Lowasa:Mikutano Ya Ndani Imekuwa Mitamu Zaidi Na Imetuimarisha


Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amesema anamshukuru  Rais Dk. John Magufuli kwa kuruhusu vikao vya ndani.

Amesema vikao hivo,  “ni vitamu zaidi kuliko vile ya nje.”

Hayo aliyasema   Dar es Salaam alipofungua mafunzo ya siku mbili kwa madiwani, wabunge na viongozi wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam yanayoendelea kutolewa na Shirika la Konrad Adenauer Stiftung (KAS) la   Ujerumani.

Akizungumzia   ziara za kanda zilizofanywa na viongozi wa chama hicho  hivi karibuni, Lowassa alisema vikao vya ndani vimewapa nafasi na muda mwingi wa kuzungumza na wanachama  kwa karibu zaidi.

“Tumefanya ziara, tumeona hali ya barabara ni nzuri lakini hali ni nzuri zaidi tulivyozungumza na wanachama wetu na tunamshukuru Rais.

“Aliona hakuna haja ya mikutano ya nje akatupatia vikao vya ndani, Loh! Ni vizuri, ni vitamu zaidi kuliko vile vya nje.

“Tunapata nafasi nzuri ya kuzungumza na wanachama ana kwa ana, kwa muda mrefu kwa mapenzi na mahaba.

“Nataka niwaambie Chadema ipo imara sana. Watu walidhani wamekata tamaa lakini wapo imara katika kuhakikisha chama kinapata ushindi  mwaka 2020,”alisema Lowassa.

Alisema yapo malalamiko madogo madogo likiwamo watu wengi kutaka uongozi wa chama.

Alipendekeza yawepo mabadiliko katika katiba ya nchi kuongeza nafasi za uongozi.

“Wana malalamiko madogo madogo lakini mengi ni ya uongozi, kila mtu anataka kuwa kiongozi hadi nikakumbuka kule Kenya walipobadilisha  Katiba wakaongeza nafasi za uongozi, magavana, mameya na nyingine ili zipatikane nafasi za siasa za kuongoza  na mimi nadhani tungepata muda tufafanue katiba ili ziongezwe nafasi za uteuzi.

“Au mnaonaje?” Lowassa aliwauliza wajumbe ambao kwa pamoja waliitikia: “Ndiyoo”

Alisema kuna kila dalili ya Chadema kushinda uchaguzi wa 2020.

Aliwataka  viongozi wa chama hicho kushikamana na kuepuka maneno ya kuwagawa akisisitiza kuwa  bila mshikamano hawataweza kushinda uchaguzi ujao.

“Dalili zote zinaonyesha tutashinda lakini kama tutakuwa wamoja.

“Bila umoja hatuwezi kushinda na CCM wanajua maana ya umoja ndiyo maana wanasema umoja ni ushindi, hivyo maneno ya kutugawa tusiyakubali, viongozi tushikamane,” alisema Lowassa.

Alitaja mbinu nyingine ya ushindi kuwa ni kwenda vijijini kutoa elimu kwa sababu utafiti unaonyesha kuwa CCM imekuwa ikishinda maeneo yaliyo nyuma katika elimu.

“Wakati tukiwa Dodoma kwenye ziara kuna vijiji mtu anakuambia mimi nampigia kura Nyerere (Hayati Baba wa Taifa Mwalimu  Nyerere), na akiona polisi anakimbia.

“Sasa kama mtu anakimbia akimwona polisi anawezaje kulinda kura?  Hivyo bila kwenda kutoa elimu vijijini hatuwezi kushinda,” alisisitiza Lowassa na kuongeza:

“ ‘There is no time left’ (Hatuna muda wa kupoteza),  muda uliobaki ni mdogo sana hatuna budi kuutumia vizuri kwa kuangalia wapi tulikosea na turekebishe vipi na tuongee kutoka moyoni tusiogopane.

“Tukosoane bila kusingiziana na tuone muda uliobaki tunafanya nini ili tushinde,” alisema Lowassa.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment