UTANGULIZI:
Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu;
Mtukufu, Muumba wa Ulimwengu na vyote vilivyomo, kwa kuturuzuku neema ya uhai,
afya na uwezo wa kukutana leo hii tarehe 5 Aprili, 2016, katika tukio hili
muhimu kwa mustakbali wa nchi yetu na maendeleo ya wananchi wake.
Tunawaombea dua wenzetu waliotangulia mbele ya haki, Mwenyezi Mungu awasamehe makosa yao na awape malazi mema peponi. Kadhalika, kwa wale wenzetu waliopata mtihani wa maradhi mbali mbali, tunamuomba Mola wetu awape uzima, ili waendelee kushirikiana nasi katika shughuli za ujenzi wa Taifa letu.
Tunawaombea dua wenzetu waliotangulia mbele ya haki, Mwenyezi Mungu awasamehe makosa yao na awape malazi mema peponi. Kadhalika, kwa wale wenzetu waliopata mtihani wa maradhi mbali mbali, tunamuomba Mola wetu awape uzima, ili waendelee kushirikiana nasi katika shughuli za ujenzi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika,
Tumekutana katika shughuli hii muhimu
ya kulizindua Baraza la Wawakilishi la Tisa, tangu lilipoanzishwa miaka 36
iliyopita ikiwa ni hatua muhimu ya kukuza demokrasia, uwakilishi wa wananchi na
kuimarisha utawala bora nchini. Tunamuomba Mola wetu atupe uwezo na hekima, ili
tuweze kutumia busara na maarifa katika kutekeleza majukumu yetu ya kikatiba na
kisheria kwa ajili mafanikio ya wananchi wa Zanzibar, kwa kuzingatia mamlaka
kilichopewa chombo hiki muhimu, katika Sura ya Tano ya Katiba ya Zanzibar ya
mwaka 1984, pamoja na kanuni nyengine zinazoongoza Baraza hili.
Baada ya kumshukuru Mola wetu Subhana
Wataala na kulitakia baraka Baraza letu la Tisa la Wawakilishi tunalolizindua
leo, napenda niitumie fursa hii ili nimpongeze kwa dhati Mheshimiwa Zubeir Ali
Maulid kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar. Kuchaguliwa kwako kwa kura nyingi kuongoza
mhimili huu wa dola, ni kielelezo cha imani waliyonayo waheshimiwa wajumbe
kwako kutokana na hekima, busara, uadilifu, taaluma na uzoefu wako. Hapana shaka wala khofu kuwa waheshimiwa
wawakilishi watashirikiana nawe katika kuyatekeleza majukumu yako na kuleta
ufanisi katika utendaji wa Baraza hili Tukufu.
Kadhalika, natoa shukurani kwa
Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza hili la Wawakilishi, kwa kuamua kwa dhati
kugombea nafasi ya ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa lengo la kuja
kuwatumikia wananchi wa Zanzibar. Aidha,
nakupongezeni kwa kuchaguliwa na wananchi huku mkielewa kuwa ushindi huo una
maana ya kuchukua dhamana ya kuwatumikia wananchi tunaowawakilisha na
Wazanzibari wote. Wananchi waliokuchagueni wana imani na mategemeo makubwa
kwenu katika kushirikiana nao kwenye suala zima la kuwaletea maendeleo. Mwenyezi
Mungu akuwezesheni kuyakidhi matarajio hayo ya wananchi wetu. Naamini kwa dhati
ya moyo wangu kwamba mtafanya kazi zenu kwa kushirikiana na kwa kuzingatia
matakwa ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na kanuni za Baraza la Wawakilishi.
Mheshimiwa
Spika,
Kwa mara nyengine, natoa shukurani
zangu za dhati kwa wananchi wote wa Zanzibar kwa kupiga kura kwa amani katika
uchaguzi wa marudio hapo tarehe 20 Machi, 2016 na kukichagua Chama cha
Mapinduzi na wagombea wake wote na tukashinda kwa kishindo. Wananchi waliitumia
vyema haki yao ya kidemokrasia ya kuwachagua viongozi wao na hasa nyinyi
Waheshimiwa Wawakilishi mnaounda Baraza la Tisa la Wawakilishi. Nakupongezeni
sana kwa kuchaguliwa kwenu.
Kwa mara nyengine, natoa shukurani
zangu za dhati kwa Chama changu, Chama cha Mapinduzi, kwa kuniamini na
kuniteua, kukiwakilisha katika kuwaomba ridhaa wananchi wa Zanzibar ya
kunichagua niwe Rais wa Zanzibar, katika uchaguzi wa tarehe 20 Machi,
2016. Natoa shukurani kwa CCM, Viongozi,
Wanachama, Wapenzi wa CCM wa ngazi mbali mbali na wananchi kwa kuniunga mkono
na kukiwezesha chama chetu kupata ushindi wa asilimia 91.4. Matokeo haya
yamekiwezesha chama chetu kupata mamlaka ya kuunda tena Serikali, kwa mujibu wa
Katiba ya Zanzibar ya 1984. Hatua hiyo,
itatupa fursa ya kuitekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 pamoja
na sera na mipango mengine ya maendeleo ambayo tulianza kuitekeleza katika
kipindi cha kwanza cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba.
Kadhalika, natoa shukurani kwa viongozi
wa vyama vyote vya siasa vilivyoshiriki katika uchaguzi na kuheshimu uamuzi wa
wananchi wa kuwachagua viongozi wao katika uchaguzi uliokuwa huru na haki. Aidha, shukurani zangu maalum nazitoa kwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama vya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kwa kusimamia ulinzi wa nchi yetu katika kipindi chote cha kabla ya uchaguzi,
wakati wa uchaguzi hadi hivi leo. Vile
vile, naipongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC); kwa kutekeleza vyema
majukumu yake ya kisheria na kikatiba, hali ambayo iliwawezesha wananchi kupata
haki yao ya kupiga kura kwa amani, salama na utulivu mkubwa.
Mheshimiwa
Spika,
Kwa sasa, uchaguzi umekwisha na
wananchi wamekipa tena Chama cha Mapinduzi ridhaa ya kuiongoza Zanzibar. Nasaha
zangu kwenu, Waheshimiwa Wawakilishi na wananchi wote, ni kuwa tuendeleze umoja
wetu na mshikamano kwa maslahi ya wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote
kwani sote ni wamoja na uchaguzi usiwe chanzo cha kuhasimiana na kukwamisha
malengo yetu ya kuongeza kasi ya maendeleo nchini.
KAZI
ILIYO MBELE YETU
Mheshimiwa
Spika,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Awamu ya Saba, katika kipindi chake cha pili itaweka vipaumbele kwa sekta mbali
mbali kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2015 – 2020 pamoja
na ahadi nilizozitoa kwa wananchi, wakati nikiomba ridhaa ya kunichagua pamoja
na wagombea wenzangu wa Chama cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu
uliomalizika. Tuna kila sababu ya
kushirikiana katika kutekeleza majukumu yetu, jambo ambalo ni muhimu katika
kuimarisha huduma za jamii, amani, umoja na mshikamano baina yetu, pamoja na
kutekeleza wajibu wetu wa kudumisha na kuendeleza shabaha ya Mapinduzi Matukufu
ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari, 1964.
Katika kuelezea kazi iliyo mbele yetu,
nitaeleza kwa ufupi tu pale ambapo itakuwa lazima kuyaeleza mambo tuliyoyafanya
na tukapata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita; kwani
mambo hayo nilikwishayaeleza kwa kina
katika hotuba yangu niliyoiwasilisha wakati nilipolivunja Baraza la Nane la
Wawakilishi tarehe 26 Juni, 2015.
UCHUMI
Mheshimiwa
Spika,
Ukuzaji wa uchumi ni wajibu wa msingi
wa Serikali ili iweze kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuwaletea
maendeleo. Ninashukuru kuona kwamba, tunaanza Kipindi cha Pili, cha Awamu hii
ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (2015–2020), tukiwa tumepiga hatua
kubwa katika kujenga misingi imara ya kuimarisha uchumi wetu. Katika kipindi
cha miaka mitano ya kwanza, kasi ya ukuaji wa uchumi ilikua ni ya kuridhisha,
ambapo katika mwaka 2015 uchumi wetu ulikua kwa
asilimia 6.6. Kasi hii ya ukuaji
Pato la Taifa imechangiwa zaidi na kuimarika kwa sekta ya huduma, sekta
ya viwanda, kuongezeka kwa idadi ya watalii walioingia nchini pamoja na
kuendelea kuwepo kwa hali ya amani na utulivu.
Pato la Taifa liliweza kuongezeka
kutoka TZS bilioni 1,050.8 mwaka 2010
kufikia TZS bilioni 2,133.5 mwaka 2014,
sawa na ongezeko la asilimia 103. Aidha, Pato la Mtu binafsi liliongezeka
kutoka TZS 856,000 sawa na Dola za Kimarekani 613 mwaka 2010 hadi kufikia TZS
milioni 1.552 sawa na Dola za Kimarekani 939 mwaka 2014. Kasi ya mfumko wa bei
imeendelea kushuka kutoka asilimia 6.1 mwaka 2010 kufikia asilimia 5.6 mwaka
2014 na asilimia 5.7 mwaka 2015. Katika kipindi chote hicho, kasi ya mfumko wa
bei iliendelea kudhibitiwa na kuwa katika wastani wa tarakimu moja.
Lengo la Serikali ninayoiongoza, ni
kuhakikisha kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi inafikia asilimia 8-10 katika miaka
mitano ijayo. Shabaha yetu tufikie
kiwango cha uchumi wa nchi zenye kipato cha kati, kama ilivyoelekezwa na
kusisitizwa katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2015-2020, Dira ya
Maendeleo 2020 pamoja na mipango mingine ya maendeleo.
Tutahakikisha kwamba tunaimarisha
ustawi wa wananchi kwa kuongeza zaidi Pato la Mtu binafsi kutoka kiwango
tulichokifikia hivi sasa, cha wastani wa TZS milioni 1.552 sawa na Dola za
Kimarekani 939 hadi kufikia kiwango cha Pato la Mtu binafsi kwa nchi zenye
kipato cha kati ambacho kinaanzia Dola za kimarekani 1,046.
Katika kipindi cha mwaka 2010/2011 hadi
mwaka 2014/2015, tumeweza kwa kiasi kikubwa kuongeza ukusanyaji wa mapato
kutoka TZS bilioni 181.4 hadi TZS bilioni 362.8, sawa na ukuaji wa asilimia 100
kwa kipindi hicho. Haya ni mafanikio makubwa na napenda kutumia fursa hii
kuipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB)
kwa juhudi kubwa walizochukua za kuimarisha ukusanyaji wa Mapato.
Dhamira ya Serikali katika kipindi hiki
cha pili, cha Awamu ya Saba ni kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kutoka
TZS bilioni 362.8 mwaka 2014/2015 hadi
kufikia TZS bilioni 800 ifikapo mwaka 2020/2021. Waheshimiwa Wajumbe tuna
wajibu na kazi kubwa ya kufanya ili tuweze kuyafikia malengo hayo na Zanzibar
iweze kwenda sambamba na kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi nyingi zinazoendelea.
Mheshimiwa
Spika,
Licha ya mafanikio makubwa tuliyoyapata
katika ukusanyaji wa Mapato, imani yangu ni kuwa bado tunaweza kuongeza
ukusanyaji wa mapato kwa kiasi na kwa kasi kubwa zaidi. Matumaini yangu ni kuwa katika kipindi cha
pili, watendaji wa Taasisi zetu muhimu za kukusanya mapato hasa Bodi ya Mapato
ya Zanzibar (ZRB), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Taasisi zilizoko
bandarini, viwanja vya ndege na Wizara zenye vyanzo vya mapato wataongeza kasi
katika kusimamia majukumu yao, wakitambua kuwa Serikali itakuwa inafuatilia
utendaji wao kwa karibu na kwa umakini zaidi. Ufanisi katika mambo hayo ndio
utakaotuwezesha kuyafikia malengo tuliyojiwekea katika Dira ya Maendeleo ya
mwaka 2020.
Hatua hii itakuwa muhimu katika kupunguza utegemezi wa
wahisani hatua kwa hatua ili baadae tuweze kujitegemea katika kupanga na
kutekeleza mipango yetu ya maendeleo katika miaka ijayo. Tutafanya kila
tuwezalo liliomo kwenye uwezo wetu ili tufanikiwe. Tumeamua kubana matumizi kwa kuyaondoa na
kutoyafanya mambo ambayo si ya lazima.
Katika kipindi hiki, tutajitahidi
kupanga vipaumbele vichache vinavyotekelezeka kwenye wizara zetu, kwa kutumia
uwezo tulio nao na mapato yetu. Tunataka
tuanze kujitegemea na hilo ni lazima tuliweze.
Nataka Mawaziri na Makatibu Wakuu washirikiane katika kulifanikisha
jambo hili. Tutaendelea kupokea misaada kutoka kwa wahisani wetu pale
tutakapopewa na tutashirikiana nao kwa ajili ya maendeleo yetu.
Mheshimiwa Spika,
Mipango yote ya nchi yetu, inasimamiwa
na kuratibiwa na Tume ya Mipango ya Zanzibar. Katika mwaka 2015, Serikali
kupitia Tume ya Mipango imeratibu mapitio ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na
Kupunguza Umasikini (MKUZA II) unaomaliza muda wake mwezi wa Juni 2016. Kazi hii inafanywa kwa kuwashirikisha
wahusika mbali mbali kuhakikisha kuwa mpango wa muda wa kati ujao, unakuwa
wenye ufanisi zaidi. Serikali itaanza kutumia rasmi mkakati huo mpya, kuanzia
bajeti ya mwaka 2016/17.
Mkakati huo utaendeleza mageuzi ya
kiuchumi na kijamii ili kutuwezesha tufikie uchumi wa kipato cha kati ifikapo
mwaka 2020. Katika kipindi hiki hadi
mwaka 2020, mkakati utajikita katika kuimarisha uchumi endelevu kwa kukuza
uzalishaji kwenye sekta ya kilimo, utalii na viwanda vidogo vidogo. Vile vile, mkakati huo utaimarisha rasilimali
watu, ubora wa huduma za jamii ikiwemo elimu, afya, mazingira endelevu na
misingi imara ya utawala bora.
