Mfumuko
 wa bei wa taifa wa mwezi Juni, 2016 umeongezeka hadi asilimia 5.5 
kutoka asilimia 5.2 mwezi uliopita kutokana na kuongezeka kwa kasi ya 
upandaji wa bei za bidhaa na huduma.
Akizungumza
 na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Sensa na
 Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephaim Kwesigabo amesema
 kuongezeka kwa mfumuko wa bei kumesababishwa na kuongezeka kwa bei za 
baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi.
“Mfumuko
 wa bei umesababishwa na kuongezeka kwa bei za vyakula kama vile mahindi
 ambayo yameongezeka kwa asilimia 3.2, unga wa muhogo kwa asilimia 2.4, 
samaki wabichi kwa asilimia 3.8, maziwa mgando kwa asilimia 4.3, 
maharage mabichi yaliyomenywa kwa asilimia 6.1, kitunguu swaumu kwa 
asilimia 12.5, njegere kwa asilimia 6.2, viazi mviringo kwa asilimia 
2.5, mihogo mibichi kwa asilimia 6.7, magimbi kwa asilimia 4.5, na ndizi
 za kupika kwa asilimia 2.7,” amesema Kwesigabo.
Amesema
 bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi za bei 
ni pamoja na huduma ya kinywa na meno ambayo imeongezeka kwa asilimia 
13.8, mafuta ya dizeli kwa asilimia 2.4 na mafuta ya petroli kwa 
asilimia 4.3.
Kwesigabo
 amesema mfumuko wa bei wa mwezi Juni, 2016 unaopimwa kwa kipimo cha 
mwezi umeongezeka kwa asilimia 0.5 ongezeko sawa na mwezi uliopita.
Aidha
 amesema mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwaka wa bidhaa za vyakula 
majumbani na migahawani umeongezeka hadi asilimia 8.3 mwezi Juni, 2016 
kutoka asilimia 7.2 mwezi Mei, 2016. Fahirisi za bei zimeongezeka hadi 
103.47 mwezi Juni, 2016 kutoka 103.00 mwezi uliopita.
Kwesigabo
 amesema uwezo wa Shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na 
huduma umefikia Shilingi 96 na senti 65 mwezi Juni, 2016 kutoka mwezi 
Disemba, 2015. 



Blogger Comment
Facebook Comment