Nkupamah media:
![]() |
Mafundi wakikarabati bomba kuu la kusambaza maji toka Ruvu juu katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo jirani. |
Na Raymond Mushumbusi MAELEZO
March 1 2016
Tatizo la ukosefu wa huduma ya
maji katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam linatarajiwa kuwa
historia mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa tanki kubwa lenye uwezo
wa kuhifadhi maji lita million 10 kwa siku lililopo Kibamba.
Hayo yamebainika mara baada ya
wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dar es Salaam walipotembela
mradi huo unaofadhiliwa na nchi ya India ambapo mbali na kujionea ujenzi
wa tanki hilo pia walitembelea na kujionea ulazaji wa bomba
litakayokuwa linasafirisha maji toka vyanzo vya maji vya Ruvu Chini na
Ruvu Juu na kwenda kuifadhiwa katika tanki hilo tayari kwa kusambazwa
katika maeneo ya Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake.
Hata hivyo Disemba 31, 2015
Serikali ya Tanzania na India zilisaini mkataba wa ufadhili wa Dola
Millioni 59.3 ili kutekeleza mradi wa ulazji wa bomba la maji kutoka
Mlandizi mpaka Kimara na kuishia Kinyerezi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa
tanki hilo la Kibamba.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika
Marchi 31 mwaka huu ambapo mpaka sasa umekamilika kwa asilimia 90 ili
uanze kusambaza maji katika Mkoa wa Dar es Salaam na viunga vyake.
Mkuu wa msafara wa Kamati ya
Ushauri ya Mkoa wa Dar es Salaam alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe.
Raymond Mushi aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Said
Meck Sadiq ambaye ndio mwenyekiti wa kamati hiyo amesema lengo la kamati
hiyo ni kuona Jiji zima linakuwa na huduma ya maji safi na salama kwa
matumizi mbalimbali na kuondokana na suala la maji ya mgao linalolikumba
Jiji la Dar es salaam kwa miaka mingi.
“ Tatizo la maji litakuwa
historia katika Jiji letu maana mradi huu ni mkubwa sana na utawezesha
watu wengi kupata huduma ya maji safi na salama na tutaondokana na uhaba
wa maji katika baadhi ya maeneo na yale ambayo yalikuwa hayana kabisa
huduma ya maji kwa kipindi kirefu sana yatapatiwa huduma hiyo”
“ Nawaomba wananchi na
wafanyakazi wa Dawasco kutunza miundombinu hii kwani ni hazina kubwa si
kwetu tu hata kwa vizazi vijavyo, na ni marufuku kwa watu kujenga nyumba
katika eneo lilipopita bombala maji, alama maalum ziwekwe ili kuonesha
kuwa sehemu hii bomba limepita ili kuzuia uharibifu wa miundombinu”
Alisema Mushi.
Mara baada ya kukamilika kwa
ujenzi wa tanki la Kibamba litakuwa na uwezo wa kusambaza maji katika
maeneo yafuatayo; Ruvu, Kiluvya, Kibamba, Mbezi, Kimara, ubungo,
Segerea, hadi kinyerezi ambapo bomba linatakuwa limeishia hapo na maeneo
yote ambayo yanapata maji kupitia mtambo wa Ruvu Juu na Chini na wale
amabao bado hawajaunganishwa na huduma ya maji wataunganishwa ili waweze
kupata huduma hiyo kwa urahisi zaidi.
Aidha, mmoja kati ya wajumbe wa
kamati ya ushauri ya mkoa wa Dar es Salaam mbunge wa viti maalum Ilala
(CHADEMA) Mhe. Anatropia Theonest amesema huduma ya maji ni suala muhimu
sana kwa maendeleo ya nchi yoyote, hivyo basi Serikali iliwekee uzito
na kulitekeleza kwa nguvu zake zote na kuonya wale wanaohujumu
miundombimu ya maji kuchukuliwa hatua za kisheria, iwe ni kwa
wafanyakazi wa idara za maji au wananchi ili kuhakikisha huduma hiyo
inawanufaisha wananchi.
Kamati ya ushauri ya mkoa wa Dar es Salaam
inaundwa na wakuu wa Wilaya zote za mkoa wa Dar es salaam, Mameya wote,
wabunge wa Mkoa wa kuchaguliwa, kuteuliwa au viti maalum na kamati hiyo
inakuwa chini ya Uwenyekiti wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
0 comments :
Post a Comment