MIRADI
YA MASHIRIKIANO BAINA YA SEKTA YA UMMA NA SEKTA BINAFSI (PPP)
Mheshimiwa
Spika,
Serikali inatambua umuhimu wa
kuishirikisha Sekta Binafsi katika kuleta na kusimamia maendeleo ya kijamii na
kiuchumi. Miradi ya PPP, itaongeza
ajira, uimarishaji wa huduma na ukuaji wa uchumi. Kadhalika, hii ni njia bora ya kukabiliana na
changamoto ya upatikanaji wa fedha za kuendeshea miradi. Ili kuleta ufanisi kwa miradi ya PPP,
Serikali imefuta Sheria Namba 1 ya mwaka 1999 ya Miradi ya Maridhiano na
imetunga Sheria mpya ya PPP; Namba 8 ya mwaka 2015.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo,
Serikali itatekeleza Miradi ya PPP, baada ya kuifanyia Upembuzi Yakinifu miradi
10 ya awali ikiwemo Ujenzi wa Kituo cha daladala Kijangwani, Mradi wa
Uendelezaji wa Soko la Mwanakwerekwe, Mkokotoni, Kinyasini, Soko la Mombasa kwa
Unguja na Kengeja kwa Pemba. Miradi
mengine ni Kituo cha Mikutano cha SUZA, Mradi wa Ujenzi wa Nyumba katika Mji
Mkongwe pamoja na Mradi wa Hifadhi ya Mji wa Ng’ambo. Kadhalika, miradi mengine
itakayotekelezwa ni Kuendeleza Vivutio vya Utalii katika eneo la Bandari ya
Malindi, Uanzishwaji wa Kituo cha Usarifu wa Mazao, Kuanzishwa kwa Viwanda vya
Usarifu wa Mazao ya Baharini, Kuendeleza Viwanja vya Ndege pamoja na Ujenzi wa
viwanja vya michezo ya aina mbali mbali. Ninaihimiza na ninaishajiisha Sekta
Binafsi ijiandae kutumia fursa hizo kikamilifu.
MATOKEO
KWA USTAWI (RESULTS FOR PROSPERITY-R4P)
Mheshimiwa
Spika,
Katika utekelezaji wa Mpango wa Matokeo
kwa Ustawi, mnamo mwaka 2014, Serikali iliandaa programu maalum za
utekelezaji wa shughuli mbali mbali kupitia utaratibu wa Maabara katika Sekta
ya utalii, Uimarishaji wa biashara na Upatikanaji wa rasilimali fedha.
Utekelezaji wa programu hizi umefikia hatua ya
Kukamilika kwa Sera na Sheria ya Mashirikiano baina ya Sekta ya Umma na
Sekta Binafsi, Kuandaliwa kwa Rasimu ya Mkakati wa Mawasiliano ya Utalii,
Kuanzishwa kwa mchakato wa Mfumo wa Kisasa wa Upatikanaji wa Soko kwa kutumia
Mtandao unaotegemewa kuwa na lugha 5 za Kimataifa, pamoja na Kukamilika na
Kuidhinishwa kwa Mpango Mkuu wa Matumizi
ya Ardhi.
Hatua nyengine ni kuandaliwa kwa Rasimu
ya Awali ya Mapendekezo ya Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali, kutayarishwa kwa
Rasimu ya Mapitio ya Sheria ya Uwekezaji ambayo inaendelea kufanyiwa kazi
pamoja na kuanza kwa matayarisho ya ununuzi wa Mashine za Kisasa za Kutolea
Risiti (EFD) kwa lengo la uimarishaji wa ukusanyaji wa mapato. Kwa sasa, Serikali imo katika matayarisho ya
Maabara ya elimu na afya zinazotarajiwa kufanyika mwaka huu. Serikali
imejiandaa vya kutosha katika kutekeleza programu zitakazoibuliwa na matokeo
yatakayoafikiwa na wataalamu katika maabara, kwa sekta nyenginezo, katika
kipindi chote cha miaka mitano ijayo.
Programu hizo zitaleta msukumo na kuongeza ufanisi katika juhudi zetu za
kukuza uchumi, ajira na kupunguza umasikini.
UWEKEZAJI
VITEGA UCHUMI
Mheshimiwa
Spika,
Katika kuendeleza juhudi za kukuza
uchumi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia Mamlaka ya Ukuzaji Vitega
Uchumi Zanzibar (ZIPA), imeweza kuitangaza Zanzibar kama kituo muhimu kwa
wawekezaji, ndani na nje ya nchi.
Zanzibar imeweza kuwavutia wawekezaji katika miradi mbali mbali ya
gharama kubwa kutokana na fursa za uwekezaji zilizopo, mazingira mazuri kwa
wawekezaji na biashara, pamoja na kuimarika kwa utawala bora nchini.
Mheshimiwa
Spika,
Katika kuendeleza juhudi za kuvutia
uwekezaji katika Maeneo Huru ya Uchumi ya Fumba, Serikali imefunga mkataba na
Bakhresa Group of Companies ili kujenga miundo mbinu katika eneo ambalo Mpango
Mkuu wa Uwekezaji umeshaidhinishwa katika kipindi hiki cha miaka 5. Jumla ya kilomita 13 za barabara kuu zimeanza
kujengwa ambazo zitagharimu jumla ya TZS. bilioni 15.6 na barabara ndogo zenye
urefu wa kiasi cha kilomita 20 zitajengwa kwa kiwango cha lami zitakazogharimu
TZS. bilioni 20.
Jumla ya miradi mikubwa mitano (5)
itajengwa kwenye eneo hilo, katika kipindi hiki. Miradi hiyo ni ujenzi wa Miji ya Kisasa wa
Kibiashara “Fumba Satellite City” katika eneo la Fumba, ujenzi wa Mji wa kisasa
wa Makaazi “Fumba Town Development”
katika eneo la Nyamanzi, ujenzi wa Mji wa kisasa wa Nyumba za Biashara
na Makaazi pamoja na ujenzi wa Maeneo ya Kupumzikia Watu “Fumba Uptown Living” katika eneo la Fumba.
Vile vile, eneo lenye ukubwa wa hekta
102 limetengwa huko Fumba, kwa ajili ya ujenzi wa viwanda ambapo viwanda viwili
vya ujenzi wa nyumba katika vijiji vya Kororo na Nyamanzi tayari
vimeshajengwa. Aidha, mtambo wa lami
umeshafungwa katika eneo la Kororo na kiwanda cha maziwa kimeshaanza kazi. Katika uimarishaji wa eneo hili, vile vile,
kitajengwa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa na eneo maalum la kiuchumi pamoja
na Gati ya mizigo na abiria.
Vile vile, Kampuni ya S.S. Bakhresa
“Group of Companies” tayari imepata ruhusa na inaendelea na hatua mbali mbali
za uwekezaji mkubwa katika maeneo ya Mtoni Marine - Maruhubi. Mradi huo unajumuisha ujenzi wa Hoteli kubwa
ya nyota tano; Maeneo ya michezo ya maji (Water Park); “Marina” na kujenga
Kisiwa chenye nyumba za watu wenye kipato cha juu (Chapwani Paradise Island)
Kusini mwa Kisiwa cha Chapwani.
Mheshimiwa
Spika,
Kwa upande wa Mkoa wa Kaskazini Unguja,
Mradi wa ujenzi wa mji wa kisasa wa kibiashara pamoja na hoteli kubwa ya nyota
tano umekwishaanza kutekelezwa huko Matemwe na unatarajiwa kugharimu jumla ya
Dola za Marekani milioni 800. Kampuni ya
“Pennyroyal ya Gibralter” ndiyo inayotekeleza mradi huo.
Aidha, mnamo mwezi wa Novemba 2015,
Serikali ilifunga Mkataba na Kampuni ya “Quality Group Limited” ambayo
itaanzisha mradi mkubwa wa kuendeleza Hoteli ya Bwawani na maeneo
yaliyoizunguka. Mradi huo utawekeza mtaji wa Dola za Marekani kiasi cha Milioni
200 na utahusisha kulifanyia matengenezo makubwa jengo la Hoteli ya Bwawani na
kuwezesha upatikanaji wa huduma za hoteli za nyota tano. Jengo hili la hoteli
litaimarishwa ili kuhifadhi kielelezo cha mafanikio cha Mapinduzi Matukufu ya
Zanzibar ya 1964. Majengo ya biashara ya
ghorofa na maduka makubwa ya kisasa (Shopping malls) yatajengwa pamoja na Kituo
cha Mikutano ya Kimataifa, Maeneo ya Michezo na Soko la Bidhaa zinazozalishwa
Zanzibar.
Ni matumaini yangu kwamba Wajumbe wa
Baraza hili, mtashirikiana na Serikali katika kuhakikisha mipango hii muhimu ya
uwekezaji inatekelezwa ipasavyo na malengo ya Zanzibar ya kuwa na uchumi wa
kati yanafikiwa kwa manufaa ya nchi yetu na watu wake.
Mheshimiwa
Spika,
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo,
Serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) itaendelea na ujenzi
wa nyumba za kisasa uliokwishaanza katika eneo la Mbweni - Unguja, ambao
unajumuisha majengo 18 ya ghorofa 7 kila moja. Majengo hayo yatakapomalizika
yatakuwa na jumla ya vyumba 252. Ujenzi
huu unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miaka mitatu. Vile vile, kwa
kushirikiana na Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ), ZSSF itajenga
nyumba 128 za gharama nafuu katika eneo linalomilikiwa na umoja huo wa UWZ
lilioko Mombasa - Zanzibar.
Zaidi ya hayo, Mfuko wa Hifadhi ya
Jamii (ZSSF), italifanyia matengenezo makubwa jengo la ‘CHAWAL’ tunaloliita
“Jumba la Treni” liliopo Darajani.
Ujenzi huu unategemewa kuanza hivi karibuni. Aidha, Serikali inaandaa
mpango na inaendelea na mazungumzo na
wawekezaji mbali mbali kwa ajili ya kuliendeleza eneo la Darajani kwa ujenzi wa
maduka makubwa ya kisasa ya biashara.
Kwa upande wa eneo la Michenzani,
Serikali kupitia ZSSF imeandaa awamu ya pili ya mradi wa uimarishaji wa eneo la
hilo baada ya kukamilika kwa Mnara wa kumbukumbu ya Miaka 50 ya Mapinduzi na
bustani yake. Serikali imejipanga kujenga maduka ya kisasa (shopping malls) na
sehemu za kupumzikia katika eneo hilo.
Mheshimiwa
Spika,
Wahenga walisema, “Ukipata chungu kipya, usitupe cha zamani”. Katika kipindi kijacho,
Serikali itahakikisha inachukua hatua madhubuti katika kuuhifadhi Mji Mkongwe,
ili uendelee kuwa kivutio cha utalii na kubakia katika orodha ya Mji wa Urithi
wa Dunia. Tutaendelea kuyafanyia ukarabati majengo mbali mbali ya kihistoria. Vile vile, tutakamilisha mradi wa ZUSP wa
ujenzi katika eneo la Mizingani, utiaji wa taa za barabarani katika barabara
mbali mbali, ujenzi wa misingi ya maji machafu
katika Mji wa Unguja, Mji wa Chake chake, Wete na Mkoani kwa Pemba. Kupitia Baraza hili Tukufu,
nataka niwahimize viongozi wa
Manispaa, Mabaraza ya Miji, Halmashauri za Wilaya, Mamlaka ya Mji
Mkongwe na Taasisi zote zinazoshughulika na usafi wa Miji na usimamizi wa
biashara, waongeze jitihada katika kuimarisha usafi wa Mji na kusimamia sheria
na nidhamu ya uendeshaji wa shughuli za biashara. Usafi ni jambo la lazima katika maisha yetu
na hapana mbadala wake. Kwa hivyo, wale
wote waliopewa dhamana ya kusimamia usafi katika Miji yetu, wajue kuwa
wanachukua dhamana kubwa na watawajibishwa endapo watashindwa kutimiza wajibu
wao katika kipindi hiki.
UIMARISHAJI
WA MIJI KWA KUZINGATIA MKAKATI WA
MATUMIZI YA ARDHI ZANZIBAR - 2015
Mheshimiwa
Spika,
Katika mwaka 2015, tulikamilisha
Mkakati wa Matumizi ya Ardhi Zanzibar (National Spatial Development Strategy -
2015). Katika Mkakati huu, Miji Kumi na
Nne (14) itapangwa, ikiwemo Mji wa Zanzibar, Chake-Chake, Wete, Mkokotoni,
Konde na Kengeja. Kati ya Miji hiyo, Serikali imekamilisha mipango ya miji
mitano ambayo ni Mji wa Zanzibar, Nungwi, Mkokotoni, Chwaka na Makunduchi. Matayarisho
ya mipango ya miji ya Chake-Chake na Wete imeshaanza.
Vile
vile, katika mwaka uliopita, Serikali ilikamilisha Mpango Mkuu wa Mji wa
Zanzibar. Katika Mpango huo, Serikali
imeamua kuanzisha eneo jipya la Biashara na Utamaduni. Eneo lote kutoka Darajani hadi Kariakoo na
kutoka Maisara hadi Kinazini litapagwa upya ili kuanzisha ujenzi wa nyumba za
ghorofa, kuweka kituo kipya cha mabasi, kuongeza sehemu mpya za maduka na
biashara na kujenga sehemu mpya za bustani. Aidha, Mji wa Zanzibar utakuwa na
miji mitatu mipya; Chuini kwa upande wa Kaskazini, Tunguu kwa upande wa
Mashariki na Fumba kwa upande wa Kusini. Mipango hii inafanywa kuhakikisha kuwa
Zanzibar inaendelea ikiwa na uwiyano wa kiuchumi, kijamii na kimazingira,
ili kufikia lengo lake la Milenia na kuelekea katika Malengo Mapya ya Maendeleo
Endelevu (Sustainable Development).
