Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema
kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika
kuhakikisha rasilimali ya gesi na mafuta inakuwa ni chachu ya kukuza
uchumi wa taifa na wa wananchi kwa ujumla.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema hayo jana
22-Nov-2016 Jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa mwaka wa
kujadili masuala ya gesi na mafuta barani Afrika ulioandaliwa na Kampuni
ya Getenergy ya Uingereza.
Katika hotuba yake, Makamu wa Rais aliwahakikishia
washiriki wa mkutano huo kuwa Tanzania imeweka mazingira mazuri ya
uwekezaji kwenye sekta ya mafuta na gesi na itakuwa bega kwa bega na
wadau wanaotaka kuwekeza katika sekta hiyo ili kuhakikisha uwekezaji
utakaofanyika unakuwa na manufaa kwa pande zote mbili.
Alisisitiza
kuwa kwa sasa Serikali ya Tanzania inaendelea na mkakati kabambe wa
kusomesha wataalamu wa fani ya mafuta na gesi ndani na nje ya nchi ili
kuhakikisha taifa linajitosheleza kwa wataalamu hao ambao watakuwa na
uwezo na ujuzi wa kufanya kazi kwa viwango vinavyotakiwa katika sekta za
gesi na mafuta.
Makamu wa Rais alisema
Tanzania imegundua kiasi kikubwa na gesi na ana imani kubwa kuwa mafuta
nayo yanapatikana hivyo ni muhimu kwa mataifa ya Afrika kujipanga kuwa
na wataalamu wake wazalendo wa kutosha watakaoshikiri katika uchumi wa
gesi na mafuta kwa kuajiriwa kwenye makampuni yanajihusisha na utafiti
na
uchimbaji wa gesi na mafuta.
Asema
anaimani kubwa kuwa rasilimali ya gesi na mafuta zitakazogundulika na
kuchimbwa barani Afrika zitasaidia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa
mataifa hayo, uchumi ambao utasaidia kuimarisha utoaji wa huduma bora
za kijamii kwa wananchi katika nchi husika.
Mkutano
huo wa siku Mbili wa Kimataifa umekutanisha wadau mbalimbali wa sekta
ya gesi na mafuta kutoka ndani na nje ya nchi ambao wanajadili kwa kina
na kubadilishana uzoefu kuhusu njia bora za uwekezaji katika sekta hiyo
barani Afrika.
Kwa upande wake,Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo alisisitiza kwa Serikali itaendelea kusomesha wataalamu wake ndani na nje ya nchi ili kujitosheleza kwa wataalamu wa sekta hiyo.



0 comments :
Post a Comment