Katibu
Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amesema kwa
sasa viongozi madalali wanaouza viongozi ndani ya chama hicho
hawatakiwi, huku akiwataka watafute kazi nyingine za kufanya.
Kutokana
na hali hiyo amesema sasa wamejipanga kuhakikisha CCM inaendelea
kutawala maisha yote huku akiwataka wenyeviti wa kata, wilaya na mikoa
kutokuwa sehemu ya malalamiko na badala yake wawe sehemu ya kusimamia
Serikali kama anavyofanya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Dk. John
Magufuli.
Kauli
hiyo aliitoa jana mjini Dodoma katika kilele cha maadhimisho ya miaka
40 ya CCM yaliyofanyika katika ukumbi wa Dodoma Convention Centre, ambao
unamilikiwa na chama hicho, ambapo Kinana awalitaka viongozi wa chama
hicho kuacha kuwa walalamikaji na badala yake wawe sehemu ya kuisimamia
Serikali katika kutimiza wajibu wake.
“Sasa
hatutaki kuwa na viongozi madalali ndani ya chama, kwa hiyo kama wapo
wajitafakari wenyewe. Ndiyo maana hata sisi tumekubaliana maadhimisho
sio sherehe lazima tuachane na tabia za sherehe ukisema sherehe itabidi
pia mlipane na posho jambo ambalo halikubaliki,’’ alisema Kinana.
Akielezea
sababu za kuendelea kushinda kwa chama hicho katika chaguzi mbalimbali,
Kinana alisema wamekuwa wakisimamia na kupigania haki za wananchi huku
akidai kwa sasa kuna viongozi wamekuwa madalali ndani ya chama hicho.
“CCM
ni chama chenye nguvu wana CCM wamekuwa wamoja na hiyo ndiyo imetufanya
tumekuwa tukiendelea kuaminiwa na wananchi na sababu zipo wazi ni
kusimamia na kupigania haki zao hakuna mwenye kauli wana CCM
wanamuunganiko.
“Sababu
nyingine ya kuendelea kuaminiwa ni uwepo wa demokrasia pana na yenye
kina kwa kila mwanachama kuwa na uhuru wa mawazo kwa kusema na hata
kushauri.
“Wanaoamua
ndani ya chama ni wanachama wakisema ndiyo ni ndiyo na wakisema hapana
ni hapana katika uchaguzi mwanachama ana haki ya kuchagua na ana uhuru
wa kuchukua fomu na kugombea,’’ alisema Kinana.
Alisema
kwa sasa vipo vyama vitatu pekee duniani ambavyo vinaoongoza kwa
maandiko mazuri na yenye tija ambapo alivitaja vyama hivyo kuwa ni
Chama cha Kikomunisti cha China, CCM na ANC cha Afrika Kusini.
Kinana
alisema mwaka 2015 chama hicho kilifanya tathmini kwa miezi 12 kuanzia
katika shina mpaka taifa lengo likiwa ni kupunguza urasimu na
umangimeza, ambayo iliwasaidia kujua upungufu na marekebisho
wanayotakiwa kufanywa.
Kuhusu suala la Serikali kuhamia Dodoma, alisema Serikali inatakiwa iungwe mkono japo alikiri kwamba mwanzo utakuwa mgumu.
Pia aliwataka wanachama wa chama hicho kuchagua viongozi wenye kazi zao katika uchaguzi mbalimbali utakaofanyika.
“Muwachague viongozi bora waadilifu wenye shughuli zao zisizotokana na CCM awe na shughuli ya kufanya,’ ’alisema.
Kwa
upande wake Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula, alisema CCM
kimehusika kwa asilimia kubwa katika kuleta amani na utulivu nchini huku
akiponda vyama vingine kuhusika na maandamano kila kukicha.
“Hivi
vingine ni vyama vya maandamano tu, amani na utulivu imeletwa na CCM
kumbukeni zamani tulikuwa tunasema chuo kikuu sasa hivi tunasema vyuo
vikuu Udom pekee wanamaliza wanafunzi 36,000,’’ alisema Mangula.
Maadhimisho
ya miaka 40 kwa mwaka huu yamekuwa ya aina yake ambapo yamehudhuriwa na
wabunge wote wa chama hicho, wakiwamo mawaziri wakuu wastaafu, John
Malecela na Mizengo Pinda pamoja na Spika wa Bunge, Job Ndugai.
0 comments :
Post a Comment