BIASHARA
Mheshimiwa
Spika,
Sekta ya biashara ina umuhimu mkubwa
kwa kuchochea maendeleo na kukuza ajira kwa watu wa Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
awamu zote imekuwa ikichukua hatua za kuiimarisha na kuiiongezea ufanisi sekta
hii. Katika kipindi cha pili, cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya
Saba, Serikali itahakikisha kuwa inaendelea kuimarisha mazingira na wepesi wa
kuendesha shughuli za biashara hapa Zanzibar. Nitahakikisha kuwa tunafanikiwa
kukuza biashara za ndani,
biashara kati ya Zanzibar na Tanzania Bara na
kati ya Zanzibar na nchi
Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
pamoja na Mataifa mengine ya nje. Lengo
letu ni kuongeza bidhaa zitakazouzwa
Tanzania Bara ili zivuke kiwango cha mwaka 2014/15, cha bidhaa zenye
thamani TZS. Milioni 2,203.8. Kadhalika, tuvuke kiwango cha bidhaa zenye
thamani ya TZS. milioni 133,591.7 zilizosafirishwa kwenda nchi za nje mwaka
2014/2015.
Ili kuyafikia malengo hayo, Serikali
itaendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara juu ya fursa zilizopo na utumiaji
mzuri wa masoko yaliyopo Tanzania pamoja na Jumuiya za Kiuchumi ambazo Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ni mwanachama. Serikali itaanzisha ujenzi wa Kituo cha Biashara cha Kimataifa katika eneo la
Nyamanzi na itaendelea kuwahamasisha
wafanyabiashara na wajasiriamali wa
Zanzibar ili washiriki katika maonesho ya biashara ya Kimataifa yatakayofanyika
hapa Zanzibar na nchi mbali mbali.
Katika kudhibiti ubora wa bidhaa na
huduma zinazotolewa na wananchi, Serikali itaimarisha Taasisi ya Viwango ya
Zanzibar iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria Namba 1 ya Viwango ya Zanzibar ya
mwaka 2011, kwa kuanza ujenzi wa Ofisi
na Maabara ya kisasa katika eneo la Maruhubi ili kuimarisha ufanisi wa taasisi
hiyo.
Mheshimiwa
Spika,
Kwa kutambua umuhimu wa zao la karafuu
kwa uchumi na historia ya Zanzibar na watu wake, Serikali inaendeleza juhudi
mbali mbali za kuliimarisha zao hili. Katika kipindi cha miaka mitano
iliyopita, tumepata mafanikio makubwa katika kulifufua zao hilo. Tulianzisha
mpango maalum wa miaka 10 wa kulifufua na kuliendeleza zao hili na kwa
kulifanyia mageuzi makubwa Shirika la ZSTC ambalo kwa sasa linaendeshwa kwa
ufanisi mkubwa.
Kwa mara nyengine, nawaahidi wananchi kuwa Serikali itaendelea
kuwalipa wakulima wa karafuu asilimia 80 ya bei ya karafuu ya soko la dunia
kama nilivyoahidi katika kipindi kilichopita.
Serikali itaendelea kuwapa mikopo na miche wakulima kutoka kwenye vitalu
tulivyovianzisha. Tutaendeleza vita dhidi ya magendo na tutaendelea
kuliimarisha Shirika la ZSTC, ili liendelee kusimamia vizuri biashara ya
karafuu na viungo vyengine ili lijiendeshe kibiashara na liendelee kupata
faida. Wito wangu kwa wananchi na wakulima wa karafuu ni kuwa, tushikamane
katika kuyaendeleza mafanikio haya. Vile
vile, Serikali itaendeleza ujenzi wa barabara za ndani zinazoelekea kwenye
maeneo yenye karafuu nyingi. Jumla ya
barabara nne zitajengwa kwenye maeneo mbali mbali katika kipindi hiki.
Mheshimiwa
Spika,
Katika kipindi hiki, Serikali
itaendeleza utaratibu wa kudhibiti ubora wa karafuu za Zanzibar (Branding) ili
kumnufaisha mkulima wa zao la karafuu.
Hatua ya awali ya vyeti vya kudhibiti ubora kutoka “TBS” na “Tan-cert”
umepatikana. Usajili utapangwa kwa wakulima pamoja na wanaojishughulisha na
biashara ya zao la karafuu kwa ajili ya kuwawezesha kwa kuwapatia misaada mbali
mbali. Jitihada zitafanywa ili waweze
kuendesha shughuli zao kwa ufanisi pamoja na kuwalipa fidia wale wanaopata ajali
katika uchumaji wa karafuu. Shirika
litaweka utaratibu wa kuwepo kwa karafuu
kwa mfumo wa kilimo hai (Organic cloves).
Mazao mengine ya mfumo wa kilimo hai
tayari yameshaandaliwa utaratibu wake.
Mazao hayo ni Pilipili hoho, Pilipili manga, na Mdalasini kazi ya kutoa
elimu ya ulimaji wa mazao hayo inaendelea.
Maeneo ambayo yamepatiwa elimu hai ni Matemwe (Pilipili hoho) na
Dayamtambwe na Gando (Mdalasini na Pilipili manga).
VIWANDA
Mheshimiwa
Spika,
Nafahamu kwamba, tunaanza kipindi cha
pili cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba ikiwa bado
tumekabiliwa na changamoto nyingi katika kuiendeleza sekta ya viwanda. Miongoni
wa sababu za kuwepo kwa changamoto hizo ni uchache wa rasilimali tulizonazo
hapa Zanzibar ambazo zingeweza kutumika zikiwa ni malighafi kwa kuendeleza
viwanda vya aina mbali mbali. Wakati wa kampeni za Uchaguzi wa mwaka 2015,
katika nyakati mbali mbali nilielezea kuhusu juhudi pamoja na mipango yetu ya
kuendeleza viwanda, hasa viwanda vya kusindika samaki, mazao ya kilimo na
mifugo, viwanda vya ushoni na viwanda vyengine vidogo vidogo.
Nataka niwahakikishie wananchi kuwa
katika kipindi cha miaka mitano ijayo, nitasimamia utekelezaji wa ahadi hiyo
niliyoitoa wakati wa Kampeni huku tukishirikiana na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Tutazidisha kasi ya kutafuta wawekezaji wenye mitaji
mikubwa, uwezo na dhamira ya kweli ya
kujenga viwanda katika eneo huru la huko Micheweni vitakavyokuwa na uwezo
mkubwa wa kutoa ajira kwa vijana wetu, kama tulivyokwishaanza kwa eneo la
Fumba. Kadhalika, Serikali itaendeleza viwanda katika Maeneo Maalum ya Kiuchumi
(SEZ) na kuwavutia wawakezaji wenye mitaji mikubwa kuwekeza katika miundombinu
ya viwanda vinavyotoa ajira kwa wingi.
UTALII
Mheshimiwa
Spika,
Ni jambo la kutia moyo kuona kwamba
tumemaliza miaka mitano ya kwanza tukiwa tumepata mafanikio makubwa katika
kuiendeleza sekta ya utalii ambayo hivi sasa ndiyo sekta kiongozi katika uchumi
wetu. Jitihada zetu za kuendeleza utalii
kwa wote na kufikia azma yetu ya kuufanya utalii kuwa sekta kiongozi ya uchumi,
zimeweza kuzaa matunda. Tumeweza kuongeza idadi ya watalii, kutoka 132,836
mwaka 2010 hadi kufikia 311,891 mwaka 2014. Hata hivyo, idadi ya watalii
waliotembelea Zanzibar katika mwaka 2015 ni 294,243.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo,
tutaongeza kasi ya kuiimarisha sekta ya utalii ili tuweze kulifikia lengo
lililobainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 – 2020, la
kufikia idadi ya watalii 500,000, wanaoitembelea Zanzibar kwa mwaka, ifikapo
mwaka 2020. Serikali itaongeza kasi ya utekelezaji wa Matokeo kwa Ustawi
(Results for prosperity), mafanikio ya utalii kwa wote, kushajiisha ushiriki wa
wananchi katika sekta ya utalii na kuhusisha sekta zetu zote za kiuchumi na
shughuli za utalii. Serikali itaongeza kasi katika kuvitangaza vivutio vyetu
vya utalii pamoja na uzuri wa Zanzibar na ukarimu wa watu wake katika masoko
mapya katika Bara la Ulaya, Marekani, Mashariki ya Kati na Mashariki ya Mbali.
Mheshimiwa
Spika,
Tutaendelea kuwashajiisha wawekezaji
ili waje wawekeze katika ujenzi wa hoteli za kisasa na utoaji wa huduma huku
tukiwa tumeelekeza nguvu kubwa katika kuimarisha utalii unaozingatia hifadhi ya
mazingira na kuulinda utamaduni wetu. Katika kipindi hiki, Chuo cha Utalii cha
Maruhubi kitaunganishwa na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), ili
kuimarisha utoaji wa mafunzo ya utalii kwa kutoa shahada za fani mbali
mbali. Mafunzo haya yatasaidia katika
kuimarisha sekta ya utalii na kuongeza ajira za vijana.
Katika
kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itaongeza juhudi za kuziimarisha
sehemu za kihistoria na kufanya matengenezo ya Makumbusho pamoja na kufanya
uhifadhi wa mapango ya asili kwa lengo la kuyatunza na kuchochea shughuli za
utalii. Kadhalika, Serikali itaendeleza utekelezaji wa Mpango wa Uhifadhi wa
Mambo ya Kale na kuanzisha Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu za Kale pamoja na
vituo vya kuhifadhia kumbukumbu katika kila Mkoa.
KILIMO
Mheshimiwa
Spika,
Sekta ya kilimo ina umuhimu mkubwa na
inachangia asilimia 31 katika Pato la Taifa (GDP). Kilimo huchangia katika
kuwawezesha wananchi walio wengi kujikimu kimaisha na kuwapatia uhakika wa
chakula na lishe bora. Sekta ya kilimo
ilipata mafanikio makubwa katika kipindi kilichopita kutokana na utekelezaji wa
miradi na programu mbali mbali za kilimo. Tutayaendeleza mafanikio pamoja na
kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazoendelea kuwakabili wakulima wetu. Katika
kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya kilimo kwa
kuendelea kutoa ruzuku ya asilimia 75 ya gharama za pembejeo za kilimo na
huduma za matrekta kwa wakulima kama tulivyoanza katika kipindi cha kwanza.
Aidha, Serikali itaendeleza programu za mapinduzi ya kilimo na usimamizi wa
rasilimali za misitu na kuongeza idadi ya mabwana/mabibi shamba kutoka 172
mwaka 2014 hadi kufikia mmoja kwa kila shehia ifikapo mwaka 2020. Vile vile, tutaendeleza mafunzo kwa wakulima
na kutilia mkazo matumizi ya kanuni za kilimo bora katika uzalishaji wa mazao
ya chakula na biashara pamoja na matumizi ya zana za kisasa.
Vile vile, kilimo cha mpunga cha
umwagiliaji maji kitaimarishwa kwa kuzingatia Mpango Mkuu wa Kilimo cha
Umwagiliaji maji na kuimarisha eneo la hekta 2,105 za miundo mbinu ya
umwagiliaji maji katika bonde la Cheju, Kilombero na Chaani kwa Unguja, Mlemele
na Makwararani kwa Pemba. Maeneo hayo yanategemewa kuzalisha tani za mpunga
25,260 ifikapo 2018. Katika miaka mitano ijayo, minazi na
mikarafuu itapandwa zaidi pamoja na uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara hasa
manjano, hiliki, tangawizi, pilipili manga, kungu manga, kilimo cha alizeti na
kuanzisha mazao mapya ya biashara. Kadhalika, vituo vya huduma za udhibiti wa
maradhi vitaimarishwa, hasa vya mazao,
wadudu waharibifu pamoja na ukaguzi na karantini dhidi ya maradhi na wadudu
waharibifu wa mimea na mifugo ili kudhibiti maradhi ya mimea na mifugo hapa
Zanzibar.
Mheshimiwa
Spika,
Vile vile, Serikali itaendeleza utafiti
wa mbegu za mazao ya chakula, biashara, mboga na matunda na kuhakikisha kwamba
matumizi ya takwimu na matokeo ya utafiti huo, yanawafikia wakulima na
yanatumika katika kufanya uamuzi. Katika kipindi hiki, eneo la Kibonde mzungu,
litaandaliwa kwa kilimo cha mbegu za mpunga.
Kadhalika, Chuo cha Kilimo Kizimbani, kitaimarishwa ili kiongeze idadi
ya wataalamu wa kilimo na mifugo nchini kwa kukiunganisha na Chuo Kikuu cha
Taifa cha Zanzibar (SUZA), ili kiweze kutoa masomo ya shahada kwa kuwa Chuo
Kikuu Kishiriki. Vile vile, Serikali katika kipindi hiki itasimamia utekelezaji
wa Sheria ya Hifadhi ya Taifa ya chakula ili kujikinga na baa la njaa na
ukosefu wa chakula na lishe. Maghala ya kuhifadhia chakula matatu (3)
yatakamilishwa katika kipindi hiki na kuanza kutumika.
Kadhalika, Serikali itaihamasisha sekta
binafsi ijenge viwanda vya usarifu wa mazao,
ili kuongeza thamani na ubora wa mazao ya mboga na matunda, na kadhalika, ili
kukuza kipato cha wakulima na kurahisisha upatikanaji wa soko. Serikali
imetiliana saini Mkataba na Kampuni ya Mahindra-Mahindra ya India kwa ajili ya
ununuzi wa matrekta mapya katika kipindi hiki.
Taratibu za ununuzi wa matrekta hayo tayari yameanza. Vile vile, kiwanda cha matrekta cha Mbweni
kitatumika kwa ajili ya kuyaunganisha matrekta ya Mahendra ili baadae yauzwe
kwenye soko la nje yakisafirishwa kutokea Zanzibar.
