Kesi namba 208 ya mwaka 2016 ya gazeti la Mawio imeaghirishwa hadi Oktoba 4, 2016 baada ya mshitakiwa namba moja Tundu Lissu kutohudhuria mahakamani kwa ajili ya kusikiliza shitaka.
Awali, wadhamini wa Lissu Ibrahim Ahmed na Robert Katula walisimama mbele ya Hakimu Thomas Simba anayesimamia kesi hiyo, na kusema kuwa Lissu hakutokea leo mahakamani kwa sababu amesafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Hata hivyo, upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali Mutalemwa Kisheruji uliiomba mahakama kuzuia hati ya kusafiria ya mshitakiwa Lissu pamoja na kumuwekea sharti la kuiomba mahakama kibali cha kusafiria endapo atarudia tena kosa hilo kutokana kwamba hakufuata sheria kwa sababu alitakiwa kutoa taarifa mapema kabla ya siku ya shtaka kusikilizwa.
Lakini Hoja hiyo ilipingwa na Wakili wa upande wa utetezi Peter Kibatala na kuiomba mahakama kutenga siku nyingine ambapo alimuahidi hakimu kuwa kosa hilo halitajirudia tena na siku husika ya kusikilizwa shitaka mshatikiwa atakuja mahakamani.
Baada ya kusikiliza maombi ya pande zote mbili, Hakimu Simba alitoa onyo kali kwa mshitakiwa na kuwaambia wadhamini wa Lissu kuwa, endapo siku nyingi mshitakiwa huyo hatakuja mahakamani, wadhamini watalipa dhamana.
Hakimu Simba ameiaghirisha kesi hiyo hadi Oktoba, 4, 2016 baada ya mawakili wa pande zote mbili kuiridhia tarehe hiyo iwe siku ya kusikilizwa shtaka hilo.