Haikuwa ubashiri, badala yake
ilikuwa ni mipango thabiti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) kuhakikisha kwamba inavuna ushindi na kuwa mabingwa wa Kombe la
Chalenji la CECAFA kwa wanawake baada ya kuilaza Kenya mabao 2-1 katika
mchezo wa fainali uliofanyika Uwanja wa Nambole jijini Jinja nchini
Uganda.
Mabao ya timu ya taifa Tanzania ya
wanawake maarufu kama Kilimanjaro Queens katika mchezo wa leo Septemba
20, 2016 yamefungwa na Mwanahamisi Omari katika kipindi cha kwanza kabla
ya Kenya kujitutumua na kupata bao la kufutia machozi kipindi cha pili
katika mchezo uliokuwa na ushindani wa aina yake.
Matokeo hayo yatakuwa kupozwa kwa
ndugu zao wa Zanzibar Queens ambao walitolewa mapema katika mashindano
hayo yaliyoanza Septemba 11, 2016 kabla ya kufikia tamati leo katika
fainali hizo zilizovutia mashabiki wa mpira wa miguu nchini Uganda
ambako kila upande ulikuwa na watu wanaowasapoti.
Timu hiyo inatarajiwa kuondoka
nchini Uganda kesho Jumatano na kwenda moja kwa moja Kagera ambako
ilipiga kambi kabla ya kwenda Jinja. Itarudi hapo kusema ahsante kwa
wenyeji, lakini pia kuwapa pole ya janga la Tetemeko la Ardhi wakazi
lililotokea katika mikoa huo na mikoa jirani ya Kanda ya Ziwa na nchi
jirani. Mikoa ambayo iliathirika zaidi ni Kagera na Mwanza kadhalika
nchi jirani za Uganda na Rwanda.
Mara baada ya kuwapa pole, timu
hiyo itasafiri kutoka Kagera kwa usafiri wa anga ambako taratibu za
safari hiyo zitatangazwa na TFF hapo kesho ambako wananachi watapata
fursa ya kuipokea na kuishangilia timu hiyo inayonolewa na Kocha
Sebastina Nkoma akisaidiuwa na Hilda Masanche wakiwa chini ya Mwenyekiti
wa soka la wanawake.
Safari ya ubingwa wa Kilimanjaro
Queens ulianzia hatua ya makundi kwa kuilaza Rwanda manbao 3-2 kabla ya
kutoka sare tasa na Ethiopia ambayo pia ilivuna ushindi wa mabao 3-2
kutoka kwa Rwanda. Tanzania na Ethiopia zilitoka sare na kurusha sarafu
ambako Tanzania ikawa ya kwanza katika kundi B hivyo kucheza na Uganda
ambayo ililala kwa mabao 4-0 katika mchezo wa nusu fainali. Na leo
Septemba 20, 2016 ikatawazwa kuwa mabingwa kwa ushindi wa mabao 2-1.
Timu zote shiriki zilikuwa
Tanzania, Burundi, Zanzibar, Kenya, Ethiopia, Rwanda pamoja na mwenyeji
Uganda. Mashindano ya Kombe la Chalenji la CECAFA kwa timu za wanawake
yamefanyika kwa mara ya kwanza jambo linaloleta tafsiri kuwa michuano
hiyo inaweza kuinua soka la wanawake kwa ukanda wa nchi za Afrika
Mashariki na Kati.


0 comments :
Post a Comment