Halmashauri
ya Jiji la Tanga ipo hatarini kuvunjwa kufuatia madiwani wake kushindwa
kuelewana katika kikao kilichositishwa leo na Mkurugenzi mtendaji.
Kikao
hicho cha baraza la madiwani wa Halmashairi ya Jiji la Tanga kwa mujibu
wa barua za mwaliko walizopewa madiwani hao kilikuwa ni cha mwendelezo
wa mkutano wa desemba 19 mwaka jana ambacho pia kilivunjika baada ya
kutokea vurugu.
Chanzo
cha kuvunjika kikao cha leo ni baada ya diwani wa kata ya Tangasisi
(CUF) ambaye pia ni Naibu Meya, Mohamed Haniu kuchukua kipaza sauti na
kutangaza kwamba kama wanataka kikao hicho kiendelee ni lazima ufanyike
uchaguzi wa Meya.
“Kwenye
wito wa barua za kikao hiki hakuna ajenda ya uchaguzi kwa hivyo
tukubaliane kwanza kwamba tunaanza na uchaguzi wa Meya ndipo tuendelee
kwa sababu hatuna meya hadi sasa”alisema Haniu.
Tangazo
hilo lilisababisha madiwani wa kutoka chama cha wananchi (CUF)
kushangilia jambo lililomlazimu Meya wa Jiji, Mohamed Mustapha
(Selebosi) kutamka kwamba kikao anakiahirisha.
Tamko la Selebosi lilisababisha madiwani wa CUF kushangilia kwa mara ya pili huku wakiimba nyimbo za kukisifu chama hicho.
Baada
ya kuahirishwa kwa kikao hicho,Meya wa Jiji hilo, Mohamed Selebosi,
Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Abdullah Lutavi, Mbunge wa Jimbo la Tanga,
Mussa Mbarouk na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Dk Wedson Sichalwe waliingia
katika ofisi ya Mkurugenzi kufanya kikao chao cha ndani.
Akizungumza
na waandishi wa habari,Kaimu Mkurugenzi , Sichalwe alisema ajenda
ambazo zilikuwa zijadiliwe ni kuunda kamati za kudumu za halmashauri,
kupanga ratiba za vikao vya halmashauri, kupokea taarifa ya utendaji wa
halmashauri katika kipindi ambacho madiwani hawakuwepo na kupokea
taarifa ya Serikali.
“Kama
mlivyoshuhudia kikao kimevunjika,inapotokea vurugu kama vile hakuna
sababu ya kuendelea na kikao, sheria inamruhusu Meya kukivunja” alisema Dk Sichalwe na kusisitiza kuwa taarifa zaidi atatoa baadaye.
Diwani
wa Kata ya Duga (CUF), Halid Rashid alisema watakuwa tayari kuendelea
na kikao iwapo madiwani wa CCM watakubali uchaguzi wa nafasi ya meya
ufanyike upya kwa sababu hawamtambui Mohamed Mustafa kama Meya.
“Ni
bora Halmashauri ya jiji ivunjwe kama Serikali inalazimisha tumtambue
Selebosi kuwa ni Meya, sisi hatutakubali akae mbele kuongoza kikao aje
huku ndiyo kikao kiendelee” alisema Halid.
Mohamed
Haniu (CUF) alisema anaamini Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela
anaweza kumaliza mgogoro wa nafasi ya Meya wa Tanga kwa kutumia busara
ya kuamuru uchaguzi wa meya ufanyike upya.
Diwani
wa kata ya Chumbageni (CCM) Saida Gaddafi aliwataka madiwani kutoka
chama cha CUF kukubali matokeo yaliyomtangaza Selebosi kuwa Meya kwa
sababu hata wao walimkubali Mohamed Haniu kuwa Naibu Meya.
Mkuu
wa Wilaya ya Tanga aliwahimiza madiwani wa Jiji kukubaliana ili vikao
vya kupitisha miradi ya maendeleo ya wananchi viweze kuendelea.
Dalili
za kutokea vurugu katika kikao hicho zilijitokeza mapema kufuatia jeshi
la polisi kumshikilia Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Tanga na aliyekuwa
mgombea wa nafasi ya Meya wa jiji la Tanga, Rashid Jumbe asubuhi kabla
ya kuanza kikao hicho.
Taarifa
za kushikiliwa na jeshi la Polisi diwani huyo zilienea na hata kikao
kilipoanza hakuwepo ukumbini ambapo madiwani wenzake walisema alikamatwa
kwa madai ya kuratibu shughuli za matangazo kuhusiana na kikao hicho
kwa kutumia gari lililopita mitaani.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Tanga,Leonard Paul alithibitisha kukamatwa kwa
diwani Rashid Jumbe na kwamba alikuwa akituhumiwa kutangaza mitaani kwa
kutumia gari kuhusu kikao hicho.
0 comments :
Post a Comment