NA BEATRICE LYIMO-MAELEZO
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
imevionya vyama vya siasa na wagombea wanaoshiriki katika uchaguzi mdogo
wa mbunge na madiwani kuheshimu na kuzingatia Maadili ya uchaguzi
katika kampeni zinazoendelea.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa
na Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar Hamid M.
Hamid alisema kuwa vyama au wagombea watakaokiuka maadili ya Uchaguzi
katika mikutano ya kampeni inayoendelea katika maeneo yenye uchaguzi
mdogo watachukuliwa hatua.
Alisisitiza kuwa kwa mujibu wa
kipendele cha 5.3 cha maadili ya uchaguzi, chama au mgombea atakayekiuka
maadili hayo katika jimbo au kata yenye uchaguzi mdogo atafikishwa
katika kamati ya maadili ngazi husika na kuchukuliwa hatua stahiki kwa
mujibu wa kipengele cha 5.10 cha maadili ya uchaguzi ya mwaka 2015.
“Katika kampeni zinazoendelea,
baadhi ya vyama vya siasa vimeanza kukiuka taratibu za kampeni na
maadili na kutumia fursa hiyo vibaya ikiwa ni pamoja na kuwasema
viongozi vya kitaifa, kutoa matamko ambayo kihalisia siyo ya kumnadi
mgombea wao,” alisema Jaji Mst. Hamid.
“Hivyo Tume inavitaka vyama na wagombea kuheshimu na kuzingatia maadili ya uchaguzi” alisema Mwakamu Mwenyekiti Huyo.
Aidha, Tume ya Taifa ya Uchaguzi
inatoa wito kwa wagombea na vyama vya siasa kufanya kampeni za
kistaarabu, amani na utulivu, wote wanahimizwa kuzingatia, Sheria za
Uchaguzi, Kanuni na Maadili ya Uchaguzi.
Kwa mujibu wa kipengele cha 2.1(m)
cha Maadili ya Uchhaguzi, Vyama vya Siasa, wagombea na wafuasi wao
wanatakiwa kufanya kampeni kwa kuzingatia misingi inayolenga kutangaza
Sera zao ambayo haijengi chuki, mfarakano na mgawanyiko wa jamii.
Kwa sasa vyama vya siasa na
wagombea wanashiriki kwenye kampeni za Uchaguzi Mdogo unaotarajiwa
kufanyika Januari 22 mwaka huu katika Jimbo la Dimani Zanzibar na kata
20 za Tanzania Bara.
0 comments :
Post a Comment