Mjumbe
wa Kuteuliwa wa Baraza la Wawakilishi, Hamad Rashid (ADC) ametaka
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutobabaishwa na nchi
washirika wa maendeleo kwa kususa misaada yao kwa kile alichosema,
nafasi ipo ya kutumia rasilimali zilizopo kikamilifu.
Rashid,
ambaye alikuwa mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ADC
katika uchaguzi wa marudio, alisema hayo wakati akichangia hotuba ya
rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein aliyoitoa katika uzinduzi wa
baraza la wawakilishi.
Mwakilishi
huyo alionya nchi hizo akitaka zisitumie uwezo wao kwa ajili ya
kulazimisha matakwa yao na kupinda sheria za nchi zinazotokana na
demokrasia iliopo.
Alisema
Tanzania bado inao uwezo mkubwa wa kutumia rasilimali zake zinazotokana
na utajiri mkubwa kwa ajili ya kujenga nchi na kupambana na umasikini
lakini viongozi walikuwa wakibweteka kutokana na kuwepo kwa misaada ya
nchi matajiri.
“Tusibabaishwe
na wahisani kwa tishio lao la kusitisha misaada ya maendeleo...wakati
umefika wa kufanya kazi na kutumia rasilimali zetu kikamilifu ikiwemo
kukusanya mapato na kupambana na viongozi wazembe na wabadhirifu."
Rashid
mwanasiasa mkongwe ambaye aliwahi kuwa naibu waziri wa fedha na uchumi
wa Serikali ya Muungano katika miaka ya 1987, alisema huu ni wakati wa
kuiga mfano wa nchi ya Kenya wahisani walizuia misaada kwa asilimia 80
lakini walitumia walichonacho kwa ajili ya matumizi ya ndani.
Mapema
Rashid alimpongeza Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohmed Shein kwa kumteua
kuwa mwakilishi, hatua ambayo imetimiza ndoto zake za kuunda serikali
itakayovishirikisha vyama vya siasa nchini kinyume ma matarajio ya
wapinzani.
“Hii
siyo serikali ya umoja wa kitaifa lakini ni serikali iliyowajumuisha
wananchi na vyama vyote vya siasa na sasa tupo tayari kufanya kazi kwa
ajili ya kuleta na kusimamia maendeleo kwa faida ya wananchi wote kwa
sababu uchaguzi umekwisha,’’alisema.
0 comments :
Post a Comment