MIFUGO
Mheshimiwa
Spika,
Sekta ya ufugaji inaendelea kuwa na
mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kutoa ajira kwa wananchi wengi wa Unguja
na Pemba. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, Awamu ya Saba, katika kipindi chake cha kwanza iliiendeleza sekta ya
ufugaji kwa kauli mbiu ya “Mapinduzi ya Ufugaji”, yaliyolenga kuwa na ufugaji
wenye tija na kuongeza ubora wa mazao ya mifugo. Sekta ya ufugaji inakabiliwa na changamoto ya
uhaba wa ardhi kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu na kupanuka kwa
shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo,
Serikali itaendelea kuhimiza na kuimarisha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na
nyama, ufugaji wa mbuzi pamoja na kuku wa nyama na mayai, ili kuongeza tija na
kipato cha wafugaji. Katika
kulifanikisha lengo hilo, Serikali itasimamia utekelezaji wa sera, sheria na
programu mbali mbali za elimu kwa wafugaji, ili kuwawezesha wafugaji wadogo
kutekeleza kanuni za ufugaji wa kisasa na kuongeza uzalishaji wa mazao ya
mifugo kwa lengo la kukidhi mahitaji ya viwango vya soko la ndani na nje.
Mheshimiwa
Spika,
Kadhalika, Serikali itaviimarisha vituo
vya utafiti na huduma za kinga na tiba za mifugo na kuwapa wafugaji huduma za
upandishaji wa ng’ombe kwa shindano, ili kupata mbegu bora pamoja na
kuhamasisha sekta binafsi kutoa huduma za afya na pembejeo za mifugo. Aidha, Serikali itawahamasisha wawekezaji wa
ndani na nje wawekeze katika sekta ya mifugo na viwanda vya usindikaji wa mazao
ya mifugo pamoja na kuongeza uwezo wa kitaalamu kwa wafanyakazi wa sekta ya
mifugo nchini.
UVUVI
NA MAZAO YA BAHARINI
Mheshimiwa
Spika,
Uvuvi na uzalishaji wa mazao ya
baharini ni miongoni mwa shughuli muhimu za kiuchumi zinazofanywa na wananchi
wengi wanaoishi katika maeneo ya karibu na bahari. Kwa kutambua umuhimu wa shughuli hizi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, katika kipindi chake cha
kwanza (2010 – 2015) ilichukua jitihada mbali mbali za kuimarisha sekta ya uvuvi
na mazao ya baharini kwa ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa
Spika,
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo,
Serikali itaendeleza juhudi katika kusimamia utekelezaji wa Sera na Sheria za
Uvuvi ili kuimarisha usimamizi wa rasilimali za bahari na uhifadhi wa mazingira
na kuendeleza jitihada za kuwahamasisha wavuvi wadogo katika kuanzisha vikundi
vya ushirika na kuwapatia mafunzo na mikopo nafuu ya zana za kisasa ili
kuongeza mapato yao.
Vile vile, Serikali itaandaa mpango na
mazingira ya kuvutia Sekta Binafsi kuwekeza katika uvuvi wa bahari kuu,
utengenezaji wa boti za uvuvi, ujenzi wa vyumba vya baridi (cold rooms) pamoja
na viwanda vya kusindika samaki. Aidha, wavuvi hasa vijana watahamasishwa na
kupatiwa mafunzo na zana za kisasa zitakazowawezesha kuvua katika kina kirefu
cha maji.
Serikali itanunua vihori 500 vya
kuchukulia mwani na kuvisambaza kwa wakulima wa mwani 3,000 Unguja na Pemba ili
kuongeza uzalishaji wa mwani. Aidha, itawahamasisha wafugaji wa samaki, chaza,
kaa, kamba na majongoo ili kuendeleza uzalishaji wa mazao hayo. Vile vile,
juhudi zitachukuwa katika kutafuta masoko kwa mazao ya baharini. Aidha,
tutasimamia Mpango Shirikishi wa Maeneo ya Hifadhi ya Bahari yakiwemo maeneo ya
Tumbatu, Chumbe – Bawe, Minai kwa Unguja na Kisiwa Panza, Kokota na Mwambe kwa
upande wa Pemba. Tutahakikisha kwamba
jamii inayozunguka maeneo hayo inanufaika na uhifadhi huo.
Kwa
kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tutaandaa Sera ya Uvuvi wa Bahari Kuu ili
kuwavutia wawekezaji wa ndani na wa nje wawekeze katika Sekta ya Uvuvi wa
bahari kuu, wajenge viwanda vya kusindika samaki, waanzishe Chuo cha Mafunzo ya
Uvuvi na wajenge Bandari ya Uvuvi. Tayari Kampuni ya Hairu ya Sri Lanka
imetiliana saini Makubaliano ya Awali ya kuanzisha uwekezaji katika uvuvi kwa
kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vile vile, Serikali imetiliana saini mkataba
na Shirika la Kimataifa la Kilimo na Chakula (FAO) kwa ajili ya kuanzisha Mradi
wa kuendeleza shughuli za ufugaji wa samaki, utakaogharimu Dola za Kimarekani
milioni 3.23. Mradi huu utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu na
utajumuisha ujenzi wa kituo cha kuzalisha vifaranga vya samaki, huko
Beit-el-Ras. Fedha za mradi huo
zitatolewa na Serikali ya Korea kupitia Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo
la Kimataifa la Korea ( KOICA).
ARDHI
Mheshimiwa
Spika,
Ardhi ni rasilimali muhimu katika nchi
ambapo kwa kuzingatia umuhimu wake, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tangu
Awamu ya Kwanza ilizingatia haja ya rasilimali hiyo kumilikiwa na
Serikali. Kwa kuzingatia udogo wa ardhi
tuliyonayo, Serikali imetilia mkazo umuhimu wa matumizi bora ya ardhi kwa
kuandaa Sera na Sheria za mipango ya matumizi yake. Katika miaka mitano ya
mwanzo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, ilipanga na
ilitekeleza mikakati mbali mbali iliyolenga katika kuimarisha matumizi bora ya
ardhi na kupunguza migogoro ya ardhi nchini.
Katika kipindi hiki cha pili cha miaka
mitano, Serikali itaendelea na juhudi zake za kuimarisha matumizi ya ardhi na
kutatua migogoro iliyobakia na kuimarisha huduma za Mahakama za Ardhi katika
Mikoa yote ya Unguja na Pemba. Tutaendelea kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu
wa kutambua na kufuata sheria mbali mbali za ardhi zinazohusiana na utambuzi,
upimaji na usajili wa ardhi. Aidha, Serikali, itaendeleza kazi ya upimaji wa
viwanja na utoaji wa hati kwa ajili ya matumizi mbali mbali ya kiuchumi na
kijamii, kwa kuzingatia mpango wa kitaifa wa Matumizi bora ya Ardhi.
Mheshimiwa
Spika,
Waheshimiwa Wajumbe,
mna jukumu la kushirikiana na viongozi wa Shehia zenu katika majimbo yenu,
Uongozi wa Wilaya, Mkoa na Serikali kuu, ili kwa pamoja tuhakikishe kuwa
Zanzibar inatekeleza mpango wa matumizi bora ya ardhi yanayozingatia uhifadhi
wa mazingira. Vile vile, tunafanya jitihada za kuiondoa migogoro ya ardhi
ambayo haina tija kwa maendeleo yetu.
Napenda nitoe indhari kuwa Serikali haitomvumilia kiongozi wa ngazi yoyote
ambaye atajijengea tamaa na akajiingiza katika migogoro ya ardhi au akashindwa
kutatua migogoro iliyopo katika dhamana yake. Si siri kwani wapo baadhi ya
viongozi waliojiingiza katika matatizo ya ardhi na kusababisha mzozo mkubwa
kwenye jamii. Migororo ya ardhi ni kadhia ambayo tunataka tuimalize katika
kipindi hiki cha miaka mitano ijayo. Kwa hivyo, nawatahadharisha viongozi
watakaopewa dhamana ya kushughulikia masuala ya ardhi wayazingatie maelezo
yangu haya.
MAZINGIRA
Mheshimiwa
Spika,
Kila mmoja wetu anafahamu umuhimu wa
mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho na uharibifu wa mazingira ni
tishio kwa maisha yetu. Katika miaka
mitano iliyopita, Serikali ilichukua juhudi mbali mbali za kuimarisha uhifadhi
wa mazingira. Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali italiangalia
upya, suala la uchimbaji mawe na mchanga na ukataji ovyo wa minazi. Serikali
itaandaa mbinu mpya katika kulishughulikia suala hilo. Nitahakikisha kuwa
juhudi za uhifadhi wa mazingira zinaendelea kupata ufanisi huku tukitambua kuwa
dunia imekabiliwa na changamoto mbali mbali zitokanazo na uharibifu wa
mazingira na mabadiliko ya tabia ya nchi. Changamoto hizo zimekuwa na athari
zaidi na katika nchi za Visiwa.
Serikali itaendelea kuhamasisha
upandaji wa miti, ushajiishaji wa matumizi ya aina nyengine ya nishati na
itatilia mkazo zaidi katika kufanya tathmini ya athari za mazingira katika
miradi ya uwekezaji. Tutaendelea kuiridhia mikataba iliyowekwa na Jumuiya za Kimataifa
yenye lengo la kuhifadhi mazingira. Matumaini yangu ni kuwa watendaji wa idara
na taasisi zinazoshughulikia masuala ya mazingira watawajibika ipasavyo ili
tuweze kuyafikia malengo haya tuliyojiwekea.
VYAMA
VYA USHIRIKA NA SACCOS
Mheshimiwa
Spika,
Serikali katika kipindi cha miaka
mitano iliyopita, iliwahamasisha wananchi kuanzisha vyama vya Ushirika na
SACCOS kwa lengo la kuwawezesha kukabiliana na tatizo la ajira na kupambana na
umasikini wa kipato. Katika kipindi hicho, Serikali iliviendeleza vikundi vya
ushirika kwa kuvipatia mafunzo, mikopo na kuvifanyia ukaguzi. Aidha, katika kipindi hicho Serikali
ilianzisha Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambao ilitoa mikopo 286 yenye
thamani ya TZS milioni 436.2. Mikopo hiyo iliwanufaisha wananchi wapatao
8,976.
Mheshimiwa
Spika,
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo,
Serikali itayaendeleza mafanikio yaliyopatikana pamoja na kuendelea kuimarisha
Mfuko wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi ili kuongeza uwezo wake wa kutoa
mikopo kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo. Sambamba na juhudi hizo,
Serikali itakiimarisha kituo cha kulelea wajasiriamali kilichoko Mbweni pamoja
na kuendelea kutoa mafunzo mbali mbali kwa lengo la kuwajengea wananchi uwezo
wa kujiajiri na kuondokana na umasikini.
Aidha, Serikali itaanzisha vituo 10 vya
huduma za biashar; kimoja kila Wilaya ili kuongeza tija katika shughuli za
wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo pamoja na kutoa mikopo 5,000 yenye
thamani ya TZS. bilioni 2.5. Mikopo hii itawanufaisha jumla ya wananchi 50,000
kutoka kwenye makundi mbali mbali ya wananchi hususan wanawake, vijana na watu
wenye walemavu.
KAZI,
AJIRA NA UTUMISHI WA UMMA
Mheshimiwa
Spika,
Suala la ajira bado ni changamoto
katika nchi yetu kama ilivyo katika Mataifa mengine. Tuna matumaini makubwa ya kupata mafanikio
katika ongezeko la nafasi za kazi katika
kipindi kijacho kutokana na mikakati tuliyojipangia. Miaka mitano iliyopita,
zilipatikana nafasi za ajira 5,370 katika taasisi mbali mbali za serikali na
nafasi 25,006 katika sekta binafsi zikijumuisha ajira za nje ya nchi.
Tutahakikisha jitihada za Serikali za
kutekeleza mageuzi ya uchumi zinafanikiwa katika sekta ya utalii na viwanda kwa
kuwashajiisha wawekezaji. Tutahakikisha
kwamba sekta binafsi inaimarishwa na kuwa
chanzo kikuu cha ajira. Vyama vya ushirika navyo vitaunganishwa ili
viwawezesha wananchi kubadili maisha yao ili wajiendeleze kiuchumi. SACCOS na Asasi ndogo za fedha zitaimarishwa
na kupatiwa mafunzo ya kitaalamu, uongozi na kuwaongezea mitaji, ili ziweze
kutekeleza shughuli zake kwa ufanisi kwa lengo la kuongeza ajira.
Mheshimiwa
Spika,
Serikali itaendelea na jitihada zake za
kuimarisha maslahi ya wafanyakazi pamoja na mazingira ya kufanyia kazi.
Tutaendelea kuimarisha miundo ya utumishi, ili wafanyakazi waendelee kufaidika
na elimu, uwezo na uzoefu walioupata wakiwa kazini pamoja na viwango vya elimu
walivyonavyo. Hata hivyo, nataka nikumbushe kuwa, wafanyakazi sote tufahamu
kuwa mshahara ni matunda na tunzo mtu anayopata kutokana na juhudi aliyoifanya
katika uzalishaji. Kuna baadhi ya watu wamejenga tabia ya kudai mishahara
mikubwa na kuilaumu Serikali kuwa haipandishi mishahara bila ya wao kuwa na ari
na dhamira ya kweli ya kujitahidi kufanya kazi na kuzalisha.
Natumai kuwa watu wa aina hiyo
wataiacha tabia hiyo ambayo haina manufaa kwa maendeleo yetu. Kwa pamoja tunawajibika kulitekeleza kwa
vitendo agizo langu nililolitoa mwaka 2011, mara tu baada ya kuingia madarakani
kuwa “tubadilike na tusifanye kazi kwa mazoea”.
