………………………………………………………………………
Habari picha na- Aron Msigwa – MAELEZO.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu
imetangaza Mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi Machi 2016 na kusema kuwa
umepungua kidogo hadi kufikia asilimia 5.4 kutoka asilimia
5.6.iliyokuwepo mwezi Februari, 2016.
Hii inamaanisha kuwa kasi ya
upandaji wa bei ya bidhaa na huduma kwa mwezi Machi 2016 imepungua
kidogo ikilinganishwa na kasi ya upandaji wa bei ya bidhaa na huduma
iliyokuwepo mwezi Februari mwaka huu.
Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na
Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bw. Ephraim
Kwesigabo akitoa taarifa ya Mfumuko wa Bei wa Mwezi Machi, 2016 leo
jijini Dar es salaam amesema kuwa kupungua kwa mfumuko huo
kumesababishwa na kupungua kwa bei ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo
za vyakula katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema Takwimu zilizokusanywa
katika mikoa yote ya Tanzania Bara Machi 2016 kwa mujibu wa bei za
bidhaa zilizoainishwa kupima mfumuko wa bei zinaonyesha kuwa bidhaa
zisizo za vyakula katika soko zikiwemo Gesi, dizeli na mafuta ya taa
zimechangia kupungua kwa mfumuko huo.
Amesema kuwa pamoja na kupungua
kwa kasi ya upandaji wa bei ya bidhaa hizo mwezi Machi mwaka huu baadhi
ya bidhaa za vyakula zikiwemo za mchele, Mahindi, vyakula kwenye
Migahawa na mkaa zimeonesha kuongezeka katika soko.
Kuhusu Fahirisi za Bei ambacho ni
kipimo kinachotumika kupima mabadiliko ya bei ya bidhaa na huduma
zinazotumiwa na kaya binafsi hapa Tanzania kwa mwezi Machi, Kwesigabo
amesema kuwa zimeongezeka hadi kufikia 101.93 kutoka 101:44 za mwezi
Februari.
Amesema baadhi ya bidhaa za
vyakula za vyakula zikiwemo unga wa muhogo, matunda, maharagwe na samaki
zimechangia kuongezeka kwa Fahirisi hizo na kuongeza kuwa bidhaa zisizo
za vyakula zilizochangia ongezeko hilo ni Mavazi ya wanawake, mkaa na
kuni.
Kwa upande wa uwezo wa shilingi
100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za mlaji kwa mwezi Machi
, 2016 umefikia shilingi 98 na senti 11 ikilinganishwa na uwezo wa
shilingi 98 na senti 58 wa mwezi Februari 2016.
“Uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania
katika kununua bidhaa na huduma zilezile kwa mlaji kwa mwezi Machi 2016
umepungua, hii ina maana kuwa sasa mtu kuongeza ziada ili aweze kununua
bidhaa na huduma sawa na zile alizokuwa na uwezo wa kuzinunua mwezi
Februari”
Kwa upande wa mfumuko wa Bei kwa
nchi za Afrika Mashariki mwezi Machi, 2016, Kwesigabo amesema una
mwelekeo unaofanana; Kenya umepungua kidogo hadi kufikia asilimia 6.45
kutoka 6.84 huku Uganda ukifikia asilimia 6.2 kutoka asilimia 7.0 za
mwezi Februari.


0 comments :
Post a Comment