Mchezaji na kocha wa zamani wa Simba, Abdallah King Kibaden amefunguka kuhusu uwekezaji ambao Mkurugenzi Mtendaji na Rais wa Makampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL Group), Mohammed Dewji anataka kuufanya katika klabu ya Simba kwa kununua hisa asilimia 51 kwa kitita cha Bilioni 20 za kitanzania.
Akizungumza katika kipindi cha Sports Xtra cha Clouds Fm, Kibaden alisema mchezo wa soka unahitaji pesa nyingi ili kufanikiwa na kama MO Dewji ana nia ya dhati kuwekeza pesa kwa ajili ya kuisaidia Simba basi yeye anakubaliana na jambo hilo.
“Pesa ni muhimu kwenye soka, kila kitu kinahitaji pesa, maana hata wachezaji wanalipwa, kuna vitu vingi vinahitaji pesa, inabidi wapatikane watu wa kutusaidia ili tuwe kwenye biashara maana mpira ni biashara na lazima kupata watu sahihi wa kufanya nao biashara, pesa inahitajika ili kufanikiwa,
“Kuwepo na matajiri sio tatizo, tunataka biashara ya kuleta maendeleo, mimi kama MO anataka kuwekeza nabariki kuchukua Simba na sio hata MO peke yake, kama kuna watu wengine watajitokeza ambao watataka kuwekeza wanaweza kujitokeza na kuwekeza,” alisema Kibaden.