BALOZI wa
Visiwa vya Comoro nchini Tanzania Dk. Ahamada El Badaoul Mohamed
(kushoto), akizungumza na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji
wa Serikali ya Zanzibar, Mhe. Ali Abeid Karume, mbele ya watendaji wa
wizara na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika makao makuu ya
wizra hiyo huko Kisauni Wilaya ya Magharibi B leo. (Picha na Salum
Vuai-Maelezo).
Na Salum Vuai, MAELEZO
SERIKALI ya
Mapinduzi Zanzibar na Jamhuri ya Visiwa vya Comoro, zina nafasi kubwa ya
kubadilishana uzoefu katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Aidha, nchi hizo
zimeelezewa kwamba zinapaswa kuimarisha zaidi ushirikiano wao wa miaka
mingi unaoambatana na udugu wa damu kati ya watu wa pande mbili hizo.
Balozi wa Comoro
nchini Tanzania Dk. Ahamada Badaoul Mohamed, aliyemtembelea Waziri wa
Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Mhe. Ali Abeid Karume leo, amesema
udugu wa Comoro, Zanzibar na Tanzania kwa jumla, unapaswa kuongezewa
nguvu.
Amesema nchi hizo zinapaswa kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.
Alieleza, kwa
kuwa nchi hizo ni visiwa, kuna umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika
usafiri wa baharini ambao kwa muda mrefu umekabiliwa na uhaba wa
miundombinu ya uhakika.
Dk. Badaoui
amemueleza Waziri Karume kuwa, baada ya Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed
Shein kutembelea visiwa vya Comoro miezi kadhaa iliyopita, nchi hizo
zilisaini mkataba wa ushirikiano unaofungua milango ya kuimarisha sekta
za uchumi kati yao.
Kupitia
makubaliano hayo, alisema nchi yake na Zanzibar ambazo zina vivutio
vingi vya utalii, zinalazimika kuvitumia kuongeza mapato yao kupitia
safari za kitalii miongoni mwao.
Kwa upande wa
sekta ya elimu, alifahamisha kuwa, wanafunzi wa Zanzibar wanakaribishwa
kujiunga na elimu ya juu katika vyuo vya Comoro, kama wanafunzi wa nchi
yake wanavyoweza kuja kusoma katika vyuo mbalimbali vilivyoko hapa
nchini.
“Udugu wetu wa
damu na ushirikiano wa miaka mingi, ni mambo yanayotuunganisha na lazima
sote kwa pamoja tutafute njia za kuuimarisha na kuudumisha,”
alifahamisha.
Aidha alisema
Zanzibar na Comoro zinafanana kwa mengi, ikiwemo dini na tamaduni zake,
na kwamba nchi yake inaangalia uwezekano wa kuleta wanafunzi wake hapa
nchini kwa ajili ya kujifunza muziki hasa wa taarab.
Kwa upande wake,
Waziri Karume alieleza kufarijika na ujio wa Balozi huyo, na kumtaka
ajisikie yuko nyumbani kutokana na muingliano wa watu wa pande mbili
hizo.
Waziri Karume
amesema, hatua ya Zanzibar kununua meli mpya ya MV Mapinduzi II, ni
mwanzo mzuri wa kurejesha safari za kibiashara na za kutembeleana kati
ya watu wa nchi hizo.
Alisema Zanzibar
imekumbwa na misukusuko kadhaa ya ajali za baharini, lakini sasa hilo
litabaki kuwa historia, kwani MV Mapinduzi II ina uwezo mkubwa kuhimili
vishindo vya safari kutokana na muundo wake wa kisasa.
Balozi Karume
alieleza kuwa mafungamano kati ya wananchi wa Zanzibar na Comoro kwa
upande wa dini, tamaduni na ndoa, ni daraja muhimu la kuimarisha
uhusiano wao uliodumu kwa miaka mingi.


0 comments :
Post a Comment