Tulijitahidi kubadilika na kuyaondoa mazoea. Lakini ni ukweli usiopingika matatizo bado
yapo, viwango vya utendaji na nidhamu kazini bado havijaongezeka sana. Ni
jukumu letu tufanye kazi kwa bidii na tuipende kazi. Kwani wapo baadhi ya wafanyakazi ambao hawapendi
kufanyakazi (kwa vitendo vyao), na wengine hawataki kufanyakazi, lakini wao
ndio wa mwanzo wanaotaka mishahara mikubwa, posho nzuri, safari za kila wakati
na kuhudhuria kwenye semina na mikutano kila mara.
Wapo baadhi ya wafanyakazi kwenye
taasisi muhimu zinazotoa huduma kwa wananchi, ambao hawajali kazi zao na
wanakwepa wajibu wao. Upo ushahidi
kutoka kwa baadhi ya wananchi kwamba wanapokwenda kutaka huduma wanadharauliwa,
wanapuuzwa, wananyanyaswa na wengine hutakiwa watoe kitu chochote. Baadhi ya wafanyakazi wenye tabia hizi
walichukuliwa hatua za kinidhamu, lakini bado hawajajirekebisha. Wafanyakazi wa namna hii huwavunja moyo
wananchi na hupelekea wananchi waichukie Serikali yao bila ya sababu za msingi.
Zaidi ya hayo, wapo baadhi ya watumishi
wenye tabia ya kutoroka kazini, kuchelewa na hawazijali kanuni ziliopo za
utumishi wa umma. Wao hujifanya wababe
mbele ya viongozi wao. Wafanyakazi wenye
sifa mbaya nilizozielezea katika kipindi hiki tutawachukulia hatua
watakapobainika na kama hapana budi tutawafukuza kazini. Hatuwezi kuwa na wafanyakazi waliokuwa hawana
nidhamu. Sasa basi, imetosha. Waliopewa dhamana ya kuziongoza Idara mbali
mbali za Serikali watapaswa watekeleze wajibu kwa kuwasimamia wafanyakazi walio
chini yao. Pindi kama hawatawawajibisha
wafanyakazi wao, basi watawajibishwa wao.
Lengo letu liwe kutoa huduma kwa wananchi, kwani sote tunawajibika kwao;
kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.
Mheshimiwa
Spika,
Nataka niwahakikishie wananchi kuwa
nitatekeleza ahadi nilizozitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015,
za kuimarisha maslahi ya wafanyakazi katika sekta mbali mbali ukiwemo utoaji wa
kima cha chini cha mshahara cha TZS. 300,000 kwa mwezi ndani ya kipindi cha
mwaka mmoja baada ya kuingia madarakani.
Kadhalika, ahadi yangu kwa Idara Maalum za SMZ ya maslahi yao yalingane
na wenzao wa SMT ipo pale pale. Tumuombe
Mwenyezi Mungu atupe uwezo wa kukusanya mapato vizuri, ili Serikali ipate uwezo
wa kuzitekeleza ahadi hizo.
Serikali itaimarisha zaidi huduma za
Hifadhi ya Jamii kwa wanachama wake kwa kubuni utoaji wa mafao mapya na
kuongeza kiwango cha malipo ya kiinua mgongo na pensheni. Madeni ya viinua mgongo vya wafanyakazi
waliostaafu tutayalipa, tunawaomba wastaafu wawe na subira. Sina shaka
Mheshimiwa Spika, kwamba juhudi hizi za kuimarisha utawala bora zinaungwa mkono
na zitapata baraka zote katika Baraza lako.
MIUNDOMBINU
Mheshimiwa
Spika,
Miundombinu ya kiuchumi ikiwemo
barabara, bandari na viwanja vya ndege ina mchango muhimu katika kuongeza kasi
ya kukua kwa uchumi wa nchi na kuimarisha huduma za jamii katika shughuli zao
za kila siku. Katika kipindi
kilichopita, jumla ya barabara zenye urefu wa kilomita 124.7 kwa Unguja
zilijengwa kwa viwango mbali mbali, na kilomita 203.4 za barabara zimejengwa
huko Pemba.
Kwa lengo la kuimarisha zaidi miundombinu
ya barabara katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itaendeleza kazi ya
utunzaji na matengenezo ya barabara zilizokwishajengwa na kufanya marekebisho
katika maeneo yanayotuama maji ya mvua na kuathiri ubora wa barabara hizo.
Kadhalika, tutakamilisha ujenzi wa barabara ya Jendele – Cheju-Kaebona (km
11.7) na barabara ya Koani hadi Jumbi (km 6.3) kwa kiwango cha lami kwa Unguja
na barabara ya Ole hadi Kengeja (km 35), Makanyageni hadi Kangani (km 6.5),
Finya hadi Kicha (km 8.8) na barabara kutoka Mgagadu hadi Kiwani (km 7.6) kwa
kiwango cha lami kwa upande wa Pemba.
Kadhalika, Serikali itajenga jumla ya
kilomita 160.8 za barabara kwa kiwango cha lami kwa Unguja katika maeneo mbali
mbali ya Mikoa yote na jumla ya kilomita 51.1 kwa kiwango cha lami huko Pemba
kwa maeneo yote ya Mikoa ya Pemba. Barabara
zote hizi zimefafanuliwa vizuri kwenye Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu na
mipango yake ya ujenzi tayari imepangwa. Kazi nyengine zitakazoshughulikiwa na
Serikali ni kuendeleza kazi ya uwekaji wa taa za kuongozea magari kwa kuweka
taa katika sehemu sita, ili kupunguza msongamano katika baadhi ya maeneo ya
miji hasa katika mji wa Unguja, Wete na Chake chake. Vile vile, karakana kuu ya Serikali
itaimarishwa kwa mashirikiano na sekta binafsi kwa lengo la kuongeza ufanisi na
utoaji wa huduma bora za kiufundi kwa taasisi mbali mbali za Serikali na watu
binafsi.
Mheshimiwa
Spika,
Kwa lengo la kuiendeleza sekta ya
usafiri wa anga katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itakamilisha
ujenzi wa jengo jipya la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha
Abeid Amani Karume (AAKIA), ili kuongeza idadi ya abiria wanaotumia kiwanja
hicho pamoja na kiwango cha mizigo ili kuongeza mapato ya Serikali. Kiwanja cha
ndege cha Pemba nacho kitapanuliwa ili ziweze kutua ndege kubwa za aina ya
Boeing 737, jengo la abiria litajengwa upya na miundombinu na huduma za abiria,
ndege na mizigo katika Kiwanja cha Ndege cha Pemba itaimarishwa. Vile vile, huduma za umeme zitaimarishwa na
kukamilisha kazi ya ujenzi wa uzio wa kiwanja hicho. Serikali, vile vile itaendelea kuwapatia
mafunzo na vifaa vya kisasa wafanyakazi wa Viwanja vya Ndege vya Unguja na
Pemba pamoja na kuimarisha huduma za zimamoto na usalama wa viwanja vya ndege.
Katika nchi za Visiwa kama Zanzibar,
usafiri wa baharini ni shughuli muhimu; jambo linalosababisha haja ya kuwepo
kwa bandari za kisasa ambazo huwa ni milango mikuu ya biashara na chachu ya
ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi kwa jumla. Katika kipindi changu cha kwanza, jitihada za
kuziimarisha bandari zetu na shughuli za usafiri wa baharini zilichukuliwa na
kuleta mafanikio makubwa.
Mheshimiwa
Spika,
Kwa lengo la kuimarisha bandari, katika
kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itatekeleza mradi wa ujenzi wa bandari
mpya ya kisasa ya kuhudumia mizigo katika eneo la Mpigaduri itakayoanza
kujengwa baadae mwaka huu kwa mkopo kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China. Vile vile, bandari ya Malindi itaendelezwa
kwa kuongeza vifaa vya huduma kwa abiria pamoja na mizigo. Bandari ya Mkoani
Pemba itaendelezwa kwa kuipatia vifaa vya kisasa vya kuhudumia abiria na
mizigo. Aidha, bandari ya Wete nayo
inatarajiwa kujengwa kwa juhudi za sekta binafsi, ambapo muwekezaji amejitokeza
na yupo tayari kuifanya kazi hiyo.
Kadhalika, Gati ya Mkokotoni nayo itajengwa kwa kukamilisha kazi ya
ujenzi wa jeti kwa ajili ya huduma za usafiri wa wananchi hasa wa Tumbatu na
usafirishaji wa mizigo kwa majahazi.
Shirika la Meli na Uwakala, litafanyiwa
mabadiliko makubwa ili liweze kujiendesha kibiashara na kununua meli nyengine
mpya ya abiria ndogo na moja ya mafuta.
Aidha, kuhusu kuziimarisha huduma za usafiri wa baharini, Serikali
itahakikisha kuwa inaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria na Kanuni za
usafiri wa baharini ili kupunguza ajali za vyombo vya baharini kwa kuimarisha
utendaji wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini (ZMA).
NISHATI
Mheshimiwa
Spika,
Upatikanaji wa nishati ya uhakika ni
muhimu katika kuimarisha ukuaji wa uchumi
na ustawi wa maendeleo ya wananchi. Mabadiliko na mafanikio makubwa
tumeyafikia nchini katika kuimarisha sekta ya nishati katika kipindi cha miaka
mitano iliyopita mijini na vijijini, Unguja na Pemba. Visiwa vyote viwili sasa vina nishati ya
umeme wa uhakika. Umeme tayari
umefikishwa kwenye vijiji 129 na kwenye visiwa vidogo vidogo kadhaa.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo,
Serikali itaendelea na juhudi za kuufikisha umeme katika vijiji na visiwa
vidogo vidogo, vilivyobakia ikiwemo Kisiwa cha Fundo ambapo huduma hizi
zinatarajiwa kupatikana katika mwaka wa fedha 2016/2017. Juhudi za kutafuta
umeme wa nishati mbadala zimefikia hatua kubwa kwa kushirikiana na washirika wa
maendeleo ambapo utafiti wa kutumia upepo unaendelea. Aidha, Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO)
litafanyiwa mabadiliko, ili liweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi na
kujiendesha kibiashara.
UCHIMBAJI
WA MAFUTA NA GESI
Mheshimiwa
Spika,
Natanguliza shukurani zangu kwa
waliokuwa Wajumbe wa Baraza la Nane la Wawakilishi kwa mijadala ya kina
waliyoiendesha juu ya suala zima la uchimbaji wa mafuta na gesi. Juhudi zao zimetuwezesha kuifikia hatua hii
nzuri. Rasimu ya mswada wa sheria ya mafuta na gesi hivi sasa ipo katika hatua
nzuri na matumaini yangu ni kuwa baada ya muda si mrefu italetwa katika Baraza
hili tukufu la Wawakilishi wa Zanzibar kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa.
Kwa mara nyengine tena, napenda
nimpongeze kwa dhati, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kuhakikisha kwamba, kabla
ya kuondoka kwake madarakani suala la Zanzibar kuchimba mafuta yake wenyewe
linapatiwa ufumbuzi. Tulishirikiana kwa dhati katika kulipatia ufumbuzi suala
hili. Hivi sasa, Zanzibar ina uwezo wa
kisheria wa kuchimba mafuta yake kwa mujibu wa Sheria Namba 21 ya mwaka 2015
iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sina shaka, Baraza
hili la Tisa litasimama imara katika kuendeleza pale tulipofika katika kipindi
kilichopita na litaharakisha katika utungaji wa sheria tunazozihitaji ili
tuweze kuyachimba mafuta na gesi na kufaidika na nishati hizi muhimu.
HUDUMA
ZA JAMII
Mheshimiwa
Spika,
Uimarishaji wa huduma za jamii ikiwemo
elimu, afya, huduma za maji safi na salama ni miongoni mwa majukumu muhimu ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika awamu zake zote saba.
ELIMU
Mheshimiwa
Spika,
Katika kipindi cha miaka mitano
iliyopita, Serikali iliizingatia huduma ya elimu kuwa ni haki ya msingi kwa
kila mwananchi na nyenzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita,
Serikali ilichukua hatua za kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa kuanzia ngazi
ya elimu ya maandalizi, msingi, sekondari, elimu ya juu na elimu inayotolewa katika
vituo vya mafunzo ya amali, vyuo vya
ualimu na Chuo Kikuu cha SUZA.
Mheshimiwa
Spika,
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo,
Serikali itayaendeleza mafanikio hayo katika sekta ya elimu pamoja na kuchukua
hatua za kuimarisha elimu katika ngazi mbali mbali. Kuhusu Elimu ya Maandalizi,
Serikali itasimamia utekelezaji wa Sera ya Makuzi na Malezi ya Mtoto na
itaanzisha vituo 150 vya Tucheze Tujifunze katika Wilaya nne za Unguja na
Pemba.
Kwa upande wa Elimu ya Msingi, Serikali
itaongeza kiwango halisi cha uwandikishaji hadi kufikia asilimia 100 mwaka
2020, itajenga skuli mpya 10 za ghorofa
katika maeneo yenye upungufu na msongamano mkubwa wa wanafunzi. Vile vile, Serikali itakamilisha ujenzi wa
madarasa yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi. Lengo la kutoa elimu bila ya
malipo katika elimu ya msingi kwa kutowachangisha wazazi michango yoyote,
litaendelezwa kutekelezwa. Kadhalika,
Serikali itaendelea kulipia gharama za mitihani ya kidatu cha tatu na mitihani
ya Taifa kwa watahiniwa wa Kidatu cha Nne na cha Sita. Hatua hii ina lengo la kuwaondolea wazazi
mzigo wa kuchangia huduma za elimu ya watoto wao.
Mheshimiwa Spika,
Serikali
itajenga vituo vipya vya Mafunzo ya Amali huko Makunduchi kwa Unguja na Daya
Mtambwe huko Pemba. Aidha, mafunzo ya ualimu yataimarishwa katika ngazi
mbali mbali. Katika kipindi hiki ujenzi
wa dakhalia katika Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) utaanza na ujenzi wa Chuo Kikuu
kipya katika eneo la Dole utaanza kwa kushirikiana na Serikali ya Saudi
Arabia. Vile vile, nafasi za masomo ya
elimu ya juu zitaongezwa kwa kuuimarisha Mfuko wa Bodi ya Mikopo, ili lengo la
kuwanufaisha wanafunzi 22,404 ifikapo
mwaka 2020 liweze kufanikiwa.
