Timu
ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro
Premium Lager Jana imefanya mazoezi katika uwanja wa Omnisports Idriss
Mahamat Ouya ulipo katika jiji la D’jamena ikiwa ni maandalizi ya mchezo
dhidi ya wenyeji Chad siku ya Jumatano.
Taifa Stars imefanya mazoezi
kuanzia majira ya saa 9 alasiri, ikiwa ni sawa na muda utakaochezwa
mchezo siku ya Jumatano sawa na saa 11 kwa saa za nyumbani Tanzania na
Afrika Mashariki.
Akiongelea maandalizi ya mchezo
huo, Kocha Mkuu wa Taif Stars Charles Boniface Mkwasa amesema anashukuru
vijana wake waliotangulia wamefika salama, hakuna majeruhi na wote
wameweza kufanya mazoezi aliyoyapangilia.
“Hapa D’jamena hali ya hewa ni
joto kali tofauti na nyumbani, kwa hizi siku mbili tutakazofanya mazoezi
hapa, naimani vijana wataweza kuzoea hali ya hewa na kufanya vizuri
katika mchezo wa Jumatano” alisema Mkwasa.
Mkwasa amesema wachezaji wake
wametoka katika vilabu vyao ambavyo vilikua na michezo mwishoni mwa
wiki, wote bado wako fit kikubwa wanafanya maandalizi ya mwisho kwa
ajili ya mchezo huo.
“Hatujapata muda mrefu wa kufanya
mazoezi kwa pamoja, wachezaji walikua na majukumu katika vilabu vyao,
nashukuru wote wamewasili wakiwa salama na kesho wataungana na wachezaji
wenzao wanaokuja katika kundi la pili kwa ajili ya mazoezi ya mwisho na
mchezo wenyewe” aliongeza Mkwasa.
Rais
wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Ravia Idarus Faina ndiye mkuu wa
msafara wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, anatarajiwa kuondoka
Dar es salaam kesho Jumanne alfajiri pamoja na wachezaji wengine
kuelekea nchini Chad kwa ajili ya mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali
za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2017.
Kundi hilo la pili lenye wachezaji
8, linatarajiwa kuungana na mshambuliaji wa klabu ya TP Mazembe Thomas
Ulimwengu kesho Jumanne asubuhi Addis Ababa kisha kuunganisha safari ya
kuelekea nchini Chad wanapotarajiwa kufika saa 6 mchana.
Wachezaji wanaotarajiwa kusafiri
kesho Jumanne alfajiri kuelekea Chad kwa shirika la ndege la Ethiopia ni
Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, David Mwantika, Himid Mao,
Farid Mussa na John Bocco.
Kesho Jumanne wachezaji wote
watafanya mazoezi mepesi ya mwisho ya pamoja katika uwanja wa Omnisport
Idriss Mahamat Ouya saa 9 mchana, kabla ya kuwavaa wenyeji siku ya
Jumatano katika uwanja huo huo.


0 comments :
Post a Comment