Mtoto mmoja anayefahamika kwa jina la Kelvin (2) amekutwa amekufa katika chemba ya choo baada ya kupotea kwa siku mbili na kutafutwa na wazazi wake bila mafanikio.
Tukio hilo lilitokea Jumanne ya Mei, 24 katika eneo la Manzese, Mferejini ambapo mashuhuda wanaomfahamu mtoto huyo walisema kuwa alipotea siku ya Jumapili Mei, 22 na kutafutwa na wazazi wake bila mafanikio.
“Kuanzia Jumapili anatafutwa hajapatikana wakaenda hadi kutangaza msikitini na taarifa ikarushwa ITV kuhusu kupotea kwake lakini hakukuwa na mafanikio yoyote,” mmoja wa mashuhuda aliiambia Mo Blog.
Alisema kuwa kupatikana kwa mtoto katika chemba ya choo ni baada ya fundi ambaye alitakiwa kujenga chemba hiyo ambayo ilikuwa imefunikwa na mabati na alipofungua ndipo alipokuta mtoto akiwa ndani ya chemba hiyo.
Baada ya kuona hivyo, fundi huyo ambaye ni ndugu na mmiliki wa nyumba alitoa taarifa kwa uongozi wa mtaa ambao walitoa taarifa kwa vyombo vya usalama ikiwemo Jeshi la Polisi na Jeshi la Zimamoto ambao walifika eneo la tukio na kumtoa mtoto katika chemba na kuondoka nae.
Aidha taarifa zingine zinaeleza kuwa hadi tukio hilo linatokea mama wa mtoto alikuwa kanisani katika maombi ya kumuombea mtoto wake na baba wa mtoto akiwa nyumbani ambaye alionekana kushtushwa na hali aliyoiona kwa mtoto wake na hivyo wasamalia wema wakamtoa eneo la tukio na kumpeleka nyumbani ili kumtuliza na tukio hilo ambalo limemtokea mtoto wake.












Blogger Comment
Facebook Comment