Katika
kipindi kijacho, Serikali itaongeza idadi ya watu wanaojua kusoma, kuandika na
kuhesabu pamoja na kuimarisha Elimu Mjumuisho kwa ajili ya watoto wenye
mahitaji maalumu. Vile vile, Serikali itaimarisha na itaendeleza michezo na
utamaduni maskulini ambapo kipindi cha miaka mitano ijayo somo la michezo
litaanzishwa katika skuli sita za sekondari zilizoteuliwa. Skuli nne Unguja na mbili huko Pemba.
AFYA
Mheshimiwa
Spika,
Sekta ya afya ni muhimu katika
kuimarisha afya za wananchi wetu ili waweze kushiriki kikamilifu katika
shughuli zao za kila siku na kutoa mchango wao katika kuleta maendeleo
nchini. Katika kipindi cha miaka mitano
iliyopita, Serikali ya Awamu ya Saba ilichukua hatua mbali mbali katika
kuziimarisha huduma za afya ambapo huduma hizi zinapatikana si zaidi ya
kilomita tano ya makaazi ya kila mwananchi.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo,
Serikali itaongeza jitihada za kuziimarisha huduma za afya kwa kuendelea
kuishirikisha sekta binafsi. Azma yetu
ya kuifanya hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa ya Rufaa itaendelezwa kwa
kuzikamilisha zile huduma muhimu ambazo bado zinashughulikiwa. Hivi sasa Serikali inakamilisha utaratibu wa
matibabu ya saratani na utibabu wa maradhi ya figo. Vile vile, huduma za uchunguzi wa maradhi
zitaimarishwa kwa ununuzi wa vifaa vya kisasa kama “Magnetic Resonance Imaging
(MRI)”, mashine ya uchunguzi wa “DNA” na vyengine. Vile vile, idadi ya madaktari na mabingwa wa
fani mbali mbali itaongezwa.
Kadhalika, Serikali itatekeleza mpango
wake wa kujenga Hospitali ya kisasa ya Rufaa katika eneo la Binguni
Unguja. Ujenzi wa Hospitali ya Abdalla
Mzee unaoendelea hivi sasa unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba, 2016. Hospitali ya Wete Pemba nayo itaimarishwa ili
hospitali zote mbili zifikie daraja na kiwango cha Hospitali za Mkoa. Aidha, Hospitali ya vijiji ya Makunduchi na
Kivunge kwa Unguja zimefika hatua kubwa ya kuwa
Hospitali za Wilaya na kazi bado inaendelea kufanywa. Kazi kama hiyo inafanyika kwa hospitali ya
Vitongoji na Micheweni.
Mheshimiwa
Spika,
Vile vile, Serikali itaendeleza
jitihada za kuimarisha Huduma ya Afya ya Mama na Mtoto kwa kuendeleza ujenzi wa
majengo mapya ya wodi ya wazazi na wodi ya watoto unaoendelea sasa katika
Hospitali Kuu ya Mnazi mmoja. Jumla ya vituo 19 vya afya ya msingi Unguja na
Pemba vitafanyiwa matengenezo makubwa na kuvipatia vifaa vya kisasa ili
kupunguza kiwango cha vifo vya mama na mtoto.
Mapambano dhidi ya maradhi ya Malaria, UKIMWI, kifua kikuu na ukoma na
maradhi mengine ya kuambukiza na yasiyokuwa ya kuambukiza yanaendelezwa kwa
mafanikio. Kiwango cha maradhi ya
malaria bado kipo chini ya asilimia moja.
Utoaji wa elimu ya afya kwa wananchi
unaendelezwa vizuri, ili kupunguza ongezeko la maradhi ya saratani,
kisukari na shinikizo la damu.
Serikali vile vile, itakiimarisha Chuo
cha Taaluma za Sayansi ya Afya kwa kukiunganisha na Chuo Kikuu cha Taifa cha
Zanzibar, ili kiweze kutoa wataalamu wenye elimu ya kiwango cha shahada; katika fani mbali mbali. Kadhalika, madaktari na madaktari mabingwa wa
fani mbali mbali watapatiwa mafunzo ili tuweze kujitosheleza na mahitaji
yaliyopo. Vile vile, idadi ya madaktari
wanaofundishwa katika kitivo cha udaktari katika Chuo Kikuu cha SUZA na
vyengine itaongezwa; ili lengo la Serikali lililowekwa kwenye Mpango wa Afya wa
mwanzo hapo 1965 wa daktari mmoja ahudumie watu 6,000 liweze kufikiwa. Hivi sasa daktari mmoja anahudumia watu 8,885
(1:8885).
Vile vile, tafiti mbali mbali katika
maeneo ya Afya ya mama na mtoto, maradhi ya kuambukiza na yasiyoambukiza
zitaendelezwa pamoja na mifumo ya utoaji huduma za afya. Huduma za matibabu ya wagonjwa walioathirika
na dawa za kulevya na afya ya akili zitaimarishwa na kujenga kituo maalumu kwa
waathirika wa dawa za kulevya. Serikali itaongeza bidii katika kukabiliana na
matumizi ya dawa za kulevya ili kuwanusuru
vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa.
Aidha, Serikali itaimarisha upatikanaji, ugawaji, usambazaji na udhibiti
wa dawa, vifaa vya utibabu, dawa za uchunguzi wa maradhi na “reagents” zenye
ubora. Vile vile, Serikali itaandaa
Sheria ya Uanzishaji wa Mfuko wa Bima ya Afya na kusimamia utekelezaji wa mfuko
huo. Kadhalika, Serikali itaandaa utaratibu
mzuri wa namna wananchi watakavyochangia huduma za afya wanapoelezwa kufanya
hivyo. Hivi sasa hakuna mpango
unaofahamika katika jambo hili.
MAJI
Mheshimiwa
Spika,
Mafanikio makubwa yamepatikana katika
kuimarisha huduma za maji safi na salama kupitia miradi na programu mbali mbali
za maji mijini na vijijini. Katika
kipindi kilichopita hadi mwishoni mwa mwaka 2015 hali ya upatikanaji wa maji
safi na salama imefikia asilimia 87 kwa mijini na asilimia 70 kwa vijijini.
katika kipindi cha miaka mitano ijayo,
Serikali itaendelea kuimarisha usambazaji wa huduma ya maji safi na salama kwa
wananchi kutoka asilimia 87 mwaka 2015 hadi asilimia 97 mwaka 2020 kwa mijini
na kutoka asilimia 70 mwaka 2015 hadi asilimia 85 kwa vijijini ifikapo mwaka
2020. Vile vile, itaendeleza jitihada za
kuimarisha miundombinu ya maji ili kupunguza upotevu wa maji. Vyanzo vya maji vitahifadhiwa, vitatunzwa na
vitalindwa pamoja na maeneo ya kuhifadhia maji. Vile vile, wananchi
watahamasishwa juu ya umuhimu wa uhifadhi, utumiaji na uchangiaji wa huduma ya
maji safi na salama. Utafiti wa
matumizi ya nishati ya jua katika visima na vyanzo vya maji utafanywa, kwa
lengo la kupatikana huduma hizi kwa ufanisi.
VYOMBO VYA HABARI
Mheshimiwa Spika,
Vyombo
vya habari vina umuhimu mkubwa katika kuhamasisha shughuli za maendeleo ya
kiuchumi, kijamii na kisiasa pamoja kupanua uhuru na haki ya wananchi ya kupata
taarifa. Katika kipindi cha miaka 5 ijayo, Serikali itahakikisha kwamba uhuru
wa vyombo vya habari unaendelea kuimarishwa na vyombo hivyo vinatimiza wajibu
wake kwa weledi na kuzingatia maadili ya kazi zao. Serikali itaimarisha matumizi ya TEHAMA na
kuendeleza mageuzi ya sekta ya Habari, ili kuongeza ufanisi na weledi.
Vile
vile, Shirika la Habari la Zanzibar (ZBC) litaimarishwa kwa kulipatia mitambo,
vifaa vya kisasa ili kuukamilisha utaratibu wa matumizi ya “Digital” kwa TV na
Redio. Aidha, mafunzo ya wafanyakazi
wake katika kada mbali mbali yatatolewa ndani na nje ya nchi. Tutaendelea
kuwashajihisha wawekezaji ili wawekeze katika vyombo vya habari binafsi.
Mheshimiwa Spika,
Kuhusu
Kiwanda cha Upigaji Chapa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, Serikali
itakiimarisha na kukiongezea vifaa na wataalamu. Vile vile, Serikali itakiimarisha Chuo cha
Uandishi wa Habari ili kiwe chachu ya kuendeleza tasnia ya habari na kuendeleza
vipaji vya uandishi wa habari. Hata
hivyo, tasnia ya habari imekabiliwa na changamoto ya matumizi mabaya ya intaneti
na mitandao ya kijamii. Matarajio yangu
ni kuwa wakati utakapofika mtahakikisha mnajadili na mnairidhia Sheria ya Makosa ya Matumizi ya
Mitandao ya Mwaka 2015 iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ili sheria hii iweze kutumika hapa Zanzibar. Lengo letu tuwe na matumizi ya mitandao
yanayozingatia sheria, heshima, faragha na haki za wananchi pamoja na utunzaji
wa siri za Serikali.
UTAMADUNI NA MICHEZO
Mheshimiwa
Spika,
Kwa kutambua kuwa utamaduni ni nyenzo
muhimu katika kulinda na kudumisha mapenzi, umoja, mila, desturi na silka njema
katika jamii, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi ilichukua juhudi mbali
mbali za kuendeleza na kulinda utamaduni wetu.
Katika kipindi hiki cha pili, Serikali
itaendelea na juhudi za kuulinda, kuudumisha na kuutangaza utamaduni wa
Mzanzibari kwa kuendelea kuandaa
matamasha ya utamaduni. Aidha,
tutawaelimisha wananchi hasa vijana juu ya matumizi bora ya mitandao pamoja na
kufanya ukaguzi wa kazi za sanaa mbali mbali. Tutaendelea na jitihada za
kuimarisha lugha ya Kiswahili na kuzifanya lahaja za Zanzibar kuwa ni chimbuko
la Kiswahili fasaha. Vile vile, tutaendelea kuimarisha tasnia ya sanaa kwa
kuongeza kasi ya kutafuta na kukuza vipaji vya wasanii pamoja na kuimarisha
maslahi yao kwa kuimarisha mfumo uliopo wa matumizi ya hakimiliki.
Mheshimiwa
Spika,
Vile vile, tutazidisha juhudi zetu
katika kuyaendeleza mafanikio tuliyoyapata katika sekta ya michezo kwa
kuyaimarisha mashindano ya riadha ya
Wilaya na kuliimarisha Bonanza la michezo la vikundi vya
mazoezi. Jitihada zetu za kuimarisha michezo katika maskuli, bila ya shaka
zitafanikiwa. Kadhalika, tutakamilisha
matengenezo ya Kiwanja cha Mao Tse Tung na kujenga viwanja vya michezo kwa kila
Wilaya. Tutahamasisha ushiriki wa michezo na ufanyaji wa mazoezi ya viungo kama
ni hatua muhimu ya kuimarisha afya za wananchi. Tutaendeleza michezo ya asili
ya Zanzibar, ikiwemo mashindano ya resi za ngalawa, bao, karata, mchezo wa
ng’ombe na mengineyo.
Watu wenye ulemavu nao tutawahamasisha
kwa kuwapatia vifaa pamoja na vyama vya michezo vinavyohusika, ili waweze
kushiriki kikamilifu katika kuendeleza michezo. Wasanii wataendelea kusaidiwa,
wataendelezwa na wale walioijengea nchi yetu heshima katika ulimwengu wa
utamaduni, wataenziwa na watapewa heshima yao.
KUYAENDELEZA
MAKUNDI MAALUM
VIJANA
Mheshimiwa
Spika,
Serikali inatambua umuhimu wa kundi la
Vijana kuwa ni rasilimali na nguvukazi ya Taifa. Vijana walioandaliwa vyema na
kujipanga vizuri wanao mchango mkubwa katika kukuza uchumi na maendeleo ya
jamii. Changamoto kubwa inayowakabili vijana
mijini na vijijini ni ukosefu wa ajira, kukosa ujuzi na maarifa ya kisasa
pamoja na mitaji, hivyo kushindwa kujiendeleza na kutekeleza wajibu wao wa
kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa kisasa.
Serikali ilichukua hatua mbali mbali za
kuwaendeleza vijana katika kipindi kilichopita.
Kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili vijana,
Serikali katika kipindi kijacho cha miaka mitano, itachukua hatua za
kuuimarisha mfuko maalum wa vijana, ili vijana wengi zaidi waweze kunufaika na
mfuko huo na kwenye kazi mbali mbali pamoja na kujiajiri katika kilimo cha
kisasa na kuanzisha "green house'
moja kwa kila Wilaya. Aidha, Serikali itawahamasisha vijana 5,000 waliomaliza
vyuo Vikuu kuanzisha vikundi vya uzalishajimali na utoaji wa huduma na kuwapatia
mafunzo na mikopo ili waweze kujiajiri.
Kadhalika, Baraza la Vijana litaendelezwa, ili kuongeza ushiriki wa
vijana katika ngazi mbali mbali za uamuzi.
Aidha, jitihada za Serikali za kuongeza ajira kwa kushirikiana na sekta
binafsi, zitaendelezwa.
WANAWAKE
Mheshimiwa
Spika,
Ni dhahiri kuwa wanawake wana uwezo
mkubwa katika kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Serikali katika kipindi kilichopita, iliwaendeleza wanawake kwa lengo la kuwapa
uwezo wa kutumia fursa zilizopo katika kujiendeleza kiuchumi, kijamii na
kisiasa.
Kwa lengo la kuwawezesha wanawake
kiuchumi, kijamii na kisiasa katika miaka mitano ijayo, Serikali itayaendeleza
yale mafanikio yote yaliyopatikana.
