Wednesday, December 2, 2015
@nkupamah blog
Wakazi watano wa Zanzibar wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka ya kusafirisha kobe 201 aina ya India wenye thamani ya Sh30 milioni.
Wakili
wa Serikali Ester Martin akishirikiana na Neema Mwanga, aliwataja
washtakiwa hao kuwa ni David Mungi (36), Mustafa Bakar (43), Mohammed
Seleman (43), Salum Wakili (30) ambao ni wafanyabiashara na mvuvi,
Shaban Haji (45).
Wakili
Martin alidai kuwa kati ya Novemba 1 na 16 katika maeneo tofauti jijini
Dar es Salaam na Zanzibar, washtakiwa hao kwa pamoja walisafirisha
nyara za Serikali kinyume cha sheria ya wanyama pori.
Ilidaiwa kuwa Novemba 16 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), washtakiwa hao walikamatwa na kobe hao.
Alidai
kuwa washtakiwa Seleman, Wakili na Haji wanadaiwa kuwa katika kipindi
hicho katika maeneo tofauti walipokea na kusafirisha nyara hizo bila ya
kibali cha wanyama pori.
Baada
ya kusomewa mashtaka hayo, upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi
bado haujakamilika na washtakiwa hawakuruhusiwa kuongea chochote kwa
kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi
hadi watakapofikishwa Mahakama Kuu baada ya upelelezi kukamilika.
Hakimu
Mkazi, Respicius Mwijage aliahirisha kesi hadi Desemba 14 na kuwashauri
washtakiwa kuwasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu.
Washtakiwa hao walirudishwa rumande.
0 comments :
Post a Comment