Kamati
ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji (PIC) imeshtushwa baada ya kubaini
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilitumia Sh18 bilioni mwaka
2013/2014 kwa ajili ya mafunzo, semina na warsha.
Makamu
mwenyekiti wa kamati hiyo, Lolesia Bukwimba alisema matumizi ya fedha
hizo ni makubwa ikilinganishwa na kazi iliyofanywa na mamlaka hiyo kwa
mwaka huo wa fedha.
Alisema wakati mapato ya TCRA kwa mwaka huo yalikuwa Sh79 bilioni, gharama za uendeshaji zilikuwa Sh76 bilioni.
“Hii
ina maana fedha zilizopelekwa Hazina zilikuwa kidogo. Kama mamlaka
ingepunguza matumizi, Serikali ingepata mapato ya kutosha,” alisema.
Bukwimba alisema hilo ni tatizo na kamati hiyo itatoa maagizo kwa mamlaka hiyo Jumamosi ijayo itakapoitembelea.
“Kuna
mambo mengi ya kitaalamu ambayo tunahitaji kuona shughuli zake
zinazofanywa na mamlaka, tutatoa maagizo siku ambayo tutaitembelea,” alisema Bukwimba.
Hata
hivyo, mwenyekiti wa Bodi ya TCRA, Profesa Haji Semboja aliitetea
mamlaka hiyo akisema kiasi hicho kilichotumika kwa ajili ya semina,
mafunzo na warsha kinatokana na unyeti wa taasisi hiyo.
“Taasisi
inasimamia kampuni zinazotoa huduma za teknolojia za kisasa ambayo ni
ngeni hapa kwetu, hivyo wafanyakazi wetu wanatakiwa kuwa na ufahamu
zaidi ya hao watoa huduma,” alisema Profesa Semboji.
Semboja, ambaye ni mchumi, alisema: “Pamoja
na mambo mengine, wafanyakazi wetu wanasimamia kampuni za mitandao ya
simu, matoleo ya simu yanatoka mara kwa mara, wanatakiwa kufahamu
teknolojia wanayoisimamia. Hapa ni lazima waende darasani.”
Alisema
wafanyakazi hao wakiachwa bila kupata mafunzo ya mara kwa mara
watajikuta baada ya kipindi kifupi wanapitwa na teknolojia zinazozidi
kuibuka kila wakati.
Kwa
upande wake, Sabrina Sungura ambaye ni mjumbe na mbunge wa Viti
Maalumu, aliitaka mamlaka hiyo kufanya marekebisho ya minara ya simu
mkoani Kigoma.
0 comments :
Post a Comment