Vile vile, itaendelea kusimamia upatikanaji wa haki za wanawake na
kupiga vita mila na desturi zinazowabagua au kuwadhalilisha na kusimamia
utekelezaji wa sheria na mikataba yote ya Kimataifa inayohusu ustawi wa
wanawake. Aidha, Serikali itaanzisha jumla ya vikundi 500 vya wanawake na
kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali pamoja na mikopo ili waweze kujiajiri
wenyewe. Kadhalika, kituo kiliopo Kibokwa cha kuwafundisha wanawake kutengeneza
vifaa vya umeme wa jua kitaendelea kuimarishwa ili kiwafundishe wanawake wengi
zaidi. Vile vile, kampeni ya kupinga
udhalilishaji wanawake na watoto itaendelezwa kwa kasi, ili hatimae matatizo
haya yasiwepo kwenye jamii zetu.
WAZEE
Wazee ni hazina na chem chem ya busara
na hekima katika jamii kutokana na uzoefu walionao katika maisha. Serikali
inaheshimu mchango wa wazee katika maendeleo yetu pamoja na malezi na maadili
mema wanayoyatoa kwenye jamii yetu.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo,
Serikali itaongeza juhudi katika kuziimarisha huduma za kijamii na mahitaji
muhimu wanayopewa wazee wanaotunzwa katika nyumba za wazee za Unguja na Pemba.
Kadhalika, Serikali itaanza kutekeleza Mpango
wa kuwapatia Pencheni maalum wazee wote waliofikia umri wa miaka 70 bila
ya kujali historia ya kazi walizokuwa wakizifanya. Vile vile, Serikali itaandaa utaratibu maalum
wa kuwapatia wazee huduma za matibabu bure.
WATOTO
Mheshimiwa
Spika,
Watoto wana haki ya kulindwa na kuishi
vizuri bila ya matatizo na ni sehemu muhimu ya wanajamii. Watoto wetu wanayo haki ya kuishi, kutoa
mawazo yao, kupata lishe bora, kupata haki ya elimu na kutobaguliwa kwa namna
yoyote. Serikali katika miaka mitano
iliyopita ilizingatia umuhimu huo na ilitekeleza mipango ya kuwapatia watoto
haki zao za msingi.
Ili kuhakikisha haki za watoto
zinaendelea kulindwa, katika kipindi kijacho Serikali itayaendeleza yale
mafanikio yote yaliyopatikana. Vile vile, itaziimarisha Mahkama za watoto na
kusimamia uanzishwaji na uendeshaji wa
mabaraza ya watoto na kamati za wazazi katika Shehia, Wilaya na Mikoa yote ya
Zanzibar, ili kupinga vitendo vya udhalilishaji dhidi ya watoto. Kadhalika, jitihada zetu za kupiga vita ajira
za watoto zitaendelezwa pamoja na kusimamia utekelezaji wa sheria na mikataba
ya Kimataifa inayohusu haki, usawa na hifadhi ya mtoto.
WATU
WENYE ULEMAVU
Mheshimiwa
Spika,
Watu wenye ulemavu wana haki kwa mujibu
wa Katiba ya Zanzibar ya 1984, kutambuliwa utu wao, kuendelezwa, kuheshimiwa,
kushirikishwa na kulindwa dhidi ya vitendo vinavyowabagua. Katika kipindi hiki,
tutaendeleza kusimamia utekelezaji wa mipango na programu mbali mbali zenye lengo la kuwaendeleza watu wenye
ulemavu. Mfuko wa Watu Wenye Ulemavu
tuliouanzisha kipindi kilichopita
utaimarishwa na tutahakikisha kuwa
huduma muhimu na mahitaji ya nyenzo zote pamoja na dawa zinapatikana
bila ya malipo. Aidha, tutaendeleza na utoaji wa mafunzo na elimu kwa wazazi,
walezi na walimu juu ya namna ya kuwakuza watoto wenye ulemavu na
tutayazingatia makaazi yao wanayoishi.
DEMOKRASIA
NA UTAWALA BORA
Mheshimiwa
Spika,
Demokrasia na utawala bora ni nguzo na
nyenzo muhimu katika ujenzi wa jamii yenye umoja, mshikamano, uadilifu na
uwajibikaji. Kwa lengo la kuimarisha utawala wa sheria, Serikali imefanya
jitihada kubwa ya kuziimarisha taasisi zinazosimamia utawala bora, watendaji
wake pamoja na mazingira ya kufanyia kazi.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo,
Serikali itaongeza kasi katika kuziendeleza juhudi hizo kwa lengo la kuongeza
ufanisi. Pamoja na mambo mengine, Serikali ina mpango wa kujenga wa jengo jipya
la Mahkama Kuu huko Tunguu, kukamilisha ujenzi wa Mahkama ya Watoto Mahonda na
kuyafanyia matengenezo makubwa majengo ya mahkama ya Mfenesini, Mwanakwerekwe
na Wete na kuzisogeza huduma za Mahkama karibu na wananchi.
Mheshimiwa
Spika,
Katika kusimamia maadili ya viongozi na
nidhamu ya utumishi, Serikali katika kipindi kilichopita ilianzisha Sheria ya
Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Namba. 1 ya 2012 na Sheria ya Maadili ya
Viongozi wa Umma Namba 8 ya mwaka 2015.
Kufuatia sheria hiyo, Serikali ilianzisha Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na
Uhujumu Uchumi na hivi karibuni nitaianzisha Tume ya Maadili ya Viongozi wa
Umma.
Katika kipindi hiki, nitahakikisha
kwamba Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, inafanya kazi ipasavyo ili viongozi
wote waliotajwa katika sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma wanatangaza mali
zao kwa mujibu wa sheria hio. Kila
kiongozi atatakiwa atekeleze wajibu wake kwa wakati uliowekwa. Katika kupambana
na rushwa na uhujumu wa uchumi, Serikali haitomvumilia mtu yeyote
atakayebainika kuzibeza na kutaka kuzirudisha nyuma jitihada za Serikali
kutokana na udhaifu wake wa kimaadili.
Hapana asiyejua kuwa rushwa ni adui wa
haki na Mwenyezi Mungu ameikataza rushwa. Katika kulikemea jambo hili, Mwenyezi
Mungu katika aya ya 188 ya Surat Al-Baqarah ametuasa kwa kusema:”Wala msiliane mali zenu kwa batili na
kuzipeleka kwa mahakimu ili mpate kula sehemu ya mali ya watu kwa dhambi, na
hali mnajua”. Kadhalika, ipo hadithi
mashuhuri ambapo, Mtume Muhammad (SAW) amesema kwamba: “Mwenyezi Mungu amemlaani mtoa rushwa na mpokeaji rushwa na
anaeshuhudia na anaeandika”.
Lakini Serikali nayo inaichukia na
inaipiga vita, ndio maana tunafanya
jitihada za kushughulika nayo na
tumelazimika kutunga Sheria ya Kuzuia na Rushwa na Uhujumu Uchumi. Kwa upande mwengine, wananchi nao wanaichukia
rushwa na hawavipendi vitendo vinavyoambatana nayo. Wapo wananchi
wanaovijua vitendo vinavyoashiria
rushwa ambavyo vinafanywa katika maofisi yetu, inasemekana baadhi yao
wanadiriki kuvisema. Tutawachunguza
viongozi na watumishi wanaofanya vitendo hivyo, kwa kuzingatia sheria na
taasisi zake, ili tuujue ukweli na hatimae tuchukue hatua. Iwapo mambo hayo yanayofanyika, wanayoyasema
baadhi ya wananchi; ndio hayo yanayoitwa
majipu, basi nataka niahidi, tutayatumbua na moyo wake tutautoa.
Nataka niwahakikishie wananchi kwamba,
kauli yangu hii si maneno matupu bali yataambatana na vitendo.
Mheshimiwa
Spika,
Vile vile, katika jitihada zetu za
kusimamia matumizi bora ya fedha za umma, Serikali itadhibiti na kuzuwia safari
za nje za kikazi zisizo za lazima.
Semina, kongamano na mikutano inayofanywa kwa kutoa posho wakati wa saa
za kazi, itawekewa utaratibu mpya. Serikali itahakikisha kuwa ubora wa miradi inayotekelezwa na ununuzi wa vifaa na
huduma mbali mbali zinalingana na thamani ya fedha zilizotumika (Value for
Money). Zipo taarifa kwamba kuna
ubabaishaji mkubwa unafanyika, katika ununuzi wa vifaa na nyenzo. Ni jukumu la Watendaji Wakuu na wale wote
wenye dhamana ya manunuzi na kuidhinisha miradi, kuzingatia Sheria Namba 9 ya
2005 ya Manunuzi na Uondoshaji wa Mali za Umma,
wahakikishe kwamba taratibu zote za manunuzi zinafuatwa.
Nachukua nafasi hii, kuwahimiza
viongozi watakaopewa nyadhifa mbali mbali kuwa wabunifu katika kupanga na
kutekeleza mipango iliyo kwenye dhamana walizokabidhiwa. Ni vigumu kwenda
katika kasi tunayoitaka ikiwa kila kiongozi atategemea maelekezo na mipango
kutoka kwa Rais au Makamu wake ndipo atekeleze wajibu wake. Nawahimiza viongozi
watakaopewa dhamana kutumia utaalamu wao kwa kuleta maendeleo na lazima
waielewe mipango na sheria zinazohusiana na majukumu waliyopewa na taasisi
wanazozifanyia kazi na kuzitekeleza ipasavyo.
Lazima waifanye kazi ya kuwasimamia watumishi walio chini yao na wale
watakaozikiuka sheria na taratibu watapaswa wawachukulie hatua na
kuwawajibisha. Kama hawatafanywa hivyo,
basi na wao watawajibishwa.
Mheshimiwa
Spika,
Katika utekelezaji wa utawala bora,
nitaendelea kuhakikisha kuwa Mihimili yetu Mitatu, (Serikali, Baraza la
Wawakilishi na Mahkama), kila mmoja unafanya kazi ukiwa huru na kwa mujibu wa
sheria zilizobainishwa katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. Tutahakikisha
kila muhimili unapata fedha za kuendesha shughuli zake kwa mujibu wa uwezo wa
Bajeti ya Serikali na si zaidi ya hilo.
Hapatakuwa na fedha za ziada, zaidi ya zile zitakazopitishwa katika bajeti.
BARAZA
LA WAWAKILISHI
Mheshimiwa
Spika,
Kwa mara nyengine tena, nakupongezeni Waheshimiwa
Wajumbe wa Baraza hili kwa kuchaguliwa
na wananchi ili muwawakilishe
katika Baraza hili la Tisa. Sote
tunafahamu kwamba ili ushinde nafasi ya Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi,
panahitajika juhudi na ujasiri mkubwa. Aidha, mgombea anahitaji busara, hekima,
uvumilivu, ufasaha na uwezo wa kujieleza na mapenzi kutoka kwa wananchi. Hapana
shaka, nyinyi mnapendwa na ni chaguo la wananchi. Kwa msingi huo, mtaithamini
heshima waliyokupeni wananchi kwa kukuchagueni ili muwaongoze na mshirikiane
nao katika jitihada za kuiletea maendeleo ya nchi yetu. Kazi iliyo mbele yetu
ni kushikamana katika kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia maadili ya uongozi na
sheria mbali mbali zinazotuongoza.
Ni matumaini yangu kuwa mtatekeleza
wajibu wenu kwa kuzingatia kifungu cha
88(a-d) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na kanuni za Baraza la Wawakilishi
ziliopo; utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 pamoja na mipango mengine ya maendeleo. Chombo hiki kinaendeshwa kwa taratibu za
sheria na kanuni. Kwa hivyo, kila mjumbe
anawajibika kuzifuata na kutekeleza majukumu yake kufuatana na sheria na kanuni
hizo.
Nimefarajika kwa kuwepo mchanganyiko
mzuri wa Waheshimiwa Wajumbe wapya pamoja na wale wa zamani, wenye uzoefu wa
shughuli za Baraza la Wawakilishi.
Mchanganyiko huo, unanipa matumaini makubwa kwamba shughuli za Baraza
zitapata ufanisi mkubwa. Waheshimiwa
Wajumbe wenye uzoefu, hamna budi kuwasaidia na kuwaongoza wajumbe wapya na wao
wawe tayari kujifunza kutoka kwenu.
Aidha, nimeridhishwa na kuwepo kwa idadi kubwa ya wajumbe wanawake na
vijana katika Baraza hili, jambo ambalo
limeongeza fursa ya uwakilishi wa makundi haya yenye idadi kubwa ya watu katika
jamii yetu. Hongereni sana.
Naamini kwamba mtarejesha imani
waliyokupeni wananchi wa Zanzibar, kwa kuunga mkono juhudi zangu za kupambana
na rushwa, ubadhirifu na uhujumu wa uchumi katika nchi yetu. Kadhalika, mtafanya hivyo kwa michango
mtakayoitoa katika Baraza hili na kwa vitendo kwa utekelezaji wa Sheria ya
Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Naelewa kwamba nyinyi ni makini na mahiri na sina shaka mtatekeleza wajibu wenu
ipasavyo.
IDARA MAALUM ZA SMZ
Mheshimiwa
Spika,
Idara Maalum za SMZ zimeonesha umahiri,
ukakamavu na umakini wao katika kutekeleza Sera ya CCM ya kulinda na kudumisha
amani nchini katika kipindi chote cha miaka mitano iliyopita. Idara Maalum zimeshirikiana vya kutosha na Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuzima majaribio pamoja na kukomesha
viashirio vya uvunjaji wa amani nchini.
