita, Watanzania wanajua na dunia inajua, lakini niliamua yaishe ili
kulinda amani tuliyonayo," alidai na kuongeza:
"Nipo salama, nipo fiti na morali yangu katika kuelekea Ikulu ipo juu sana zaidi ya mwaka jana."
Alisema ili kufikia malengo yake ya kisiasa yeye na chama chake
wanajipanga kwa nguvu nyingi ili kushiriki uchaguzi ujao wa mwaka 2020.
Alitoa mfano kuwa kuna Rais mmoja wa Marekani aliwahi kugombea mara
tano na hakukata tamaa na hatimaye alifanikiwa kuingia Ikulu.
Lowassa ambaye alitoa upinzani mkali kwa Rais John Magufuli katika
uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana, alisema hakubaliani na
matokeo ya uchaguzi huo, lakini anachoshukuru nchi ni salama na wananchi
wanaishi kwa amani.
Aliwataka wanamadiliko na wananchi wote waliompigia kura mwaka jana
wasikate tamaa kwa kuwa uchaguzi mkuu ujao hataibiwa tena kura.
UBAGUZI
Kuhusu sakata la wanachama wa CCM kupita na mabango yenye lugha za
ubaguzi katika sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar, Lowassa alikitaka
chama hicho kukemea suala hilo.
''Lazima ajitokeze mtu mzito na mwenye heshima ambaye anaweza
kulielezea vizuri hili na watu wakalielewa kwamba siyo msimamo wa chama
badala ya kumuachia mtu mwenye mipasho kulisemea,'' alisema.
Alisema kuna kiongozi ndani ya CCM ambaye alimuita mtu wa mipasho
(hakumtaja jina), kwamba hana uwezo wala nguvu za kulisemea jambo hilo
kama alivyofanya.
Katika sherehe hizo, kulikuwa na bango lililoandikwa 'Machotara wa
Hizbu Zanzibar ni nchi ya Waafrika' na bango hilo kupitishwa mbele ya
viongozi wa serikali katika sherehe hizo.
MKWAMO WA KISIASA Z’BAR
Kuhusu mkwamo wa kisiasa Zanzibar, Lowassa aliitaka Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), kumtangaza mshindi ambaye alidai ni Maalim
Seif Shariff Hammad.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa wanamabadiliko wafanyabishara hao wa
Kariakoo, Sevelin Mushi, alisema wako nyuma ya Lowassa licha ya kuwapo
vitisho mbalimbali.
Alisema wao kama wafanyabishara wapenda mabadiliko walifika ofisini
kwa Lowassa kumpongeza kwa kura nyingi alizopata katika uchaguzi mkuu
wa mwaka jana.
Alimuita Lowassa kuwa ni Rais wa mioyo ya Watanzania na kwamba
walikuwa naye katika safari ndefu ya kutafuta mabadiliko ya kweli.
CHANZO:
NIPASHE


0 comments :
Post a Comment