MKUU
wa wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Mohamed Utaly amekanusha taarifa za
watu wa wilayani yake kuchemsha mawe kwa ajili ya kukosa chakula
kutokana na kukithiri kwa njaa.
Akitoa
taarifa ya hali ya njaa kwa Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Maafa
kutoka ofisi ya Waziri mkuu, Mbazi Msuya, mkuu huyo wa wilaya alisema
kuna vyombo vya habari na mitandao ya kijamii imeripoti kuwa wananchi wa
wilaya ya Mpwapwa wanalazimika kupika mawe na pumba kutokana na wilaya
hiyo kukumbwa na njaa.
Utaly pamoja na kukiri kuwepo na njaa alisema waandishi wametia chumvi mno.
“Ukweli
katika wilaya yangu kuna njaa hasa vijijini, lakini njaa iliyopo
haijafika kiasi cha wananchi kula pumba au kuchemsha mawe kwa ajili ya
kuwadanganya watoto ili walale… baadhi ya kaya hula mlo mmoja kwa siku
lakini si kula pumba na kuchemsha mawe,” alisema Utaly na kuongeza kuwa chakula kipo lakini changamoto ni ukubwa wa bei.
Mmoja
wa wananchi wa kijiji cha Chunyu, Edward Kusena ambaye ni mkulima
mkubwa wa muhogo kijijini hapo alisema njaa katika kijiji hicho na
wilaya nzima imesababishwa na baadhi ya wananchi kuupuzia maagizo ya
wataalamu ya kulima mazao yanayo stahimili ukame na yanayokomaa haraka
kama muhogo, mtama na uwele kwa wilaya zenye mvua kidogo kama Mpwapwa.
Ofisa
kilimo, uvuvi na umwagiliaji wa wilaya ya Mpwapwa, Justina Munisi
alisema pamoja na kuwapo kwa njaa tayari kitengo cha maafa kutoka ofisi
ya waziri mkuu imetoa mahindi tani 200 ambayo yamegawiwa kwa vijiji 36
kati ya vijiji 68 vilivyoathiriwa na njaa.
Munis
alisema njaa hiyo imesababishwa na ukosefu wa mvua kwa msimu wa kilimo
wa mwaka 2014/2015 na wananchi kutokufuata ushauri wa kupanda mazao
yanayostahili kupandwa katika kanda za mikoa kame kama wa Dodoma na
wilaya zake.
Mbunge
wa jimbo la Mpwapwa, George Lubeleje alishukuru serikali kuwapatia
chakula cha msaada tani 200 ambazo alisema hazijakidhi kwa wananchi
wote, alitumia fursa hiyo kuiomba serikali kuongeza tena tani 200 ili
kuweza kufikia lengo na kupunguza ukali wa njaa kwa Mpwapwa.
Kwa
upande wake Msuya aliwataka viongozi wa halmashauri hiyo kuacha kuomba
chakula cha msaada bali aliwataka kuomba chakula cha njaa na mbegu ili
kuweza kuondokana na kuomba chakula cha njaa kila mwaka.
Pia
alisema kitengo chake kitaanza kugawa mbegu za muhogo bure kwa wakulima
watakaojiandikisha na kutaka kupanda zao hilo ambalo litaweza kuwa
mwarobaini wa wilaya hiyo kukumbwa na njaa kila mwaka.
0 comments :
Post a Comment