Idara hizi ziko mstari wa mbele katika
kutoa huduma za jamii kwa wananchi hasa elimu na afya kupitia taasisi, skuli,
vyuo na hospitali zilizoanzishwa ndani ya vituo vya Idara Maalum. Vile vile,
zimekuwa zikishiriki kikamilifu katika michezo ambapo zimefanikiwa kutwaa
ubingwa katika mashindano mbali mbali.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo,
Serikali itazidi kuziimarisha Idara Maalum za SMZ kwa kuwapatia watendaji wake
mafunzo, vifaa vya kisasa na kuimarisha maslahi yao kadri hali itakavyoruhusu
ili kuwawezesha kutekeleza majukumu ipasavyo. Nitatekeleza ahadi yangu
niliyoitoa kwao wakati wa Kampeni za uchaguzi ya kuangalia upya maslahi yao ili
yalingane na wenzao wa SMT kwa lengo la kuwapunguzia ukali wa maisha na
kuongeza ufanisi katika kazi zao. Kama
nilivyoeleza hapo mwanzo kwamba, suala hili litategemea uwezo wa Serikali
katika kukusanya mapato. Uamuzi si
tatizo na tayari nishaufanya.
USHIRIKIANO
NA NCHI NYENGINE NA WAZANZIBARI WANAOISHI NJE
Mheshimiwa
Spika,
Katika uongozi wangu, nitahakikisha
Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaendelea kuwa
na uhusiano na mashirikiano mema na nchi mbali mbali duniani pamoja na
Mashirika ya Kimataifa juu ya masuala mbali mbali ya kiuchumi, kisiasa na
kijamii. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha ushirikiano na Jumuiya ya
Afrika Mashariki pamoja na Jumuiya nyengine za Kikanda ambazo Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ni mwanachama.
Katika kipindi cha pili cha Awamu ya
Saba, nitahakikisha tunazidi kukiimarisha Kitengo maalum nilichokianzisha cha
kuratibu masuala ya Wazanzibari Wanaoishi Nchi za Nje ili kiendelee
kuwashajiisha kushiriki katika shughuli
za maendeleo ya nchi yetu. Nitaendelea kukutana nao kila ninapopata fursa ya
kuzitembelea nchi wanazoishi, ili tubadilishane mawazo kwa maslahi ya nchi yetu.
Tumedhamiria kuandaa Kongamano la Kimataifa la Wanadiaspora mwezi Agosti, 2016
ambalo litawashirikisha Wanadiaspora wa Zanzibar kwa jumla wanaoishi katika
mataifa mbali mbali. Lengo la Kongamano
hilo, ni kuushajiisha ushiriki wa Watanzania katika kupanga na kutekeleza
mipango mbali mbali ya maendeleo ya nchi yetu.
Napenda nitoe shukurani zangu za dhati
kwa “Wanadiaspora” kwa michango mikubwa wanayoendelea kuitoa, ya hali na mali,
kwa ajili ya kuendeleza sekta za kiuchumi na kijamii hasa kuendeleza elimu,
afya, biashara na uwekezaji. Nawaomba
waendelee kuwa pamoja nasi kwani; ‘Mtu Kwao ndio Ngao’.
KUWAUNGANISHA
WANANCHI WA ZANZIBAR
Mheshimiwa
Spika,
Miongoni mwa majukumu tuliyoyatekeleza
kwa ufanisi katika kipindi chote cha miaka mitano ya kwanza ni kuendeleza
mshikamano, umoja na mapenzi baina ya watu wa Zanzibar bila ya kujali rangi,
kabila, dini na itikadi zao za kisiasa.
Mafanikio tuliyoyapata ni matunda ya kushiriki kila mmoja wetu katika
kudumisha na kujenga mshikamano tukiwa na imani ya dhati kwamba Wazanzibari
sote ni wamoja. Kuwepo kwa amani na utulivu ni mambo yaliyotupelekea kudumisha
umoja wetu na kupata maendeleo makubwa.
Lazima nikiri kwamba dhamana ya
kusimamia udugu na mshikamano tulionao ina changamato nyingi. Lakini changamoto hizo tumeweza kuzipatia
ufumbuzi kwa sababu sote tuliufahamu wajibu wetu na tuliongozwa na hekima,
busara na subira. Tulifahamu kwamba
suala la amani, umoja na mshikamano tunajifanyia wenyewe na hatumfanyii mtu
yeyote. Hii ndio siri ya mafanikio yetu.
Kwa kuzingatia hayo, namshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kutekeleza dhamana yangu, kwa kipindi chote cha
miaka mitano na leo hii, Zanzibar iko salama na yenye utulivu mkubwa. Namuomba
Mola atuvushe kwa salama katika kipindi cha miaka mitano ijayo na katika awamu
nyengine zote zinazokuja. Nataka nikuhakikishieni nyinyi Waheshimiwa Wajumbe,
niwahakikishie wananchi wote wa Zanzibar na Watanzania wote kwamba, nitaendelea
kuwa muumini wa kweli wa amani na utulivu; na kufanya kila linalowezekana kwa
ajili ya kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar kwa lengo la kuimarisha udugu na
mapenzi miongoni mwetu, ili nchi yetu iweze kupiga hatua zaidi za maendeleo.
Mheshimiwa
Spika,
Nitaendelea kuyalinda maslahi ya
Zanzibar na watu wake na kutimiza wajibu wangu wakati wote, bila ya kumuonea muhali mtu yeyote, kumfanyia
chuki au kuogopa kama nilivyokula kiapo nilipoapishwa kuwa Rais. Kwa yeyote
atakaejaribu kuibeza Katiba ya Zanzibar ya 1984 na kuchezea amani na utulivu
tulio nao nitapambana nae. Nitaendelea kutumia hekima na busara kwa ajili ya
kuyalinda Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964 na kuyalinda maslahi ya Zanzibar
na watu wake.
Nayasema haya kwa dhati ya moyo wangu.
Hii ndio imani yangu na ninaamini kuwa nyote mko tayari kwa kuyalinda Mapinduzi
ya tarehe 12 Januari, 1964 na kuyatetea maslahi ya Zanzibar na watu wake na
Tanzania kwa jumla.
Nafarijika kuona kwamba viongozi wa
dini zilizopo nchini na wananchi wote wenye kuifahamu historia na kuitakia mema
nchi yetu na Muungano wetu wapo pamoja nasi katika kudumisha amani
itakayotupelekea kuyafikia malengo ya Mapinduzi yetu Matukufu ya tarehe 12
Januari, 1964. Kwa misingi huo, sote tuelewe kuwa suala la kudumisha mshikamano
ni la kila mmoja wetu wakiwemo viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, madhehebu
ya dini na viongozi wengine katika jamii na wananchi wote kwa jumla. Kila
mwananchi hana budi atii, ayaheshimu matakwa ya Katiba ya Zanzibar ya 1984,
Sheria zake na kanuni mbali mbali zilizotungwa katika kuendesha shughuli za
kiserikali na kijamii. Huu ni wajibu wetu
hatuwezi kuukwepa na hatuna budi lazima
tuutekeleze.
Mheshimiwa
Spika,
Sote tunafahamu kwamba tarehe 20 Machi,
2016, tulikuwa na Uchaguzi Mkuu wa marudio ulioendeshwa na kusimamiwa na Tume
ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya 1984 na Sheria ya
Uchaguzi Nambari 11 ya mwaka 1984.
Madhumuni ya uchaguzi huo yalikuwa ni kuchaguliwa kwa viongozi wa vyama
vya siasa wakataoingoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kipindi cha miaka
mitano ijayo.
Katika Uchaguzi Mkuu huo wa Marudio wa
tarehe 20 Machi, 2016 nafasi ya Rais iligombewa na vyama 14 vya siasa na
hakukuwa na Chama chochote zaidi ya Chama cha Mapinduzi, kilichopata matokeo ya
kura za Uchaguzi wa Rais kwa zaidi ya asilimia 10. Mimi nikiwa Mgombea wa Urais wa CCM,
nilipata asilimia 91.4. Kadhalika,
hakukuwa na Chama cha siasa zaidi ya CCM chenye wingi wa Viti vya Majimbo
katika Baraza la Wawakilishi. Kwa
kuzingatia msingi huo, na kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 39(3) cha
Katiba ya Zanzibar ya 1984, hakuna Chama cha siasa ambacho kinakidhi masharti
ya kustahiki kutoa Makamo wa Kwanza wa Rais ili kuunda Serikali ya Umoja wa
Kitaifa. Huo ni uamuzi wa wananchi wa
kukipa ushindi mkubwa Chama cha Mapinduzi na hawakutoa nafasi ya kumchagua
Makamu wa Kwanza wa Rais. Huo ni uamuzi
wao wa kidemokrasia. Kadhalika, uteuzi
wa nafasi ya Makamo wa Pili wa Rais umewekewa masharti na kifungu cha 39(6),
kuwa:-
(i)
Atateuliwa kutoka miongoni
mwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
(ii)
Atoke katika chama
anachotoka Rais. Uteuzi nilioufanya wa
kumteua Makamu wa Pili wa Rais umekidhi matakwa ya kifungu cha 39(6) cha Katiba
ya Zanzibar ya 1984.
Nimelazimika nilieleze jambo hili la
kikatiba, kwa sababu wapo waliodhani kuwa yupo Mgombea anayestahiki kuwa Makamu
wa Kwanza wa Rais, lakini Rais amekataa kumteua na hivyo Katiba imekiukwa. Nililolifanya, la kumteua Balozi Seif Ali
Iddi kuwa Makamo wa Pili wa Rais ni sahihi na ni kwa mujibu wa Katiba na
nimechukua hatua ya kuunda Serikali kwa kuzingatia Katiba ya Zanzibar ya 1984.
Mheshimiwa
Spika,
Nataka niwahakikishie Waheshimiwa
Wajumbe wa Baraza lako tukufu, kwamba Serikali nitakayoiunda itasimamia misingi
ya haki, uwajibikaji, uwazi na usawa kwa wananchi wote, bil ya kumbagua mtu
yeyote kutokana na itikadi yake, dini yake, jinsia au eneo analotoka. Mimi ni Rais wa wananchi wote wa Zanzibar. Nitashirikiana na viongozi mbali mbali, wa
vyama vya siasa, viongozi wa dini, na kadhalika. Zanzibar ni yetu sote, viongozi wa vyama vya
siasa tuna jukumu la kushikamana na kuwatumikia wananchi kwa ajili ya maendeleo
yao.
Nataka nirudie ule usemi wangu wa
mwanzo kwamba, viongozi jukumu letu hivi sasa, kila mmoja wetu na sote kwa
pamoja tufanye kazi kwa bidii na maarifa tupate maendeleo tunayoyakusudia. Uchaguzi umekwisha na washindi wamepatikana
ambao wataiongoza nchi yetu kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, hadi hapo
utakapofanyika uchaguzi mwengine mwaka 2020.
KUIMARISHA
MUUNGANO
Mheshimiwa
Spika,
Suala la kulinda na kudumisha Muungano
wetu wa Serikali mbili, kwangu halina mbadala. Nitaendelea na juhudi za
kudumisha Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar wa Serikali mbili,
ulioasisiwa mwaka 1964 ambao unatimiza Miaka 52 ifikapo tarehe 26 Aprili 2016.
Waheshimiwa Wajumbe, tuna wajibu wa
kuhakikisha kwamba Serikali zetu mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinaendelea kuimarisha
mashirikiano na kufanya kazi kwa umoja na ukaribu zaidi katika kupanga na kuitekeleza
mikakati ya uchumi na mipango mengine ya maendeleo. Nitaiongoza vyema Zanzibar
na kuhakikisha kwamba tunaimarisha mashirikiano, udugu na mapenzi baina ya watu
wa pande mbili hizi. Nitaendelea
kushirikiana na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania katika kudumisha hali ya amani na utulivu, iliyodumu tangu
kuundwa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Aprili, 1964.
Mheshimiwa
Spika,
Kutokana na kazi nzuri ya kuzipatia
ufumbuzi changamoto au kero mbali mbali za Muungano wetu, iliyofanywa katika
kipindi kilichopita, ni mambo machache tu ndio yaliyobaki kupatiwa ufumbuzi.
Kwa yale mambo yanayohitaji taratibu za kisheria, naamini kwamba Baraza lako,
Mheshimiwa Spika, litatimiza wajibu wake ipasavyo. Kwa kufanya hivyo, mtachangia kwa kiasi
kikubwa katika kuudumisha Muungano wetu na kuwarahishia wananchi kutekeleza
shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
MWISHO
Mheshimiwa
Spika,
Namalizia hotuba yangu kwa kukupongeza
kwa mara nyengine tena Mheshimiwa Spika, kwa kuchaguliwa kuliongoza Baraza
hili. Nakutakia mafanikio katika kutekeleza majukumu yako mazito yenye umuhimu
kwa maendeleo ya nchi yetu. Vile vile, napenda kukupongezeni kwa mara nyengine
tena, Waheshimiwa Wajumbe, kwa heshima kubwa mliyopewa na wananchi ili
muwaongoze na muwawakilishe katika Baraza hili.
Natoa pongezi kwa Waheshimiwa wote waliochaguliwa katika nafasi mbali
mbali za uongozi pamoja na watendaji wote wa Baraza hili, wakiongozwa na Katibu
wa Baraza la Wawakilishi Dkt. Yahya Khamis Hamad. Nakutakieni kila la kheri na
mafanikio katika kuwatumikia wananchi wote kwa jumla.
Natoa shukurani maalum kwa wamiliki wa vyombo vya habari na watendaji
wao kwa mashirikiano yao na kutangaza habari zinazohusu nchi yetu na hafla hii
ya uzinduzi wa Baraza hili. Shukurani za pekee ziwaendee wananchi wote kwa
jumla kwa kunisikiliza kwa utulivu kwa muda wote niliokuwa nikiwasilisha hotuba
yangu. Namuomba Mwenyezi Mungu aturahisishie utekelezaji wa majukumu
tuliyopewa, atuzidishie mapenzi na mshikamano baina yetu na aijaze baraka na
neema nchi yetu.
Baada
ya kusema hayo, sasa natamka kwamba Baraza la Tisa la Wawakilishi la Zanzibar
limezinduliwa Rasmi, leo tarehe 05 Aprili, 2016.
MUNGU
IBARIKI ZANZIBAR
MUNGU
IBARIKI TANZANIA
MUNGU
IBARIKI AFRIKA
Ahsanteni
kwa kunisikiliza.
0 comments :
Post a Comment