HISA za Uda zawa kaa la moto. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya jana
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe kufanya kikao
cha dharura na mameya, naibu mameya na viongozi waandamizi wa Ukawa
kujadili utata wa uuzwaji wa hisa za Shirika hilo la Usafiri Dar es
Salaam.
Mameya hao kutoka Dar es Salaam waliwasili mjini hapa juzi kwa nyakati
tofauti, kuhudhuria kikao hicho kilichofanyika jana kwenye ofisi za
Bunge.
Taarifa zilizotufikia zilieleza kuwa kikao hicho kilifanyika baada ya
kuibuka mvutano kati ya Serikali na uongozi wa Jiji hilo, linaloongozwa
na Ukawa kuhusu kuidhinisha Sh bilioni 5.8 za uuzwaji wa hisa asilimia
51 kati ya 100 kwa kampuni ya Simon Group.
Jumamosi iliyopita Baraza la Halmashauri ya Jiji hilo chini ya Meya
wake, Isaya Mwita kwenye kikao chake cha kawaida, lilishindwa kufikia
mwafaka wa kuzipangia matumizi fedha hizo kwa kilichoelezwa ni sawa na
kubariki ufisadi wa uuzwaji wa hisa hizo ambazo wanaona ni kiasi kidogo.
Kikao hicho kilifanyika baada ya agizo la Rais John Magufuli Januari 27 wakati akizindua mradi wa mabasi yaendayo haraka.
Katika agizo hilo, Rais alitoa siku tano kwa uongozi wa Jiji kuhakikisha
kiasi hicho cha fedha zilizolipwa na Simon Group kinapangiwa matumizi.
Lakini jana, Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema alisema nje ya
viwanja vya Bunge, kuwa amewaita mameya hao na manaibu wao ili
kuzungumzia sakata la hisa hizo.
“Nataka tupate msimamo wa pamoja ili wakazi wa Dar es Salaam wanufaike
na na Uda. Sioni sababu ya kuiua wala kulichukia shirika hili,” alisema.
Miongoni mwa mameya walioonekana jana kwenye viwanja vya Bunge ni Meya
wa Ubungo, Boniface Jacob ambaye alikiri kuitwa kuhudhuria kikao licha
ya kusisitiza kuwa hajui ajenda.
Mapema jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene aliwaeleza waandishi wa habari
kuwa hana la kusema juu ya kushindwa kugawanywa kwa fedha hizo.
0 comments :
Post a Comment