Hatima
ya wasaidizi wa kisheria pamoja na huduma ya msaada wa kisheria kwa
watu wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za mawakili, sasa iko mikononi
mwa Rais John Magufuli, baada ya Bunge kupitisha bila pingamizi Muswada
wa Sheria ya Huduma ya Msaada wa Kisheria wa mwaka 2016.
Waziri
wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe aliwasilisha muswada huo
bungeni mjini Dodoma juzi wenye lengo la kuwa sheria itakayosimamia na
kuratibu utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa watu wasiokuwa na
uwezo, kuwatambua wasaidizi wa kisheria na mambo mengine yanayohusu
utoaji wa msaada wa kisheria nchini.
Wakati
akitoa majumuisho waziri huyo, alikubali kuufanyia marekebisho baadhi
ya vifungu vya muswada huo baada ya kupokea maoni na ushauri kutoka kwa
wabunge mbalimbali ikiwemo Kambi ya Upinzani.
Alisema
muswada huo ukiwa sheria rasmi, utakuwa mkombozi kwa watanzania katika
eneo la sheria, kwani wengi wao hawajui kusoma na kuandika, lakini pia
wengi hawana uwezo wa kumudu gharama za kuajiri mawakili.
Alisisitiza
kuwa sheria hiyo, itasaidia pia kupambana na kusaidia wale wote
wanaoathirika na utekelezwaji wa mila na tamaduni potofu, zinazoendelea
kutekelezwa nchini.
“Kuna
mila na desturi zilizopitwa na wakati ambazo hazitambuliwi kisheria,
lakini bado mila hizo zinatumika na kuumiza watu wengi sana kwa mfano
masuala kama vile talaka, ndoa, watoto na mirathi haya ni mambo ambayo
kupitia sheria hii yatakuwa na ahueni sasa,” alibainisha.
Alisema
wananchi wengi wamekuwa wakikosa haki zao kisheria kutokana na kutokuwa
na uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya sheria; na mbaya zaidi sheria
zilizopo, hazitambui kama mhusika ana uelewa gani wa kisheria.
Pamoja
na kwamba, Dk Mwakyembe alichukua na kuyafanyia kazi baadhi ya maoni ya
Kambi ya Upinzani, yaliyowasilishwa bungeni hapo juzi na Waziri Kivuli
wa Katiba na Sheria, Tundu Lissu, alikosoa namna mbunge huyo alivyotumia
mifano ya Marekani katika suala zima la huduma ya msaada wa kisheria.
Alisema
anasikitishwa na kitendo cha mbunge huyo, kuifanya Mahakama Kuu ya
Marekani kuwa ni mfano wa kuigwa na Tanzania wakati mahakama hiyo ndio
iliyokuwa inaongoza kwa muda mrefu tangu miaka ya 1800 hadi 1960
kukandamiza haki za watu weusi.
“Kwa
muda mrefu kumekuwa watu humu ndani kazi yao ni ku google na kunukuu
Kiingereza tu humu ndani bila kuangalia context. Kwa mfano kipindi
alichotolea mfano mheshimiwa Lissu cha miaka 1800 kulikuwa na ubaguzi wa
rangi wa kupindukia,” alisema.
Alisema
mfano huo hauendani na hali halisi ya Tanzania, kwani nchi hiyo ilipata
Uhuru tangu mwaka 1961 na kuanzia hapo, kila mtu akiwemo mhindi,
mwarabu na mwafrika aliyepo nchini humo, alikuwa na uhuru hadi wa kupiga
kura.
Alipendekeza
wabunge kuhakikisha wanatumia mifano hai, inayoendana na hali halisi ya
Tanzania ikiwa ni pamoja na kutolea mifano ya wazee na waasisi waliopo.
“Wapo akina Mkwawa na kina Kinjekitile, hawa wamezungumzia mengi kuhusu
masuala ya haki,” alisema.
0 comments :
Post a Comment