TAARIFA YA UOKOZI WACHIMBAJI MADINI WALIOFUKIWA NA KIFUSI- GEITA


RZ1
Wizara ya Nishati na Madini inapenda kuufahamisha  umma kuwa, Zoezi la kuwaokoa wachimbaji 15 waliofukiwa na kifusi  tarehe 26/01/2017 kwenye mgodi wa dhahabu eneo la kijiji cha Mawemeru, Nyarugusu Wilayani Geita limekamilika kwa mafanikio.
Ajali ya kufukiwa wachimbaji hao iliyohusisha Watanzania 14 na raia 1 wa China ilitokea kwenye leseni ya uchimbaji wa Kati wa madini ya dhahabu yenye Namba ML 492/2013 inayomilikiwa na Bw. Ahmed Mubarak Adam.
Chanzo cha ajali hiyo ilikuwa ni kuanguka kwa shaft ya mgodi huo na kufukiwa na kifusi wakati wachimbaji hao wakifanya kazi mgodini chini ya ardhi.
Tukio la uokoaji limefanikiwa leo tarehe 29/01/2017 ambapo wahanga hao walianza kutolewa shimoni kuanzia saa 5 hadi saa 5:30 asubuhi wote 15 wakiwa hai ingawa walikuwa wamedhoofika kiafya.  Aidha, wachimbaji hao wamepewa huduma ya kwanza katika eneo la ajali na kisha kukimbizwa Hospitali Teule ya Rufaa ya Geita. Hadi sasa wachimbaji hao wapo Hospitali wakiendelea na matibabu kwa uchunguzi zaidi wa afya zao.
Juhudi za kuokoa wachimbaji hao  ambazo zilifanyika kwa kufukua kifusi katika eneo la ajali zilianza mara baada ya tukio hilo kutokea. Uongozi wa Mkoa wa Geita ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa Meja. Jen.(Mst) Ezekiel E. Kyunga ulishirikiana na Wataalam wa Wizara ya Nishati na Madini na Kampuni za Madini mbalimbali mkoani Geita katika zoezi la ufukuaji kifusi ili kuokoa maisha ya wchimbaji hao. 
 Kampuni zilizoshiriki kwa kutoa mitambo na vifaa mbalimbali ni Kampuni ya Busolwa Mining Ltd; Kampuni ya Geita Gold Mine (GGM); Kampuni ya Nyarugusu Mining Ltd; Nsangano Mining Project; Metchell Tanzania Drilling; WAJA Hospital pamoja na wachimbaji wadogo wa Mkoa wa Geita wakiongozwa na Viongozi wa wachimbaji madini Wilaya, Mkoa na Taifa.
Akizungumza mara baada ya kuokolewa wachimbaji hao, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard amewashukuru wadau wote walioshiriki kwa hali na mali kufukua kifusi na hatimaye kufanikiwa kuwatoa wachimbaji chini ya ardhi wakiwa hai.
Dkt. Kalemani amewaomba Watanzania kuendelea na moyo huo pale majanga kama haya yanapotokea. Aidha, Dkt. Kalemani ameagiza shughuli zifungwe kwa muda wa siku tano kwenye mgodi uliopata ajali kuanzia tarehe 29/01/2017 ili kutoa nafasi kwa Kamishna wa Madini kufanya tathmini ya hali ya usalama wa mgodi na kutoa maelekezo kabla ya shughuli kuanza.
Vilevile, amewataka wachimbaji wawe watulivu katika kipindi ambacho tathmini ya hali ya usalama wa mgodi inafanyika na kuagiza Uongozi wa Mkoa kuhakikisha kuwa ulinzi unaimarishwa eneo la mgodi ili watu wasiweze kuingia na kuhatarisha maisha yao.
Pia, ameagiza ukaguzi wa kina ufanyike kwenye migodi mingine ya wachimbaji wadogo na ya kati eneo la Nyarugusu na kwingineko nchini ili kuhakikisha kuwa migodi inakuwa salama kwa wachimbaji wa migodi husika.
Imetolewa na;
KATIBU MKUU
WIZARA YA NISHATI NA MADINI
29/1/2017
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment