Sentahafu wa Simba, Method Mwanjale amechaguliwa kuwa mchezaji bora Desemba wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa msimu wa 2016/2017.
Beki huyo wa kati, aliwashinda
kiungo mshambuliaji wa Yanga, Haruna Niyonzima na beki Yakubu Mohamed wa
Azam FC. Mwezi Desemba ulichezwa raundi tatu za Ligi hiyo, huku Simba
ikicheza mechi mbili ugenini na moja nyumbani. Raundi hizo ni ya 16, 17
na 18.
Mwanjali aliiongoza Simba kushinda
mechi zote tatu, hivyo timu yake kupata ushindi wa asilimia 100 kwa
kunyakua pointi zote tisa, na kubaki katika nafasi yao ya kwanza kwenye
msimamo wa Ligi, nafasi ambayo walikuwa nayo wakati wanaingia raundi ya
16.
Pia katika raundi hizo tatu ambapo
Simba haikufungwa bao hata moja, Mwanjali alicheza dakika zote 270, na
bila kuonyeshwa kadi yoyote. Alichangia kwa kiasi kikubwa katika
mafanikio ya timu yake huku akiongoza safu ya ulinzi.
Kwa kushinda tuzo hiyo ya mchezaji
bora, Mwanjali atazawadiwa kitita cha sh. 1,000,000 (milioni moja) na
wadhamini wakuu wa Ligi hiyo Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom
Tanzania.
Wachezaji wengine walioshinda tuzo
za mchezaji bora kwa msimu wa 2016/2017 hadi sasa ni John Raphael Bocco
wa Azam (Agosti), Shiza Ramadhan Kichuya wa Simba (Septemba), Simon
Happygod Msuva wa Yanga (Oktoba), na Rifati Hamisi wa Ndanda (Novemba).
..………………………………………………………………………………………………
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
0 comments :
Post a Comment